} });
 

 

RAIS John Magufuli amesema kuwa hatosita kuwawajibisha watendaji wake ambao watakuwa wazembe ama watafanya kazi kinyume na taratibu na sheria za nchi, hivyo ameagiza watumishi na watendaji wote wa serikali atakaowateua katika awamu ijayo na waliopo wachape kazi kwa manufaa ya taifa na si kwa manufaa yao binafsi.

 

Amesema hayo leo Novemba 13, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma na kuonyesha dira ya miaka mitano ya serikali yake ambapo imejikita katika kuboresha uchumi na maisha ya wananchi wake ikiwemo kurahisisha mambo mbalimbali katika sekta ya uwekezaji na biashara sambamba na kuweka miundombinu madhubuti ya anga, majini na barabara ili kuvutia uwekezaji na kurahisisha biashara pamoja na huduma za kijamii.


Baadhi ya mambo muhimu aliyoyasema katika hotuba yake ni yafuatayo:

“Nakumbuka wakati nakuja bungeni mara ya mwisho, tulikuwa na marais wetu wastaafu, lakini leo hatunaye Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, pia kuna wabunge ambao wametutoka, niwaomba sote tusimame dakika moja tumuombee Mkapa na wabunge wenzetu waliotangulia mbele za haki.

“Naipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia vizuri kuanzia uandikishaji, upigaji kura, kuhesabu kura mpaka matokeo, hii imeonyesha tunao uwezo mkubwa wa kusimamia uchaguzi bila kutegemea misaada kutoka nje, hongereni sana NEC. Kiasi cha Tsh bilioni 331 zilitengwa kwa ajili ya uchaguzi lakini mpaka uchaguzi unakwisha NEC imetumia Tsh bilioni 262 tu, hii inaonyesha uadilifu wa viongozi na watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, niwaombe na taasisi nyingine muige mfano mzuri wa tume hii.

“Nawashukuru viongozi wa dini kwa kuliombea Taifa letu katika kipindi cha uchaguzi na tukamaliza tukiwa salama, niwaombe muendelee kuliombea Taifa letu amani iendelee kutawala. Nampongeza Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa Naibu Spika, hongera sana huu ni uthibitisho kwamba nchi yetu kupitia serikali inayoongozwa na CCM inawaamini sana wanawake na Bunge hili la 12 lina wabunge wengi wanawake. Nawaahidi kuwa Serikali ninayoiongoza itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Nimekuja kulizindua Bunge hili baada ya nchi yetu kufanikiwa kumaliza Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020 kwa uwazi, amani na utulivu mkubwa. Napenda nirudie kuipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kusimamia vizuri zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Natoa shukrani kwa Watanzania wenzangu wote kwa kushiriki vizuri na kuonesha utulivu mkubwa kwenye Uchaguzi uliopita. Hakuna shaka Uchaguzi huu kwa mara nyingine umethibitisha watanzania ni wapenda amani, tunajitambua, hatudanganyiki na tumekomaa kidemokrasia.

“Nitashirikiana na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kulinda Amani, hatutokuwa na utani hata kidogo na mtu atakayetaka kuvuruga amani na kuingilia uhuru wetu. Namuahidi Rais Dkt. Mwinyi nitampa ushirikiano wa kutosha katika kukamilIsha aliyoyaahidi.


“Utumbuaji majipu utaendelea, tutaboresha maslahi ya watumishi wote, watumishi wasiwe na wasiwasi wachape kazi, tumeingia kwenye uchumi wa kati na tutazidi kukuza uchumi kwa wastani wa angalau 8% kwa mwaka na kutengeneza ajira zipatazo milioni 8. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, sekta binafsi itapewa umuhimu wa pekee, tunataka mtu yeyote atakayewekeza asisumbuliwe, Watanzania ni matajiri lakini wanasita kuwekeza nchini, tunahitaji kuwa na mabilionea wengi wa Kitanzania wakiwemo wabunge.

“Tutaendelea kuinua uchumi wa Wananchi wetu kwa kuwapa mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu, kuna mifuko mbalimbali ya kuinua uchumi ukiwemo wa Vijana na Wanawake, Waziri Mkuu kazi yako ya kwanza ikawe hii ikiwezekana baadhi ya mifuko iuanganishwe.. Wawekezaji wasisumbuliwe, Watanzania ni Matajiri ila wanaogopa kuwekeza nchini kwa kuhofia maswali mengi, tunataka Mabilionea wengi wakiwemo Wabunge, Watanzania wahamasishwe kuwekeza pesa kwenye Mabenki yetu, wakati wa kufanya mambo bila uoga ni sasa.

 

“Tunakusudia kukuza kilimo biashara, mazao tunayolenga kuyapa kipaumbele ni pamoja na korosho, kahawa, pamba, chai, michikichi, miwa na nyingine, tunaagiza ngano nyingi na vyakula vingine kutoka nje, ni aibu kwa Tanzania, Waziri wa Kilimo nitakayemteua akaanze na hili.

“Tunataka wafugaji wetu wasiteswe na mifugo yao, mifugo ni utajiri, tutahamisha ufugaji wa kisasa, tutakamilisha ujenzi wa machinjio saba unaoendelea maeneo mbalimbali nchini ambapo zitakuwa na uwezo wa kuchinja Ng’ombe 6,700 na Mbuzi 11,000 kwa siku.

“Kwa sababu hiyo nimeamua suala la uwekezaji ikiwemo na pamoja na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), kukihamisha kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kwenda kwenye Ofisi ya Rais ili hao wanaokwamisha nikapambane nao mimi mwenyewe.

“Nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa mifugo mingi Afrika, tutainua Sekta ya Mifugo ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Machinjio saba nchini, tunakaribisha wawekezaji kuwekeza kwenye bidhaa za mifugo ikiwemo viwanda vya ngozi, nguo, mikanda na nyingine, tutanunua nane za uvuvi.

“Niipongeze Hifadhi yetu ya Serengeti kwa kuchaguliwa kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa mwaka 2020, miaka mitano ijayo tumejipanga kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia Milioni 5 mwaka 2025, na mapato kufikia Dola za Marekani Bilioni 6.

“Tutapunguza foleni Barabarani, tutapanua viwanja vya ndege 11, tutaboresha upatikanaji wa huduma za umeme, tutafikisha umeme kwenye vijiji vyote vilivyobaki, upande wa Afya tutahakikisha Watanzania wote wanakuwa na Bima ya Afya na kuongeza Hospitali
“Wakati wa Corona licha ya kumtanguliza Mungu ila dawa za asili zimetusaidia, katika miaka mitano ijayo maduka ya tiba mbadala na matibabu ya asili yataruhusiwa na tutaendeleza Taasisi ya Utafiti wa Tiba Asili, pia tutaboresha zaidi matibabu ya kibingwa. Tutahimiza ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati hususan kwa wanafunzi wa kike. Tunakusudia kujenga Shule moja kila mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya Sayansi kwa Wasichana.”

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top