Dhambi ni uasi (1 YOHANA 3:4). Neno "dhambi" linatokana na neno la Kiyunani "HARMATIA" ambalo maana yake katika Kiingereza ni "MISSING THE MARK", kwa Kiswahili tungesema ”KUIACHA ALAMA" au "KUUACHA MSTARI".
Alama hii au mstari huu ni Neno la Mungu (ZABURI
119:9).
Dhambi ni zaidi ya kuua, kusema uongo, kuzini au kufanya uasherati, kuiba, kutotii wazazi (MATHAYO 19:18-19).
Dhambi ni zaidi ya kuua, kusema uongo, kuzini au kufanya uasherati, kuiba, kutotii wazazi (MATHAYO 19:18-19).
1. Madhara ya Awali ya dhambi kwa Wanadamu
Kila dhambi unayotenda ina madhara sasa katika maisha unayoishi na
maisha yajayo baada ya kifo. Kama wewe unafanya dhambi basi ujue umekufa kiroho
na mbele za Mungu wewe ni kama marehemu, Adamu alipoteza uhusiano wake na Mungu
kwa sababu ya dhambi, na akafukuzwa kwenye bustani ya Mungu kwa sababu ya
dhambi; na tumaini la kurejea katika mahusiano na Mungu likapotea; Kwa hiyo
hakuna dhambi isiyokuwa na madhara, kama Warumi 6:23 inavyosema “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali
karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Kila dhambi wanadamu wanazotenda zinawapelekea kwenye uharibifu, hakuna
dhambi mtu anayotenda isimpelekee kwenye uharibifu. Mfano wa madhara ya dhambi
katika maisha ya mtu ni kama vile mimba zisizotarajiwa, kupata magonjwa ya
zinaa kama ukimwi, kufukuzwa nyumbani kwa sababu ya mimba, ndoa kuvunjika;
kisasi kati ya mtu na mtu, vita, njaa, n.k; haya ni baadhi tu ya madhara ya
dhambi anayokabiliana nayo mtu anapoishi hapa duniani; Kwa hiyo hakuna dhambi
yeyote utakayotenda ukiwa hapa duniani; isiweze kukuathiri; hata kama unasema
uwongo kuna madhara ya kusema uwongo, kwenye Biblia kuna watu walikufa tu kwa
sababu walidanganya mbele za Mungu; kila dhambi unayotenda inakupelekea kwenye
kifo. Inakuweka mbali na Mungu.
2. Madhara ya Dhambi kwa Mwanadamu Baada ya Kifo
Waebrania 9:27 inasema “Na
kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa
hukumu;” Baada ya kifo hakuna tena kutubu dhambi, kama wewe
ulikuwa wenye dhambi utakwenda motoni. Tutaenda kuangalia baadhi ya dhambi,
kama zipo kwenye maisha yako basi ujue ya kwamba hautaurithi ufalme
wa Mungu endapo hautatubu, kuziacha na kumgeukia Mungu.
Neno la Mungu linatuambia kwenye 1 Wakoritho 6:9-10 inasema “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi
ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala
waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala
watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.”
Neno la Mungu linatuambia kwamba watu wote wadhalimu hawataurithi ufalme
wa Mungu, wote wanaofanya dhambi ni wadhalimu na ndio maana anasema kwamba, Au hamjui ya kuwa wadhalimu
hawataurithi ufalme wa Mungu? hapa alikuwa akizungumza na
watu waliokoka, akiwaonya wale wanaotenda dhambi kanisani,
inawezekana wewe umeokoka lakini bado unaendelea na dhambi zako; jua watu wa
namna hii hawataurithi ufalme wa Mungu.
Waasherati Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Kama wewe ni muasherati hautaurithi ufalme wa Mungu, uasherati hauwi kwa
matendo tu, hata kwa mawazo, unapowaza unazini na dada/kaka fulani mawazoni tayari
umefanya uasherati. Na siyo mawazoni tu hata pia kwa maneno, unapomtakia mdada/mkaka
neno la kiasherati lolote, umeshatenda dhambi hiyo. Mtu mwasherati ni yule
ambaye hajaoa wala kuolewa. Kama hajaoa au kuolewa na ukalala na mtu mwingine
huo ni uasherati.
Wafiraji/Walawiti Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Inawezekana wewe unafanya ufiraji kwa mtu yeyote. Mwanaume anapofanya
ngono na mwanaume mwingine ni ufiraji, na hata kama anafanya ufiraji kwa mkewe
ni machukizo kwa Mungu, na wote wanaotenda mambo hayo watakwenda motoni.
Wevi Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Wote wanaoiba mali za watu wengine hawataurithi ufalme wa Mungu. Mtu
yeyote mvivu kufanya kazi ni lazima atakuwa mwizi, Watu wote wavivu ni wezi.
Watamanio Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Neno la Mungu linasema katika Mathayo 5:28 inasema “lakini mimi nawaambia, Kila mtu amtazamaye
mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake” Hapa
alikuwa anamaanisha nini? Kwamba kuna dhambi zingine zinafanyika katika mawazo,
na zingine zinafanyika wazi wazi. Yale yote mabaya unayoyafikiri moyoni mwako
juu ya mwingine tayari unakuwa unatenda dhambi, na siyo mpaka utende kwa
matendo. Kwa mfano unapowaza kuua mtu mwingine ndani yako, hata kama haujaua;
tayari hiyo ni dhambi, hata kama baadaye roho ya huruma ikikujia tiyari mbele
za Mungu ni dhambi. Hata kama umetamani kitu fulani na ukawaza uovu juu yake ni
dhambi, unapaswa kukataa mawazo yote ya kiasherati ndani ya moyo wako
na siyo kuyakubali, hata kama msichana/kijana huyo unamuona kuwa
mzuri, ibilisi anaweza kumtumia huyo kukuingiza dhambini. Wakati mwingine mtu
anaweza kukuchukia hata kama hakuonyeshi kwa nje. Lakini ndani ya moyo wake
hapendi hata kukuona. Hizo ni dhambi, zinazofanyika ndani ya mtu, hazionekani
kwa nje.
Walevi Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Watu wote wanaokunywa pombe, wote wanaotumia madawa ya kulevya, wote
wanaovuta bangi, sigara na mihadarati, kubell na wanaovuta gundi, watu hawa
wote hawataurithi ufalme wa Mungu. Watu wote walevi ni waabudu sanamu. Kwa
mfano labda wewe ni mvuta bangi, ngoja nikupe ushuhuda mfupi, kijana mmoja
alipokuwa sekondari alijiingiza katika vikundi vya uvutaji bangi shuleni, na
alikuwa na Imani kwamba akishavuta bangi akisoma anaelewa vizuri na pia inampa
ujasiri wa kutenda mambo yake mengine. Kuna wengine wakitaka kufanya fujo au
kugombana na mtu wanasema ngoja nikamywee pombe mtu huyu ili nikirudi tugombane
vizuri, au mwingine akishakunywa anajisikia amani ndani ya moyo wake au
vyovyote vile au anapoteza mawazo. Huko kote ni kujidanganya, amani ya kweli
inapatikana kwa Yesu na siyo kwa kunywa pombe. Ambayo kila siku utahitaji ili
uwe na amani. Hawa wote wanamwabudu mungu pombe na bangi ndiyo miungu yao.
Watukanaji Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Watu wote wanaotukana hawataurithi ufalme wa Mungu. Yesu alisema kwenye
Mathayo 5:22, inasema “Bali
mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu
akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza, na mtu akimwapiza itampasa jehanamu ya
moto” Kuna watu wengine wana tabia ya kuwaambia wengine matusi
makali n.k wote wanaofanya hivyo watakwenda motoni. Kuna watu wengine hawewezi
kuongea bila kuweka tusi katika mazungumzo yao wakati mwingine mbele ya watu
wazima, na vijana wengi wanaona ni kawaida, hayo ni matusi na ni maneno ya aibu
ambayo hayapaswi kutamkwa.
Wanyang’anyi Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Watu wote wanaonyang’anya mali za wengine hawataurithi ufalme wa Mungu.
Unakuta mtu ananyanyasa watoto yatima kwa kuwadhulumu mali zao walizoachiwa na
wazazi wao, watu hawa watakwenda motoni, watu wanaodhulumu wengine kwa kutoa
rushwa ili wapewe mali ya mtu bila ruhusa yake. Wote ni wanyanganyi
hawatakwenda mbinguni.
Ndugu yangu mpendwa tumeongea mengi sana, ila naomba kwa ujumbe huu
mfupi embu chunguza maisha yako na kama kuna dhambi yeyote unayofanya kati ya
nilizotaja basi umepotea njia, tubu dhambi yako na kuamua kuiacha kabisa.
Wagalatia 5:19-21 inasema “Basi
matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya
sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda,
ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama
nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu”
Kwenye hiki kifungu tunaona wazi matendo ya mwili kama yanavyoelezewa,
wote wanaotenda hayo hawataurithi ufalme wa Mungu. Kama wewe unajihusisha
katika moja ya hayo hautaurithi ufalme wa Mungu.
Wachafu Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Hapa ana maana kwamba watu wote wanaofanya punyeto au kujichua au usagaji
na matendo mengine ya kingono kama kulala na wanyama kama mbwa, mbuzi, kuku na
mengineyo, wote wanaofanya mambo hayo machafu na watu wote wanaofanya ngono na
ndugu zao na hata baba zao na mama zao wote ni wachafu mbele za
Mungu, hawataurithi ufalme wa Mungu (Kumb 27:20-23).
Wanaofanya Ufisadi Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Ufisadi ni aina ya wizi ambao sio wa waziwazi. Wote wanaofanya hayo
hawataurithi ufalme wa Mungu.
Wanaofanya Uadui Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Inawezekana kwenye maisha yako una uadui na ndugu zako, marafiki zako au
mtu yeyote labda kwa sababu alikufanya ubaya fulani, au alikuwa anakunyanyasa,
hiyo tayari inakuonyesha kwamba haustahili kuurithi ufalme wa Mungu.
Walio Wagomvi Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Kama wewe ni mtu unayependa kugombana na wengine kwa kitu kidogo au
labda kwa sababu umeonewa au umedhalilishwa kwa sababu ya kitu fulani na
matokeo yake ukaanza kutoa lugha chafu na hata kupigana na wengine, hautaurithi
ufalme wa Mungu.
Wenye Wivu Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Kuwa na wivu ni kitu kibaya sana, wengine wameoneana wivu mpaka wamefika
hatua ya kuuana wao kwa wao. Hatupaswi kuwa na wivu eti kwa sababu fulani
amefanikiwa au fulani ana hichi au kile, tunachopaswa ni kuridhika na tulivyonavyo,
kama huna mshukuru Mungu.
Wenye Hasira Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Hupaswi kuwa na hasira, kwa sababu labda umesemwa vibaya au umetukanwa,
au umedhalilishwa na mtu, bali mshukuru Mungu katika kila jambo. Kama wewe ni
mtu mwenye hasira jua kwamba hutaurithi ufalme wa Mungu. Maana hasira wakati
mwingine humpelekea mtu kufanya mambo ambayo ni ja kijinga kabisa, na baada ya
hasira kwisha mtu huyu anaanza kujilaumu kwa nini ametenda hayo. Na mtu mwenye
hasira Biblia inamuita mpumbavu. (Mhubiri 7:9 Usifanye haraka kukasirika rohoni
mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu).
Wenye Fitina Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Kuna watu wana tabia za kusema mambo ambayo si ya kweli kwa wengine na
wanakuwa tu na lengo la kuwafanya watu wagombane labda kwa sababu tu ya kitu
kidogo. Watu hawa hawataurithi ufalme wa Mungu.
Walafi Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Utakuta mtu anakula mpaka anavimbiwa na wakati mwingine anashindwa hata
kufanya shughuli zingine, huo ni ulafi, kula zaidi unavyopaswa kula
ni ulafi, na chochote unachofanya zaidi ya vile unavyopaswa kufanya huo ni
ulafi, kwa mfano kuna watu ni walafi wa madaraka, utakuta mtu huyo mmoja ana
nafasi zaidi ya moja kwenye ofisi hiyo hiyo moja. Wengine ni walafi wa pesa,
walafi wa usingizi, yaani mtu analala hata mpaka masaa 12 kwa siku, watu hawa
ni walafi na hawataurithi ufalme wa Mungu.
Wenye Faraka Hawataurithi Ufalme Wa Mungu
Wote wenye roho za kuwatenga wengine kwa sababu ya kabila lake, dini
yake, n.k watu hawa hawaturithi ufalme wa Mungu. Tukija kwenye jamii tunaona
watu wengi wanatengwa na watu labda kwa sababu ya Imani yao, na hata wakati
mwingine jinsia fulani inatengwa kwenye jamii hiyo, Labda hiyo jamii inaona
kwamba jinsia hii haistahili kufanya kazi fulani, au kujihusisha kwenye elimu
au kitu fulani. Hiyo ni roho ya matengano.
Na tukisoma tena kwenye kitabu cha Ufunuo 21:8 linasema “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na
wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu
yao ni katika lile ziwa la moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.” Nitaelezea
hichi kifungu kama ifuatavyo:
Waoga Watakwenda Motoni
Kama wewe ni muoga utaenda kwenye ziwa la moto, inawezekana umesikia
injili na hutaki kuokoka kwa sababu ya kuogopa kuuziwa na familia au kwa sababu
ya kuogopa kutengwa na jamii inayokuzunguka, au kwa sababu ya maisha uliyonayo
ni magumu au kwa sababu ya kazi unayofanya au kwa sababu ya mtu fulani, dini
n.k basi hautaurithi ufalme wa Mungu, Unakuta mwingine alikuwa anafanya kazi
bar, kwa hiyo anaona kama akiokoka itabidi kuacha kazi hiyo, kwa hiyo anaachana
na habari za kuokoka.
Wasioamini Watakwenda Motoni
Inawezekana wewe huamini kama Yesu ni Bwana na Mwokozi wako, huamini
kama kweli alikuja na alikufa kwa ajili ya dhambi zako na alifufuka na anaishi
milele, pia hautaona ufalme wa Mungu, inawezekana wewe huamini Neno la Mungu,
unaona ni kama stori ambazo hazina ukweli wowote, watu hawa hawataurithi ufalme
wa Mungu.
Wanaochukiza Watakwenda Motoni
Inawezekana wewe ni mtu unayechukiza watu wengine kwa kuwafanyia mambo
yasiyofaa, kuna mambo mengine sio mazuri, unapomfanyia mtu kitu kwa lengo la
kumfanya akasirike tiyari hilo ni kosa mbele za Mungu, Na ndio maana wote
wanaopenda kuwafanyia wenzao yasiyofaa hawatauona ufalme wa Mungu. Watenda
dhambi wote ambao hawataki kuachana na dhambi ni machukizo mbele za Mungu. Au
kufanya jambo lolote ambalo unajua hili nitakapolifanya huyu atachukizwa,
hawataurithi ufalme wa Mungu.
Wauaji Watakwenda Motoni
Kwa mfano wewe umewaza juu ya kumuua mtu kwa kumchoma kisu au kumkata
panga au kwa vyovyote ndani ya moyo wako, tayari hiyo ni dhambi, hata kama
hujaua kimwili, hapo kiroho umeua, na watu wote wanaoshiriki kutoa mimba pia ni
wauaji hawataurithi ufalme wa Mungu. Hata kama wewe ulishauri mimba itolewe na
hata daktari mwenyewe, wote ni wauaji. Na wote wanaofanya dhambi ni wauaji kwa
namna moja au nyingine.
Wazinzi Watakwenda Motoni
Mzinzi ni mtu ambaye ameoa/ameolewa, lakini anatembea na wanawake/wanaume
wengine nje, naye pia hataurithi ufalme wa Mungu. Na uzinzi sio tu unafanyika
kwa matendo bali pia kwa mawazo. Unaweza kulala na mke/mume wa mwingine kwa
njia ya mawazo, hao pia hawatauona ufalme wa Mungu.
Wachawi Watakwenda Motoni
Wote wanaologa, wanaopiga bao, wanaosoma nyota, wanaotumia utambuzi,
wote wanaochanja chale, wanaotumia hirizi, wanaosoma alama za mikono, na wote
wanaowaendea wenye pepo na waganga, watu hao wote hawatauona ufalme wa Mungu.
Kama wewe ni mtu anayekwenda kwa waganga kwa ajili ya kutaka mafanikio kielimu
na utajiri nawe pia ni mchawi. Yule aliyekupa uchawi na wewe uliyepokea wote ni
kitu kimoja (Mambo ya Walawi 19:31).
Wote Wanaoabudu Sanamu Watakwenda Motoni
Wote wanaochonga sanamu yeyote ile kwa lengo la kutumia kwenye ibada ni
waabudu sanamu, iwe ni sanamu ya Yesu, ya nabii fulani au ya ng’ombe au ya
chochote. Ni waabudu sanamu. Kama wewe unapenda jambo fulani zaidi ya Mungu na
uko tayari hata kutoa sadaka ya Mungu kwa ajili ya hicho wewe ni mwabudu
sanamu, kama wewe unaogopa kuokoka kwa sababu ya binti/kijana fulani basi wewe
ni mwabudu sanamu.
Waongo Wote Watakwenda Motoni
Haijilishi ni uongo wa namna gani, unaosema, kama wewe ni muongo hautauona
ufalame wa Mungu, wapo wale wanaosema uongo kuwasaidia wengine,
kuwaokoa wengine, wanaosema uongo kama kutumia hekima, Hekima yote ya dunia hii
ni upuuzi mbele za Mungu, Wote wenye hekima za kiduniani kwa kutumia uwongo
wamepotea milele, falsafa zako hazitakuasidia chochote, wala kusoma kwako
kwingi, utakuta watu wengi walioelimika ni watenda dhambi waliojificha, japo
moja kwa moja hakuonyeshei kisu, lakini moyoni mwake ameshakuchoma na hicho
kisu. Wamesoma lakini bado hawaelewi.
Na ukisoma tena kwenye kitabu cha
Warumi 1:18-32 inasema “Kwa maana
ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka Mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa
wanadamu waipingao kweli kwa uovu. Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana
yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo
yake yasioonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi
zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; kwa
sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali
walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena
kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na
uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya
wanyama, na ya vitambavyo.
Kwa
ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata
wakavunjiana heshima ya miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa
uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele.
Amina.
Hivyo
Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya
asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi
ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata
nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
Na kama
walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao
zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na
tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia
mbaya, wenye kuseng’enya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri,
wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiotii wazazi wao,
wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;
ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo
wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao
wayatendayo.” Kuna
watu wanaipinga kweli ya Mungu, kwa kufanya maovu, watu wengi shetani
amewapofusha na kufanya dhambi kwao ni kawaida, unapofanya dhambi ina maana
wewe una upinga ukweli wa Mungu, unakataa wokovu wa Yesu, unasema hakuna Mungu,
unasema hata bila Mungu mi ninaweza, na watu hawa wanafahamu ya kuwa kuna Mungu
na Mungu atawahukumu kwa sababu ya maovu yao, kwa sababu wamemuona Mungu lakini
bado wanaendelea kwenye maisha ya dhambi; kwa hiyo hawa watu wamepotea na macho
ya mioyo yao yamepofushwa, kwa hiyo Mungu amewaacha watu wa namna hii waendelee
kwenye dhambi zao, japo wanaujua ukweli; na akawaacha wafanye mambo ya aibu
kabisa, Kwa hiyo Mungu amewalipa kwa haya maovu wanayoendelea nayo. Kwa hiyo
wote wanaotenda dhambi Mungu amewaacha japo wanaweza kudai kuwa wao wanasali
dini ile au ile lakini hawana Mungu kwa sababu ya dhambi. Siku zote unapokataa
kumtii Mungu katika kitu chochote Mungu anakuacha, hawezi kuwa na wewe tena,
kitakachotokea hapo ni kwamba utakuwa unawapendezesha tu wanadamu na siyo Mungu
tena.
Ufunuo 21:27 inasema “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote
kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale waliondikwa
katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.” Kwa hiyo Mbinguni
hakitaingia chochote kilicho kinyonge wala yeyote afanyaye dhambi, hapa
inatuonyesha kwamba kama wewe daima umekuwa ukisumbuliwa na dhambi basi ujue
wewe ni mnyonge na hutaingia mbinguni; Mbinguni wanaingia watu wenye nguvu,
watu walio moto kwa ajili ya Bwana. Ni lazima uamue wewe wenyewe kuachana na
dhambi zako, na Mungu atakupa hayo maisha ya nguvu, maisha yenye bidii kwa
ajili yake, Je! utaamua kueguka leo Ili upate hayo maisha ya nguvu?.
Ufunuo 22:14-15 inasema “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri ya
kuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. Huko nje wako
mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao wabuduo sanamu, na kila
mtu apendaye uongo na kufanya.” Wale tu walio safi ndio wanaruhusa
ya kuingia katika ufalme wa Mungu; Wasio safi wote wako nje. Kama wewe bado
unafanya dhambi basi jua ya kuwa wewe tiyari uko nje.
Kwa hiyo hamna yeyote anayetenda
dhambi sasa, atakayeingia kwenye ufalme wa Mungu baada ya kufa katoka hapa
duniani.
WOTE WASIOKOKA WAMEKUFA KIROHO
Waefeso 2:1-3 inasema “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na
dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na
kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana
wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za
miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa
tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.” Hapa Mtu wa Mungu
anajaribu kutuonyesha hasa nini chanzo cha dhambi na kwa nini aliishi katika
dhambi kabla hajaokoka, na anazidi kutuonyesha kwamba sababu ya kwa nini
walikuwa kwenye dhambi ni kwa kuwa walikufa kwa sababu walimkosea Mungu, kwa
hiyo watu wote ambao hawajaokoka wamekufa kiroho japo wanaishi, haijalishi
wanatenda matendo matakatifu sana kama hawajamwamini Yesu basi wamekufa hao kwa
sababu ya dhambi zao.
Wakolosai 2:13 inasema “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya
makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye,
akiisha kutusamehe makosa yote;” Bado hapa anazidi kutuonyesha kuwa
watu wote ambao hawajaamini injili ya Yesu Kristo wamekufa katika dhambi zao,
dhambi inaleta kifo kwa mtu aliyeokoka, kama wewe umeokoka na ukaendelea na
maisha ya dhambi au ukaruhusu dhambi ikutawale basi unakufa kiroho, dhambi ni
risasi ya kiroho, inakuja kuua uhusiano wako na Mungu. Kwa hiyo hata kama
umeokoka ukiendelea na dhambi unarudi na kufanana na watu ambao hawajaokoka.
Kama mtoto wa Mungu umewekwa huru kutoka kwenye dhambi. Hupaswi kutenda dhambi
tena.
Yohana 5:24 inasema “Amin, amini, nawaambia, Yeye alisikiaye neno
langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii
hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” Mtu
anapookoka na kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wake katika maisha yake basi
anatoka kutoka mautini na anaingia uzimani, yaani kwenye ulimwengu wa roho,
roho yake inapewa uzima na Mungu mwenyewe, Mtu aliyeko ndani ambaye ni roho
asiyeonekana anafanywa kuwa hai, kama roho yako haijafanywa kuwa hai, huwezi
kuwa na uhusiano na Mungu tena, na hata kama ukiomba kwa Mungu hasikii hayo
maombi, kwa sababu wewe umekufa rohoni japo mwilini unaishi.
SHETANI NDIO BABA WA WATENDA
DHAMBI WOTE
1 Yoh 3:7-10 inasema “Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye;
atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa
Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa
Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na
Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi
kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa
Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani
na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.” Mtu yeyote anayetenda
dhambi, mtu huyo moja kwa moja Shetani ni Baba yake, Mtoto wa Mungu hatendi
dhambi, ana hofu ya Mungu, watu wengi wanatenda dhambi kwa sababu hawana hofu
ya Mungu, watu hawa wanahofu na mwanadamu. Na ndio maana hawezi kuwa huru toka
dhambini, hawaoni kama Mungu anawaona, wao wanachojali tu ni kwamba hawaonekani
na wanadamu na kusahau kuwa Mungu anawaona kila wanachofanya sirini. Watu wote
hawa wanafanya tu matendo ya baba yao Shetani.
Yohana 8:44 inasema “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na
tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda, Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo;
wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo
uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa
huo.” Kwa hiyo alama ya kutenda dhambi kwenye maisha yako; hii
inakuonyesha kuwa wewe ni mwana wa Ibilisi, kwa sababu unayo asili yake ndani
yako. Aina yeyote ya kusema uwongo ndani yako, hii moja kwa moja inakuonyesha
kuwa wewe ni mwana wa ibilisi au Shetani.
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment