
Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera anatarajiwa kufanya
ziara ya kitaifa ya siku tatu hapa nchini kuanzia tarehe 7 hadi 9 Oktoba 2020 kwa mwaliko wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mhe. Rais Chakwera atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini
Dar es Salaam tarehe 7 Oktoba 2020 na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli.
Hii ni ziara rasmi ya Kitaifa ya kwanza kwa Mhe. Rais Dkt. Chakwera tangu aingie madarakani
mwezi Juni, 2020 yenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili na
kuendelea kudumisha ujirani mwema.
Rais Chakwera atatembelea Bandari ya Dar es Salaam ili kujionea shughuli mbalimbali za
bandari hiyo na uboreshaji wa miundombinu ya bandari ambayo itaharakisha utoaji wa mizigo
bandarini na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora bandarini hapo lakini pia atatembelea
kituo cha kuhifadhia mizigo cha Malawi ambacho kimekuwa alama muhimu ya ushirikiano kati
ya Tanzania na Malawi.
Mhe. Rais. Dkt. Chakwera akiwa na mwenyeji wake, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, wataweka jiwe la msingi katika Kituo cha Mabasi ya kwenda mkoani cha Mbezi
Mwisho.
Uhusiano kati ya Tanzania na Malawi ni mzuri na unaendelea kuimarika siku hadi siku.
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment