} });
 

 

Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping leo amempigia simu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania hususani katika masuala ya uchumi.

Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa muda wa saa 1, Rais Xi Jinping amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha 2 na ameeleza kuwa kuchaguliwa kwake kumetokana na kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi cha miaka 5 ya kwanza ambapo uchumi umeimarika zaidi na kwamba anaiona Tanzania kuwa nchi itakayoongoza kwa ukuaji wa uchumi Barani Afrika.

Xi Jinping amempongeza Rais Magufuli kwa namna Tanzania ilivyokabiliana na ugonjwa wa Korona (Covid-19) na ameeleza jinsi China inavyoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.

Amempongeza Rais Magufuli kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway) na ujenzi wa bwawa la kuzalisha megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji (Bwawa la Mwl. Nyerere) na ameeleza kuwa China itaangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amemshukuru Rais Xi Jinping kwa kumpigia simu, kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha 2 na kumpongeza kwa hatua za kimaendeleo zinazopigwa na Tanzania hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Rais Magufuli amemhakikishia Rais Xi Jinping kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na China uliodumu kwa takribani miaka 55 baada ya kuasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong, na kwamba Tanzania itaendelea kuiunga mkono China katika masuala mbalimbali ya kimataifa.

Rais Magufuli amesema Tanzania inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, utalii, ujenzi na biashara kwa manufaa pande zote mbili.

Aidha, Rais Magufuli ameiomba China kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji wa miradi mikubwa kwa kutoa mikopo nafuu na ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni wa kuzalisha megawati 358 za umeme katika mto Ruhudji, Megawati 222 za umeme katika mto Rumakali na ujenzi wa barabara Visiwani Zanzibar.

Halikadhalika, Rais Magufuli ameiomba China kufungua zaidi masoko ya bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania hususani mazao mbalimbali ya kilimo.

Rais Xi Jinping ameahidi kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli ikiwemo ujenzi wa miradi ya kuzalisha umeme ya Ruhudji na Rumakali, ujenzi wa reli, Bwawa la Nyerere na ununuzi wa mazao ya Tanzania.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top