} });
 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma wiki iliyopita kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aweze kushiriki na kutekeleza vyema majukumu yake katika baraza hilo.

 

Baadhi ya wasomaji wetu wametaka kujua kwa nini aingie kwenye baraza la mawaziri la Tanzania wakati yeye sio waziri aliyeteuliwa na Rais John Magufuli?

Leo tutajadili kuhusu hadhi na mamlaka ya rais wa Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Wakili maarufu ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadhi Saidi anasema:

“Tumekuwa tukieleweshwa na kufafanuliwa kuwa yule mtu ambaye Wazanzibar kupitia katiba yao ya Zanzibar humchagua kuwa rais wao, rais huyo huyo, kwa kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania (ambayo kimsingi sio iliyomuweka madarakani) hupewa hadhi ya uwaziri wa kawaida tu katika baraza la mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Hana wizara)”

 

Kwa Zanzibar anakuwa “rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi”, na kwenye uchaguzi wazanzibari walimchagua hivyo; kisha anaunda serikali yake kwa kuteua makamu wa rais wawili na anateua mawaziri na anakuwa mkuu wa serikali ya Zanzibar.

 

Katika serikali ya Tanzania rais wa Zanzibar anakuwa waziri wa kawaida tu na kwenye hilo baraza la mawaziri la Tanzania, rais wa Tanzania ndiye anaongoza vikao vya baraza la mawaziri, na ikitokezea hayupo vikao vinaongozwa na makamu wa rais; na ikitokea wote hawapo vikao vinaongozwa na waziri mkuu – kifungu 54 (2).

 

Rais wa Zanzibar hadhi yake ni sawa na hadhi ya waziri wa kawaida tu wa Tanzania.

Kifungu cha 54 (1) cha Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 kinasema:

“Kutakuwa na baraza la mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni makamu wa rais, waziri mkuu, rais wa Zanzibar na mawaziri wote.”

 

Sambamba na hayo, kifungu hicho cha 54 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinaeleza kwamba Baraza la Mawaziri litamsaidia Rais na kumshauri juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo kwa mujibu wa maagizo maalum au maagizo ya jumla yatakayotolewa na Rais.

 

Wakili Awadhi anasema wakati Zanzibar inaungana na Tanganyika mwaka 1964, mkataba wa muungano ulieleza wazi kuwa rais wa Zanzibar atakuwa makamu wa rais wa Tanzania na iliendelea hivyo hadi mwaka 1994 ambapo hadhi yake ilishushwa kutoka kuwa makamu wa rais hadi waziri wa kawaida ndani ya baraza la mawaziri.

 

Mwaka 1992 wakati Tanzania inarejesha mfumo wa vyama vingi iliibuka hofu kuwa endapo serikali za pande hizi mbili zingekamatwa na vyama tofauti hali hiyo ingeleta msuguano katika masilahi ya muungano.

 

Ikaundwa kamati ya Jaji Mark Bomani ambayo ilipendekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa mgombea mwenza ili kama mgombea akitokea upande mmoja wa muungano basi mgombea mwenza atokee upande wa pili wa muungano – na kuwa huyu mgombea mwenza ndio atakuwa makamu wa rais wa Tanzania badala ya rais wa Zanzibar kama ilivyokuwa zamani.

 

Lakini pia utata ukaibuka kuwa rais wa Zanzibar itakuwa ametolewa kabisa katika mfumo wa kiuongozi wa Tanzania, ikaamuliwa aingizwe, ila awe mjumbe tu kama waziri wa kawaida kwenye baraza la mawaziri Tanzania.

 

Bunge la Jamhuri ya Tanzania likarekebisha Katiba kukidhi mabadiliko hayo.

“Baadhi ya wazanzibar walilipinga hili. Mwaka 1995, wazanzibar 50 wakiongozwa na Mtumwa Said Haji walikwenda kufungua kesi Tanzania bara kupinga jambo hili. Kesi yao (kesi no 2 ya 1995) ilipigwa na chini.

 

Ulipofika wakati wa mawaziri kula kiapo cha utiifu na uaminifu kwa rais wa Tanzania, kukawa na ukakasi kwa rais wa Zanzibar (wakati huo alikuwa Dk. Salmin Amour) kwenda kula kiapo kwa rais mwenzake.

 

“Utaratibu ukabuniwa kuwa rais wa Zanzibar ale kiapo cha uaminifu mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba namkumbuka mzee mmoja ambaye alilalamikia hadhi ya rais wa Zanzibar kwa namna ya kipekee.

 

“Alisema huyu ni rais pekee ambaye naye siku ya uchaguzi hupanga foleni kuchagua rais mwingine na ni rais pekee ambaye huunda serikali yake yeye akiwa rais lakini hapo hapo akigeuka upande wa pili na yeye huwa waziri kama hawa mawaziri wake aliowateua.

 

“Alishangazwa na utatanishi huu, anyway, tunaendelea hivyo hadi leo, pia leo tumekumbushwa kuwa rais wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka makuu kwa Tanzania nzima na kuwa ni sahihi kwake kutoa maagizo kwa mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa vile yeye ni mkuu wa nchi (head of state) na yeye ni amiri jeshi mkuu (commander in chief),” anasema Wakili Awadhi.

 

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania mtu huchaguliwa kuwa rais pale anapopata kura nyingi kushinda wagombea wenzake, hakuna sharti kuwa apate kiwango fulani cha kura kutokea upande wa Zanzibar.

 

Tanzania bara kuna wapiga kura zaidi ya milioni 20 na Zanzibar kuna wapiga kura 500,000 na ushee tu. Mgombea anaweza kuwa rais wa Tanzania kwa kura za Tanzania bara tu, hata kama kura zote za Zanzibar zimemkataa.

 

Kuhusu hilo Wakili Awadhi anasema: “Kinadharia mgombea urais wa Tanzania anaweza kushinda bila kura za Zanzibar na anaweza hata asiende kufanya kampeni Zanzibar na akanadi hadharani kuwa hataki kura yoyote kutoka Zanzibar.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top