} });
 

Image result for Images of a group of young black men and women

Kijana unatakiwa ujitambue, ujielewe wewe ni nani na una kusudi gani katika maisha yako, Kupata uelewa wa kutosha juu ya kipindi cha ujana na umuhimu wake, Kuelewa changamoto zilizopo katika kipindi cha ujana na namna ya kuzishinda, Kujenga shauku, nia na kiu kwa kijana ili uweze kuishi maisha yenye mwelekeo na uweze kutimiza maono yako ukiwasaidia na wengine kumjua Mungu na maisha yako kwa ujumla wake, Kuwekeza uthamani na nguvu ya kipindi cha ujana kwa mtazamo wa Ufalme wa Mungu.
 
Yesu amefundisha katika Mathayo 6:33 kuwa tunapaswa kuutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, yaani wewe kama kijana unatakiwa kutoa kipaumbele, kuwekeza kwa nguvu zako zote katika kuutafuta Ufalme wa Mungu lakini ni muhimu kujua kuwa ni vigumu sana kukitafuta kitu usichokijua ndio maana ni muhimu sana kuujua kwanza.
Lakini kabla ya kufika mbali napenda pia kukusaidia kujenga msimamo katika fikra zako juu ya Ufahamu wa namna Mungu anavyokutazama kama kijana ili utakaposikia jambo lolote lisilolingana na mtazamo huu basi ujue ni maamuzi gani unapaswa kuyachukua.

Ni muhimu kujua namna Mungu anavyokutazama ili utakavyotazamwa na ulimwengu uwe na msimamo wenye nidhamu katika maamuzi yako, hii inategemeana na kama umeamua kusimama katika upande wa Mungu na kujitambua. Kumbuka upo Ufalme wa giza na Ufalme wa Nuru na ni Wajibu wako kuchagua upande upi wa kuutumikia na mimi binafsi nakushauri kuwa mchague Yesu Kristo aliye Mfalme wa wafalme wote, mkubali na umpokee na umfanye kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Waamuzi 6:12 Unamkumbuka Gedioni au ulishawahi kusoma habari zake, au je, ulishawahi kumsikia? Kama bado soma Waamuzi 6, na kama tayari tafakari tena kwa upya habari zake. Wakati wana wa Israeli wamefanya maovu, mara baada ya kukaa kwa Furaha na amani kipindi cha nabii mke alieyeitwa Debora, kwa kusahau ukuu wa Mungu wana wa Israeli wakarudia uovu wako. Ndipo Waamuzi 6:1 inapoanzia na kwa sababu hiyo alitakikana mtu wa kuwatoa tena wana wa Israeli toka katika mikono ya maadui zao wamidiani.

Ndipo kuanzia msitari wa 11, tunaona malaika wa Bwana akaenda kuongea na Gidioni akiwa anapepeta ngano yako na hivi ndivyo malaika alimwambia, “…BWANA yu pamoja nawe ee shujaa.” Kumbuka kipindi hiki Gidioni alikuwa bado kijana mdogo na kwa namna yoyote ile isingekuwa rahisi kwake kujiona ni shujaa kama malaika alivyomuita. Kimsingi, Mungu alimuona kuwa yeye ni shujaa pamoja na ujana wake kwa maana ushujaa wake usingetokana na umbo la mwili wake bali na kuwa na  mahusiano mazuri na Mungu wake.
Kijana, wewe ni shujaa na ushujaa wako hautokani na:
·         Elimu yako
·         Ukoo wako
·         Nguvu za mwilini mwako
·         Mali na fedha ulizonazo
·         Umaarufu ulionao
·         Wala historia nzuri au mbaya ya maisha yako, hapana.

Wafilipi 4:19
Kijana, unayaweza mambo yote ndani ya Kristo, unayaweza mambo yote katika wewe akutiae nguvu Yesu Krsito.
Mafanikio yako na ujasiri wako ni huu, kwamba katika Kristo Yesu wewe unaweza kufanya jambo lolote. Kuyaweza mambo yote katika Kristo kuna uhusiano na nguvu zake tu na wala sio ukoo wako, familia uliyozaliwa au mambo magumu yaliyotokea kwako Wafilipi 4:19. Ni Mungu anaekupenda na kukuwazia mema siku zako zote za maisha yako, huu ndio uhakika wa mafanikio yako na kushinda kwako bila kujali wewe ni nani. Huenda wazazi au ndugu au marafiki wanakubeza na kukudharau kuwa huna kitu, uchaguzi ni wako, aidha uwasikilize hao ambao mwisho wao ni siku chache zinazohesabika au uamue leo kuishi kwa kutii na kulifuata Neno la Mungu. Zaburi 119:9.

Ujasiri na ushujaa wako umefichwa ndani ya kujitambua katika Mungu, yaani kumjua Mungu katika mahusiano yako wewe na Yesu na kujijua wewe ni nani kwa kadri Mungu anavyokufunulia katika Kristo, thamani yako pia imefichwa huko, Mungu anakuona na anakuita wewe kuwa ni shujaa kwa sababu anauona ushujaa ndani yako unaotokana na wewe mwenyewe. Waamuzi 6 Soma habari za Gidion
Kwa lugha nyingine, si kwa uweza wala si kwa nguvu zako wewe ni shujaa bali kwa nguvu na uweza wa Mungu mwenyewe katika Roho Mtakatifu unaokufanya wewe kuwa shujaa. Najua, kutokana na historia za maisha ya vijana wengi, inaweza isiwe rahisi sana kukubali ukweli huu kwamba wao ni mashujaa au kwamba wao ni wenye hekima.

Pamoja na kukataa huku bado nasisitiza kuwa wewe kijana unayenisikiliza ni shujaa na anayesema na kutaka hayo ni Mungu, mimi nimerudia tu kukukumbusha kuwa wewe umetajwa na Mungu wako kuwa wewe ni shujaa. Ni mashujaa tu wanaoweza kufanya mambo makubwa na ya ajabu na wengi wao ndio wameandikwa katika vitabu vya historian na wewe hata kama hujaandikwa bado, fahamu kuwa umechorwa kwenye kitanga cha mkono wa Mungu ambaye ndiye mratibu wa historia zote.

Ni kutokana na uhalisia huo huo, ndiyo maana hata Gidioni mwenyewe haikuwa rahisi kwake kukubali alipoitwa na malaika. Angalia jibu lake baada ya malaika kumuita wewe ni shujaa, Gidioni akamwambia malaika kuwa kama ni kweli Bwana yuko pamoja naye mbona mambo mabaya yanawatokea? Na pia yako wapi matendo makuu ya Mungu kati kati yao? Na wewe unaweza ukajiuliza pia au kumuuliza Mungu, kama ni kweli Mungu anakupenda kwanini umezaliwa kwenye familia masikini, yenye maisha magumu nk. Lakini nikwambie huo ni wakati tu.

Kwa ujumla wake, Mungu anakutazama wewe kijana katika sifa au pande tatu:

1.      Kila kijana ana nguvu
2.      Kila kijana anao uwezo wa kumshinda shetani katika Kristo
3.    Ukiwa kijana ndio wakati pekee ambao Neno la Mungu linaweza kupata nafasi nzuri ya kukaa ndani ya moyo wako.

NINI MATARAJIO YA MUNGU KWA VIJANA?

1Yohana 2:14 “…. Nimewaandikia ninyi,vijana kwa sababu mna nguvu,na neno la Mungu linakaa ndani yenu ,nanyi mmeshinda yule mwovu.”Mungu anao mtazamo wake binafsi juu ya kila kundi la watu chini ya jua,.Na kila kundi mfano wa wamama,wajane,watoto,vijana kuna mambo fulani ambayo Mungu anatarajia kila kundi litatekekleza. Mungu anazungumza na vijana na kusema nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu moja mna nguvu, mbili neno la Mungu linakaa ndani yenu, na tatu mmemshinda yule mwovu.

Nguvu zinazozungumziwa hapa ni nguvu, uweza wa Mungu wa kukusaidia kutekeleza maagizo yake. Na kwa sababu hiyo basi kuna matarajio ya Mungu kwa hao vijana. Sasa nikueleze kijana nini Mungu anatarajia/anategemea kwamba utafanya sawasawa na nafasi aliyokupa mbele zake na uwezo aliokupa. Matarajio ya Mungu kwa vijana ni kama ifuatavyo:

*Moja, Vijana wauteke ufalme wake.
Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”. Biblia inapozungumzia ufalme wa Mungu inazungumzia habari za utawala wa Mungu. Hivyo ni matarajio ya Mungu kwamba popote pale vijana walipo basi watatengeneza mazingira ya Mungu kutawala katika maeneno waliyopo iwe darasani, Chuoni, Kazini, Kanisani nk na hii ni kwa sababu wana nguvu. Sikiliza, vijana wana nguvu na ufalme unapatikana kwa nguvu, maana yake Mungu anatarajia vijana watumie nguvu zao kuuteka ufalme wake na kuuruhusu uchukue utawala duniani.

*Mbili, Vijana warejeshe urithi na mali za wana wa Mungu zilizotekwa.
Mwanzo 14:13-16. “…Akawapa silaha vijana wake, walozaliwa katika nyumba yake,watu mia tatu na kumi na nane, akawafuata mpaka Dani”. Hizi ni habari za Ibrahamu aliyeenda kumuokoa nduguye Lutu baada ya kuwa ametekwa. Ili kurejesha urithi wao na mali zao ilimbidi Ibrahimu atumie nguvu kazi ya vijana. Na hivyo hata leo Mungu anatarajia kwamba vijana wasimame kwenye nafasi zao na kupambana kwa ajili ya afya, ulinzi, uchumi, uponyaji, mafanikio ya watu wake. Hebu jipe dakika moja halafu tazama jinsi shetani anavyotesa watu na kudhulumu afya zao, ujana wao, ndoa zao, uchumi wao nk.Ni nani watakaorejesha hali nzuri, urithi huu kwa wana wa Mungu , ni Mungu kupitia Vijana.*Tatu, Vijana wasikosee katika kufanya maamuzi ya kuoa au kuolewa.
Mithali 5:18 “Chemichemi yako ibarikiwe; nawe umfurahie mke wa ujana wako”. Sikiliza, Mungu anataka ndoa yako iwe ni ndoa ya mafanikio na ya furaha, maana yake ni ndoa ambayo hautaijutia kwamba kwa nini nilimuoa au kuolewa na huyu mtu. Sasa basi, ili ndoa yako iwe ni ya furaha na amani, ni lazima huyo mwenzi wako umpate kwa uongozi wa Mungu mwenyewe. Na mtazamo wa Mungu kwa vijana ni huu, vijana hawatakosea kufanya haya maamuzi kwa sababu tayari Neno la Kristo limejaa kwa wingi ndani yao. Kumbuka Neno la Kristo ni taa ya miguu yangu.

*Nne, vijana wawe wasuluhishi wa matatizo katika jamii na taifa.
Mithali 1:4 “Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari”. Leo ndani ya kanisa, jamii tunayoishi na katika taifa kwa ujumla yapo matatizo mbalimbali ya kiroho, kiuchumi, kijamii, kiafya, kimwili, kibiashara, kindoa nk. Sasa Mungu anatarajia vijana ndio watumike kusuluhisha matatizo haya mbalimbali katika jamii kwa sababu ya wingi wa neno la Kristo ndani yao. Hii ina maana mtu mwenye Neno la Kristo kwa wingi ndani yake basi maana yake ana upeo mkubwa wa kuelewa mipango na njia za Mungu za kuwatoa watu wake kwenye matatizo yanayowakabili. Kwa hiyo basi, tumia fursa hiyo kutatua matatizo hayo na kusuluhisha kwa sababu ya kujua mawazo na njia za Mungu za kuwatoa watu wake kwenye shida walizonazo.

*Tano, vijana walitumikie kusudi lake la kuhubiri habari njema.
 Mathayo 28:19 “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu”. Sikiliza, kwa sababu ya nguvu ambayo Mungu amewekeza kwa vijana basi ni matarajio yake kwamba wewe kama kijana utatumika kuwaeleza watu wengine habari njema za Yesu Kristo ziletazo amani. Ni matarajio yake kwamba vijana watapita nyumba kwa nyumba, mtaa hadi mtaa wawaambie wengine kuhusu huyu Yesu, wakiwafungua waliofungwa na kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika. Naamini haya matarajio matano ya Mungu kwako kama kijana mwenzangu basi yatakusaidi sasa kukaa kwenye nafasi yako ili Mungu ajivunie kuwa na kijana kama wewe.

KIJANA USIKUBALI KUHARIBU UJANA WAKO.

Neno ''KUPENDA'' limekuwa msamiati mgumu sana kwa vijana wa leo, shetani amefanikiwa kwa asilimia 90 kuwanasa vijana wengi na kuwaangusha katika dhambi, akitumia msamiati huu NAKUPENDA.
2 Timotheo 2:22 '' Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi. ''

-Kwa Wasichana Kusumbuliwa Na Vijana Wasio Na Hofu Ya MUNGU Limekuwa Ni Jambo La Kawaida. Kwao Ni Kama Vile Usivyoweza Kuwazuia Ndege Wasiruke Juu Ya Kichwa Chako. Lakini Licha Ya Hayo Mimi Naamini Kila Msichana Anaweza Kuwazuia Ndege Hao Wasijenge Viota Kwenye Nywele Zake. Dada Najua Umeshindwa Kuwazuia Ndege Kuruka Juu Ya Kichwa Chako Lakini Naamini Unaweza Kuwazuia Ndege Hao Kujenga Kiota Kwenye Kichwa Chako, Shika Utakatifu Na Utunze Wokovu Wa BWANA YESU Kama Pesa.

-Mabinti jizuieni na uasherati, jizuieni maana nyie ndio mara nyingi mnafuatwa. upendo hauko katika ngono.
1 Kor 5:10 Biblia inasema ''Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.''

-Wazinzi na wenye kutamani tunao katika mazingira yetu iwe ni nyumbani au ni kazini lakini ni jukumu lako binti kukataa kutumiwa kama chombo cha kujifurahishia wadhalimu. Kataa dhambi ya uzinzi, ogopa dhambi ya uzinzi, ikimbie dhambi ya uzinzi na usifanye dhambi ya uzinzi.

BWANA YESU Anakupenda Sana Na Hataki Ukose Uzima Wa Milele Kwa Sababu Ya Hao Ndege Wanaoruka Juu Ya Kichwa.

Ufunuo 21:8 '' Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.''

-Kumbe katika watakaopelekwa jehanamu na wazinzi wamo.

-shetani analeta kila mitindo ya mavazi na mapambo ili tu kuwanasa vijana katika dhambi ya uasherati.
-Uzinzi ni moja ya dhambi zinazowakosesha wengi.

-Nduguyangu, uzinzi wa muda mfupi unaweza kukupeleka kabisa jehanamu kama hukupata nafasi ya kutubu, na sio wote wanaopata nafasi ya kutubu na kugeuka.

-Uzinzi na uasherati ni dhambi ving'ang'anizi na ndio maana shetani huitumia sana ili kuwaangamiza maelfu ya vijana, uzinzi unamfanya shetani anapata nafasi ya kukutawala.

Kijana/binti kupitia ujumbe huu nakuomba badilika. Na kama umeona imekuwa ngumu mweleze mchungaji wako akusaidie na kukuombea maana wengi hadi wana majini mahaba.

Mithali 6:32-33 '' Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. ''

-Mvulana Leo Akimwambia Msichana "NAKUPENDA" Maana Yake Hasa Ni " NATAMANI KITU, SIO WEWE MWENYEWE BALI KITU KUTOKA KWAKO, SIWEZI KUNGOJA, NATAKA KUWA NACHO SASA HIVI, BILA KUCHELEWA. SI KITU NINI KITAKACHOTUKIA BAADAE. NINAANGALIA WAKATI HUU, NINAYO HAJA KWAKO ILI KUZITULIZA TAMAA ZANGU, WEWE NI CHOMBO TU CHA KUNIFIKISHA KWENYE SHABAHA YANGU, NATAKA KUWA NA WEWE MUDA HUU"
Hiyo Ndio Maana Ya Neno "Nakupenda" Kwa Maisha Ya Leo Kwa Vijana Wengi. Maana Halisi Ya Kijana Kama Huyo Ni Hii "NINAJIPENDA MIMI MWENYEWE PEKE YANGU TU, KWA SHABAHA HIYO NAMTUMIA MSICHANA KUKAMILISHA KUJIPENDA KWANGU".

Wasichana Wengi Nao Hujikuta Wakiingia Kwenye Upendo Huu Feki Na Kuingia Dhambini.

Vijana wenzangu Tambueni Neno Hili Kwamba MUNGU Atawahukumu Adhabu Ya Jehanamu Wazinzi Na Waasherati, Waebrania 13:4 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. '',

BWANA MUNGU Anawaonya Wanadamu Kila Leo Ili Waache Uovu Huu. Dhambi Hii Ndio Ilisababisha Sodoma Na Gomora Kugeuka Matanuru Ya Moto Na Kuwateketeza Wanadamu Wote Isipokuwa Lutu Na Familia Yake

1 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. ''

Upendo Wa Kweli Haukamiliki Isipokuwa Katika Ndoa Takatifu Mlioingia Bila Dhambi. Kwa Hiyo Mvulana Asitaje Lile Neno Kubwa La Kusema "NAKUPENDA" Kwa Msichana Asipokuwa Na Nia Ya Kufunga Nae Ndoa Tena Asiseme Neno Hilo Huku Akiwa Na Mpango Wa Kufunga Ndoa Miaka 10 Ijayo Bali Miezi Kadhaa Ijayo.

Yakobo 4:4 ''Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU.''Wazinzi ni adui wa MUNGU, Ukianguka kwenye dhambi ya uasherati au uzinzi kwa sababu tu ulidanganyika na neno ''nakupenda'' basi wewe unakuwa adui wa MUNGU hadi utakapotubu.

Kijana na kiume au wa kike tambua kwamba wewe ni wa thamani sana mbele za MUNGU, Tunza uthamani wako na mwili wako bila kufanya uasherati.

Maombi yangu MUNGU akupe kinga kwa kila hatari iliyo mbele yako, akupe baraka kwa kila jambo jema unaloliwaza na kulipanga kwa ajili ya maisha yako ya baadae yakiwemo maisha ya ndoa, BWANA akupe jibu katika ombi lako la kumpata mwenzi wa maisha mwenye hofu ya MUNGU, BWANA YESU akupe tabasamu kwa kila chozi unalolia ukimuomba akupe mme/mke mwema, akujalie afya njema, furaha,amani na upendo. Nguvu ya MUNGU ikasimame na wewe katika magumu unayopitia hadi ushindi wako na maadui zako kuanzia walio ndani hadi walio nje kwa jina la YESU KRISTO washindwe.

BWANA YESU akuondoe kwenye maagano ya ukoo na mizimu yanayokuzuia kuoa au kuolewa. MUNGU akawafunge waliokufunga, wawe mateka waliokufanya mateka, wateseke wao waliokutesa, waliokufungia uchumi wafungwe wao.

Mungu wa Mbinguni akubariki sana kijana/binti ambaye umesililiza somo la leo na  MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.N kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho Kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.

MUNGU akubariki sana.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top