} });
 


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Nyamhanga amesema ofisi hiyo imeanza maandalizi ya ujenzi wa shule 26 zenye hadhi ya kitaifa kila mkoa.

Nyamhanga aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kutoa tathmini ya matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu.

Waandishi walitaka kufahamu mkakati wa serikali kuhakikisha wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani hawapangwi kusoma mbali na wanapoishi kwa kuwa wengi wamekuwa wakilazimika kupanga nyumba zinazosababisha wakutane na changamoto mbalimbali na baadhi kushindwa kuhitimu.

Nyamhanga alisema serikali imekuwa na mikakati ya kujenga mabweni na kwamba kwa sasa Tamisemi imeanza maandalizi ya ujenzi wa shule za sekondari zenye hadhi ya kitaifa ili kutekeleza uamuzi wa serikali kuhimiza ufundishaji masomo ya sayansi na hisabati hasa kwa wanafunzi wa kike.

"Tunaamini kukamilika kwa kazi hii kutawaondolea adha wanafunzi hususani wanafunzi wa kike kutembea mbali mrefu kufuata shule," alisema.

Wakati akizindua Bunge la 12, Rais John Magufuli alieleza mikakati ya serikali kujenga shule ya sekondari katika kila mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wasichana.

"Lengo la serikali ni kuendelea kuboresha elimu inayotolewa ili iweze kutoa maarifa na ujuzi wa kutosha kwa wahitimu, tutahimiza ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati hususan kwa wanafunzi wa kike.”

“Tunakusudia kujenga shule moja ya sekondari kwenye kila mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wasichana," alisema Rais Magufuli.

Pia alisema serikali itaweka mkazo kwenye elimu ya ufundi na kuanzisha vituo mahiri vya mafunzo kwa taasisi za elimu ili kuzalisha vijana wenye uwezo unaohitajika kitaifa, kikanda na kimataifa.

Rais Magufuli alisema serikali pia itaendelea kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, itaongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuongeza idadi ya wanufaika, itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu ikiwamo madarasa, mabweni, maabara, maktaba, ofisi, nyumba za walimu, hosteli na kumbi za mihadhara.  

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top