} });
 


Dunia imepata pigo, mbuyu mkubwa umeanguka katikati ya msitu na kusababisha miti mingine yote itingishike! Ulimwengu wa soka unazizima, wapenzi wa soka na hata wale wasiofuatilia mambo ya mpira wa miguu, wote wanahuzunika.

 

Hii ni kwa sababu Diego Armando Maradona, mcheza soka bora kuliko wote kuwahi kutokea, amefariki dunia jioni ya Novemba 25, 2020 akiwa na umri wa miaka 60.

 

Kifo cha Maradona kimetokea katika wakati ambao hakuna aliyetarajia! Mshumaa umezimika ghafla katikati ya usiku wa giza nene. Rais wa Argentina, Alberto Fernández, ilipo asili ya Maradona, ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, bendera zote zikipepea nusu mlingoti. Nenda mfalme, nenda Maradona!

 

“Ipo siku mimi na wewe tutacheza soka juu mawinguni,” hayo ni maneno ya mkongwe mwingine wa soka, Pele aliyoyatoa mara tu baada ya habari za kifo cha Maradona kutangazwa na Shirikisho la Soka la Argentina.

 

Chanzo cha kifo cha Diego Maradona, kinaelezwa kwamba ni shambulio la moyo lililokuja wiki kadhaa baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kichwani.

 

Safari ya mwisho ya Maradona ilianza kama masihara hivi! Novemba 2, 2020, mchawi huyu wa soka alilazwa katika Hospitali ya La Plata. Hakuwa na hali mbaya kiafya, ilielezwa kwamba alikwenda kutibiwa matatizo ya kisaikolojia yaliyokuwa yakimsumbua, yakichangiwa sana na matumizi ya madawa ya kulevya ya muda mrefu na unywaji wa pombe wa kupitiliza.

 

Lakini baada ya madaktari kumfanyia vipimo, waligundua tatizo jingine kubwa zaidi. Maradona alikutwa na uvimbe ndani ya kichwa chake, ugonjwa ambao kitaalamu huitwa subdural hematoma.

 

Siku moja baadaye, alifanyiwa upasuaji wa ubongo kuondoa uvimbe huo na hatimaye Novemba 12 aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya kuelezwa kwamba upasuaji wake umefanyika kwa mafanikio makubwa, akawa anaendelea kufuatiliwa maendeleo yake na madaktari bingwa, akitokea nyumbani kwake.

 

Novemba 25 majira ya jioni, hali yake ilibadilika ghafla, akakumbwa na shambulio la moyo akiwa nyumbani kwake, Tigre katika jiji la Buenos Aires nchini Argentina. Wakati jitihada za kutaka kuokoa maisha yake zikifanywa, malaika mtoa roho alimtembelea, akamruhusu kuvuta pumzi yake ya mwisho kabla ya kutenganisha mwili na roho yake.

 

Huo ukawa ndiyo mwisho wa maisha ya mkongwe huyo ambaye hakuna asiyelijua jina lake chini ya jua! Nenda Maradona!

 

Miaka 60 aliyojaaliwa Maradona kuishi hapa duniani, imekuwa na mchanganyiko wa mambo mengi sana, milima na mabonde, nyakati za furaha na nyakati za huzuni, nyakati za kupanda na nyakati za kushuka! Itoshe kusema Maradona ameondoka na kuacha historia kubwa ambayo kamwe haiwezi kufutika!

 

Mpaka anafikwa na mauti, Maradona alikuwa ameweka historia nyingi ambazo zitaendelea kuishi hata baada ya yeye kuondoka hapa duniani. Kubwa kuliko yote, mwaka 2000, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), lilimtangaza Maradona kuwa mchezaji bora wa karne ya ishirini huku pia akipewa heshima ya mwanasoka bora zaidi duniani kuwahi kutokea.

 

Pengine umeshalisikia sana jina la Maradona lakini haujapata wasaa mzuri wa kuifahamu historia ya maisha yake. Pengine unalisikia sana neno ‘goli la mkono’ ambalo kwa hapa nchini limekuwa maarufu sana lakini hujui ni wapi neno hili lilipotokea na mwanzilishi wake.

Twende pamoja tukiichambua historia ya mfalme huyu wa soka, hatua kwa hatua.

 

HISTORIA YA MARADONA

Alipozaliwa Oktoba 30, 1960 katika Hospitali ya Polyclinic Evita iliyopo Lanus, Bueno Aires nchini Argentina, wazazi wake walimpa jina la Diego Armando Maradona. Alizaliwa katika familia ya kimaskini ya baba Diego Chitoro Maradona na mama Dalma Salvadora Franco iliyokuwa na jumla ya watoto saba, wanne wakubwa wakiwa ni wa kike kisha ndiyo akazaliwa yeye na kufuatiwa na wadogo zake wawili wa kiume.

 

Diego na ndugu zake walikulia katika kitongoji cha watu maskini cha Villa Fiorito, Kusini mwa Jiji la Buenos Aires, wakiishi maisha duni sana.


SAFARI YA SOKA

Maradona alizaliwa kwa kazi moja tu, kucheza soka na kipaji kikubwa kilichokuwa ndani yake kilianza kuonekana akiwa na umri wa miaka mitatu tu. Na hiyo ilikuwa ni baada ya kupewa zawadi ya mpira akiwa na umri huo ambapo sasa alielekeza nguvu zake zote kwenye mpira.

 

Alipofikisha umri wa miaka nane tu, kipaji cha Maradona kiligunduliwa na maskauti wa soka akiwa anacheza kwenye uwanja wa timu iliyokuwa jirani na makazi yao ya Estrella Roja na huo ukawa mwanzo wa safari yake ya mafanikio.

 

Uwezo wake mkubwa ulifanya achukuliwe na timu ya watoto ya klabu kubwa wakati huo ya Los Cebollitas ambako mbali na mambo mengine, alikuwa pia akifanya kazi ya kuokota mipira kwenye mechi za wakubwa (ball boy) za timu za daraja la kwanza nchini humo.

 

Hii ilikuwa ni nafasi nyingine kwa Maradona kuonesha uwezo wake kwani kila muda wa mapumziko ulipokuwa ukifika, yeye na watoto wenzake walikuwa wakiingia uwanjani na kuonesha umahiri wao wa kucheza na mpira, akaanza kuwa kivutio cha mashabiki wengi wa soka nchini humo kutokana na jinsi alivyokuwa ‘fundi’ wa kucheza na mpira, akiwa bado mdogo kabisa, akabatizwa jina la The Golden Kid.

 

Alipofikisha umri wa miaka 15, alichukuliwa rasmi na Klabu ya Buenos Aires’s Argentinos Juniors iliyokuwa ikishiriki ligi kuu ya nchini humo, akichezea klabu ya watoto ya timu hiyo.

 

Oktoba 20, 1976 ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza kuichezea timu ya wakubwa ya Argentinos Juniors, ambapo aliingia uwanjani akiwa amevalia jezi namba 16 na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kushiriki ligi kuu ya nchi hiyo, Argentine Primera Division, akiwa amebakiza siku 10 tu kabla ya kutimiza miaka 16.

 

Dakika chache baada ya kuingia uwanjani, alifanya tukio ambalo litaendelea kubaki kwenye kumbukumbu za wapenzi wa soka ulimwenguni kote na hiyo ilikuwa ni baada ya kumpiga chenga kisha kumlamba tobo mchezaji maarufu wa wakati huo, Juan Domingo Cabrera, tukio lililowashangaza wengi kutokana na umri wake.

 

Wiki mbili baada ya kutimiza umri wa miaka 16, Maradona alifunga goli lake la kwanza kwenye ligi kuu ya nchi hiyo wakati timu yake ya Argentinos Junior ilipovaana na San Lorenzo, hiyo ilikuwa ni Novemba 14, 1976, akaweka rekodi nyingine ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga goli kwenye ligi hiyo, nyota yake ikaanza kung’ara.

 

Maradona aliichezea Argentinos Juniors kwa muda wa miaka mitano, kuanzia 1976 hadi 1981, akifunga jumla ya magoli 115 katika mechi 167 alizocheza.

 

Kiwango chake kikafanya timu kubwa kuanza kumuwinda kwa udi na uvumba, Klabu ya River Plate ikataka kumsajili na kumuahidi kwamba atakuwa ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wote kwenye timu hiyo, akakubali kwa shingo upande huku akiueleza uongozi wa timu hiyo kwamba ndoto zake zilikuwa ni kuichezea Klabu ya Boca Juniors.


ASAJILIWA BOCA JUNIORS

Hatimaye ndoto zake zilikuja kutimia Februari 20, 1981 aliposajiliwa kutoka River Plate kwenda Boca Juniors kwa dau la dola milioni 4 za Kimarekani. Siku mbili baadaye, aliingia uwanjani kwa mara ya kwanza akiwa amevalia jezi za timu ya ndoto yake, Boca Juniors iliyokuwa inacheza na Talleres de Córdoba, akafanikiwa kufunga mabao mawili na kuifanya timu yake ishinde 4-1.

 

Aprili 10, mwaka huohuo, Maradona aliitumikia Boca Juniors dhidi ya timu yake ya zamani ya River Plate katika Uwanja wa Bombonera Stadium, akafanikiwa kufunga bao moja.

 

Maradona aliendelea kung’ara na Boca Juniors, akifanya maajabu kila alipokuwa akiingia uwanjani na hatimaye akaiwezesha timu hiyo kutwaa kombe la ligi kuu nchini humo. Hilo likawa kombe la kwanza na la kipekee kwa Maradona kunyakua akiwa katika ligi ya nyumbani.

 

Licha ya mafanikio makubwa Boca Juniors iliyoyapata kutokana na uwepo wa Maradona, baadaye figisu za hapa na pale zilianza kati yake na kocha wa timu hiyo, Silvio Marzolini chanzo kikitajwa kuwa ni mambo yao binafsi.

 

USAJILI WA KISHINDO BARCELONA

Waswahili wanasema mlango mmoja ukifungwa, mingine inafunguka kwa wakati huohuo. Figisu alizokuwa akifanyiwa na kocha wake wa Boca Juniors, zilimfungulia mlango mwingine wa mafanikio makubwa na hiyo ilikuwa ni baada ya kusajiliwa na klabu kubwa duniani ya Barcelona.

 

Alisajiliwa kwenda Barcelona mwaka 1982 mara tu baada ya kumalizika kwa kombe la dunia lililofanyika mwaka huo, akasafiri kutoka Argentina hadi Hispania kwenda kuyaanza maisha yake huku akivunja rekodi ya uhamisho ghali zaidi kuwahi kutokea katika ulimwengu wa soka.

 

Maradona alisahiliwa kwa dau nono la pauni milioni tano, sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 15. Hebu vuta picha, bilioni 15 kwa mwaka 1982 ilikuwa na thamani kubwa kiasi gani? Ama kwa hakika Mungu akitaka kukupa, huwa hakuandikii barua.

 

Ni hapo ndipo dunia nzima ilipoanza kumtambua Diego Armando Maradona na mwaka mmoja baadaye, 1983 akiwa chini ya kocha wa Barcelona,  César Luis Menotti, Maradona aliiwezesha Barcelona kunyakua ubingwa wa Copa del Rey kwa kuinyuka Real Madrid na mwaka huohuo wakanyakua kombe jingine la Spanish Super Cup baada ya kuifunga Athletico Bilbao.

 

Umewahi kuona wachezaji wa timu fulani wakimshangilia mchezaji kutoka timu pinzani baada ya kuwafunga? Yaani mchezaji wa Simba awafunge Yanga kisha mashabiki wa yanga wamshangilie? Kwa wafuatiliaji wa soka watakuwa wanaelewa jinsi timu za Barcelona na Real Madrid jinsi zilivyo na uhasama mkubwa miaka nenda rudi.

 

Basi kwa taarifa yako, tukio la kushangaza lilitokea June 26, 1983 baada ya  Maradona akiwa barcelona, kuifunga timu pinzani ya Real Madrid kisha mashabiki wa Real Madrid wakawa wanamshangilia Maradona!

 

Tukio hili liliingia kwenye historia ya soka duniani kote na kilichowafanya mashabiki wa Real Madrid wamshangilie muuaji wao, ni umahiri wa hali ya juu aliouonesha mchawi huyu wa soka ambapo aliwalamba chenga mabeki wa real Madrid, akabaki na kipa, naye akampiga chenga na kubaki peke yake langoni.

 

Badala ya kufunga, Maradona akaanza kwanza kuleta mbwembwe za kucheza na mpira akiwa yeye na goli tu, kisha ndiyo akafunga, unaambiwa uwanja mzima ukalipuka kwa shangwe, si Barcelona, si Madrid, wote wanashangilia bao hilo.


MAMBO YAANZA KUMHARIBIKIA MARADONA

Waswahili wanasema ukiona ngoma inavuma sana, basi ujue inakaribia kupasuka! Mafanikio ya ajabu aliyoyapata Maradona akiwa na Barcelona, yalikuwa mwanzo wa matatizo mengine makubwa katika maisha ya mwanasoka huyo bora wa wakati wote.

 

Tukio la kwanza lililoanza kubadili taswira ya Maradona, ilikuwa ni pale Barcelona ilipocheza na Atletic Bilbao na kupoteza kwa bao 1-0 Septemba 24, 1983 katika Fainali za Copa De Rey katika uwanja wa Santiago Bernabeu jijini Madrid.

 

Katika mchezo huo uliokuwa wa kukamiana kuliko kawaida, ukitawaliwa na rafu nyingi zilizokuwa zinachezwa na wachezaji wa Bilbao, Maradona alifanya tukio ambalo liliushangaza ulimwengu, safari hii siyo kwa mazuri tena, bali kwa mabaya.

 

Ilikuwa hivi, mchezaji wa Atletico Bilbao, Andoni Goikoetxea ambaye miezi michache awali alimchezea rafu mbaya Maradona iliyofanya akae nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu, alirudia kosa lilelile. Akamfyeka Maradona akiwa anaelekea kufunga na kusababisha aanguke kama mzigo.

 

Maradona akaona usinitanie wewe! Yaani juzijuzi tu umetoka kunivunja, leo tena unaleta mambo yaleyale? Haiwezekani. Akainuka kwa jazba na kumfuata mchezaji huyo, wakatoleana maneno machafu, inadaiwa mchezaji huyo akazidi kumkasirisha Maradona baada ya kumtolea maneno ya kibaguzi, mwisho wakashikana na kuanza kuzichapa.

 

Tukio hilo lilisababisha wachezaji wengine wa Bilbao waingilia kati kumuokoa mwenzao, wachezaji wa barcelona nao wakaona haiwezekani mwenzetu ashambuliwe halafu tukae kimya, nao wakaingilia kati, basi ngumi zikaanza kupigwa uwanja mzima, yaani ni piga nikupige.

 

Picha za video zikamuonesha Maradona akiwarushia makonde na mateke wachezaji wengine kadhaa wa Atletico na kuwajeruhi vibaya, uwanja wa soka ukageuka kuwa uwanja wa masumbwi na mieleka. Mashabiki nao wakaanza kuvurumisha vitu vigumu huku wengine wakipigana wao kwa wao.

 

Jumla ya watu sitini walijeruhiwa katika tukio hilo, ikabidi wanausalama waingilie kati kutuliza vurugu kubwa zilizokuwa zinaendelea, Maradona akiwa katikati ya uwanja wa vita, akitembeza vitasa kama hana akili nzuri.

 

Kibaya zaidi ni kwamba tukio hilo lilitokea wakati Mfalme wa Hispania, Juan Carlos na mashabiki laki moja waliokuwa uwanjani, achana na mamilioni wengine waliokuwa wakitazama kupitia runinga.

 

Tukio hilo lilitia doa kubwa kwenye umaarufu wa Maradona, uongozi wa timu hiyo ukaamua kwa kauli moja kumuuza Maradona kwani inaelezwa kuwa nyuma ya pazia, mchezaji huyo alikuwa akigombana na viongozi wake mara kwa mara, kwa kifupi alishageuka na kuwa mtukutu. Licha ya utukutu wake, lakini bado uwanjani alikuwa moto wa kuotea mbali, alifunga jumla ya mabao 38 katika mechi 58 alizocheza.

 

Baada ya majadiliano marefu, hatimaye Maradona aliuzwa kwa klabu ya Napoli ya Italia kwa dau jingine nono lililovunja rekodi, la pauni milioni 6.9, huo ukawa mwisho wa ufalme wa Maradona nchini Hispania na sasa akahamia Napoli na kutambulishwa rasmi Julai 5, 1984.

 

Akiwa Napoli, Maradona aliendelea ufalme wake wa soka, akaiwezesha timu hiyo kumaliza ufalme wa klabu za A.C. Milan, Juventus, Inter Milan na Roma ambazo ndizo zilizokuwa zikitawala kwa muda mrefu.


Inaelezwa kwamba akiwa Napoli, ndipo Maradona alipofikia kiwango cha juu kabisa cha ubora katika historia yake ya maisha ya soka, akaiongoza Napoli kushinda kwa mara ya kwanza Kombe la Seria A katika msimu wa 1986–87.

 

Aliiwezesha pia timu hiyo kushinda kombe la Seria A kwa mara ya pili katika msimu wa 1989–90, wakashinda Kombe la Uefa kwa mara ya kwanza mwaka 1989 sambamba na makombe mengine kibao ikiwemo Coppa Italia na Italian Supercup na kuweka rekodi nyingine kibao ambazo mpaka leo bado hazijavunjwa.


SKENDO NZITO ZA MADAWA YA KULEVYA

Katika kipindi hiki akiwa Napoli, ambapo kama nilivyoeleza awali, Maradona ndiyo alifikia kwenye kilele cha mafanikio akiwa mwanasoka bora zaidi kuwahi kutokea, upande wa pili wa maisha yake binafsi, moto ulikuwa unawaka.

 

Inaelezwa kwamba Maradona alikuwa ametopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya aina ya Cocaine na wachambuzi wa mambo, wanaeleza kwamba alianza matumizi ya madawa haya akiwa Barcelonanchini Hispania.

 

Inazidi kuelezwa zaidi kwamba hata fujo zilizotokea katika mechi ya barcelona na Atletico Bilbao, chanzo kikiwa ni Maradona, zilisababishwa na tabia yake ya utumiaji wa madawa hayo ya kulevya ambayo yalimbadilisha na kuwa mtu anayependa ugomvi kupindukia.

 

Kama inavyofahamika kwamba Italia ndipo wanakopatikana wafanyabiashara wakubwa wa madawa ya kulevya, baada ya kujiunga na Napoli, Maradona aliendelea na matumizi makubwa ya madawa ya kulevya na pombe na hiyo ilisababisha awe anasuguana mara kwa mara na uongozi wa klabu hiyo kwa sababu alikuwa akilewa kiasi cha kushindwa kuhudhuria kwenye mazoezi ya klabu.

 

Klabu yake ya Napoli ikaanza kumuadhibu kwa lengo la kumrekebisha tabia lakini wapi, tayari walishachelewa, gari lilishawaka na hakukuwa na namna yoyote ya kuweza kumdhibiti tena.

 

Shirikisho la Soka la Italia baada ya kugundua kwamba alikuwa akitumia madawa ya kulevya sambamba na ya kusisimua misuli, kinyume na sheria, lilimtia hatiani, akapimwa na kugundulika kuwa na kiwango kikubwa cha madawa kwenye mwili wake, jambo lililosababisha afungiwe kucheza soka kwa muda wa miezi 15.

 

Wakati sakata la madawa likiendelea, kuliibuka skendo nyingine kwamba Maradona aliyefunga ndoa Novemba 7, 1984 na mkewe Claudia Villafane alikuwa akiisaliti ndoa yao kiasi cha kuzaa nje ya ndoa. Msongo wa mawazo ukazidi kummaliza, akawa anazidi kuongeza dozi ya madawa na safari hii akawa anachanganya na pombe kali, akageuka na kuwa gumzo kwenye vyombo vingi vya habari, kila mtu akizungumzia mabaya yake.

 

Baada ya kumaliza kifungo chake cha miezi 15, hatimaye Maradona aliondoka Napoli na licha ya klabu kubwa za Real madri na Marseile kuonesha nia ya kumtaka, aliamua kusaini kuichezea Klabu ya Sevilla ambako nako alidumu kwa mwaka mmoja tu, akahamia Newell’s Old Boys na hatimaye akarejea Boca Juniors mwaka 1995, kiwango chake cha soka kikiwa kimeporomoka huku akiwa ameongezeka uzito kwa kiasi cha kutisha.

 

Kwa upande wa maisha yake binafsi, Maradona alitengana na mkewe mwaka 2004, wakiwa wa watoto wawili wa kike, Dalma Nerea (aliyezaliwa April 2, 1987) na Gianinna Dinorah (aliyezaliwa Mei 16, 1989). Baadaye, alikuja kukiri kwamba ni kweli alizaa nje ya ndoa mtoto aitwaye Diego Sinagra mwaka 1986.


MAFANIKIO TIMU YA TAIFA

Mbali na mafanikio makubwa aliyoyapata katika ngazi ya vilabu, Maradona pia hakuwa nyuma kwenye timu yake ya taifa. Kwa mara ya kwanza, Maradona aliichezea timu yake ya taifa februari 27, 1977 timu ya Argentina ilipocheza na Hungary, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 16 tu.

 

Katika michezo 91 aliyoichezea timu yake ya taifa, alifunga jumla ya mabao 34, miongoni mwa mabao hayo likiwemo goli la mkono lililompatia umaarufu mkubwa.

Wakati akiitumikia timu yake ya taifa, Maradona aliweka rekodi nyingine ya kutwaa tuzo mbili kubwa, FIFA U-20 World Cup mwaka 1979 na FIFA World Cup mwaka 1986, rekodi ambayo mpaka sasa aliyefanikiwa kuivunja ni Lionell Messi pekee.

 

Bao la mkono au ‘bao la mkono wa Mungu’ alilifunga wakati timu yake ilipokutana na Uingereza mwaka 1986 katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia, timu hiyo ikishinda kwa mabao mawili, yote yakiwa yamefungwa na Maradona. Goli la kwanza, Maradona aliruka kichwa lakini akaukosa mpira, akajiongeza na kuupiga kwa mkono kwa namna ambayo mwamuzi hakumuona, mpira ukajaa wavuni na refa akapuliza kipyenga kuonesha kuwa ni goli halali.

 

Mvutano mkubwa ulitokea lakini goli likawa limeshakubaliwa, dakika nne baadaye akaongeza goli lingine ambalo nalo liliingia kwenye historia kutokana na jinsi alivyolifunga kwa umahiri wa hali ya juu, akiwapita mabeki watano wa England kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.

 

Bao hili la pili lilipewa hadhi na FIFA ya kuwa bao bora zaidi kuwahi kutokea katika michuano yote ya kombe la dunia na mwaka 2002, bao hilo lilipigiwa kura na kushinda kuwa bao bora la karne ya 20 na FIFA.


MAISHA YA UKOCHA

Mbali na mafanikio makubwa aliyoyapatya kama mchezaji, Maradona pia amefanikiwa kujijengea heshima kubwa, akiwa kocha.


Alianza kazi ya ukocha mwaka 1995 baada ya kustaafu rasmi soka, lakini alianza kupata umaarufu akiwa kocha mwaka 2009 alipotangazwa kuinoa Timu ya Taifa ya Argentina na kuiongoza katika michuano ya kombe la dunia 2010.

 

Mwaka 2011 alijiunga na timu ya Al Wasl FC ya Dubai akiwa kama kocha, baadaye alizifundisha pia timu za Deportivo Riestra, Fujairah, Dorados, Gimnasia de La Plata na nyingine nyingi.


Huyo ndiyo Deigo Armando Maradona ambaye anatarajiwa kuzikwa na serikali.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top