} });
 

Rais Trump akinyoosha mkono na kuonesha ishara ya kuwa sawa kwa wanahabari wakati anaelekea kuingia kwenye helikopta iliyompeleka hospitali
 

Rais Donald Trump amepelekwa hospitali akiwa na homa baada ya kuthibitishwa kuwa na virusi vya corona.

Ikulu ya Marekani imesema rais alikuwa mchovu lakini hali yake iko sawa na amepelekwa hospitali ya jeshi la taifa ya Walter Reed kama hatua ya kuchukua tahadhari.

Bwana Trump alipata matibabu ya sindano akiwa Ikulu baada ya mke wake Melania Trump kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa Covid-19.

Donald Trump amepelekwa hospitali chini ya saa 24 baada ya kuthibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa hizo zinawadia ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi wa urais ambapo atakabiliana na mpinzani wake Joe Biden.

Donald Trump akiwasili katika hospitali ya jeshi la taifa ya Walter Reed

Akiwa amevaa barakoa na suti, Bwana Trump alitembea hatua kidogo tu katika Ikulu ya Marekani hadi kwenye helikopta yake, akipelekwa hospitali.

Alinyoosha mkono na kuonesha ishara ya kuwa sawa kwa wanahabari lakini hakusema lolote kabla ya kuingia ndani ya ndege.

Katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa Twitter, Bwana Trump alisema: "Nataka kumshukuru kila mmoja kwa kuwa nami. Ninaenda hospitali ya Walter Reed. Nafikiri naendelea vizuri.

"Lakini tutahakikisha kwamba mambo yanakwenda sawa. Mke wangu pia anaendelea vizuri. Kwahiyo asanteni sana, Nawashukuru, Siwezi kusahau - asanteni."

Watoto wa rais, Ivanka na Eric, walituma tena ujumbe wa baba yao, huku wakimsifu kuwa "shujaa". Mtoto wa Trump aliongeza: "Nakupenda sana baba."

Akiwasili hospitali ya Walter Reed, rais hakupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi, lakini alikwenda moja kwa moja katika sehemu iliyotengwa ya rais, kulingana na kituo mshirika wa BBC Marekani, CBS News.

Bwana Trump alianza kuwa kwenye karantini Jumatano

Mwandishi wa habari wa rais Kayleigh McEnany alisema kwenye taarifa: "Rais Trump yuko katika hali nzuri, ana dalili za wastani, na amekuwa akifanyakazi kwa siku nzima.

"Akiwa hayuko katika hatari, na kulingana na daktari wake na wataalamu wa tiba, rais atakuwa akifanya kazi katika hospitali ya Walter Reed kwa siku chache zijazo.

"Rais Trump anatoa shukrani zake kwa ujumbe anaopokea wa kumtakia uponaji wa haraka na mke wake."

Dalili alizonazo Bwana Trump ni pamoja na kiwango cha chini cha joto, kulingana na CBS.

Walter Reed, ni hospitali iliyopo viugani mwa Washington DC. Moja ya hospitali maarufu za kijeshi ambapo marais hutibiwa na pia hufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu wa kila mwaka.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu ya Marekani Alyssa Farah amesema rais bado hajahamisha madaraka yake hadi kwa makamu wa rais Mike Pence.

"Rais ndio msimamizi," alisema.

Hata hivyo alijiondoa kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya video uliohusisha waandamizi muhimu Ijumaa, na kumuacha Bwana Pence kuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top