} });
 


Kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya Motisun Group ambaye pia alikuwa miongoni mwa mabilionea wachache nchini Tanzania na mfanyabiashara maarufu, Subhash Patel, kimeibua mjadala mzito juu ya pigo wanaloliacha mabilionea nchini pindi wanapofariki dunia.

 

Subhash Patel alifariki dunia wiki iliyopita nyumbani kwake, Kisutu jijini Dar baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kisukari.


Ndiye mmiliki wa makampuni na bidhaa za Kiboko Plastics, Kiboko Protected Sheets, MM Estates, White Sands Hotel, MMRDL, Neeklanth Cables, Pearlsun Hotel & Resorts, Sayona Drinks Ltd, Sea Cliff Hotel, Best Bite, Mamba Cement, MMI Steel na nyingine nyingi.

 

Maelfu ya watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania walituma salamu za rambirambi wakieleza namna ambavyo kifo chake ni pigo kwa Taifa na uchumi wa mtu mmojammoja walioajiriwa na makapuni yake.


Kifo cha Subhash Patel kimeibua mjadala huo ambao unahusisha vifo vya mfululizo vya mabilionea nchini ambavyo vinatajwa kuisababishia nchi pigo zito la kiuchumi.

 

WAMO PIA AKINA MENGI

Wengine waliotajwa na wachambuzi mbalimbali kwenye orodha hiyo ya mabilionea wa Tanzania waliotangulia mbele za haki na kuwa pigo kubwa kiuchumi nchini ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Abraham Mengi aliyefariki dunia mapema mwezi Mei, 2019.

 

Mwingine Ali Mufuruki aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya Infotech Investment Group aliyefariki dunia, mwezi Desemba, 2019.


Yumo pia Salum Shamte aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani aliyefariki dunia mapema mwezi Machi, mwaka huu.

 

Mwingine ni Salim Hassan Abdullah Turky almaarufu Mr White na aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makapuni ya Turkys Group akimiliki Golden Tulip Hotel, Nitak Communications, Tasakhtaa Zanzibar General Hospital na makampuni mengine ya mafuta, saruji na vyakula. Turky aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Mpendae Visiwani Zanzibar, alifariki dunia mwezi Septemba, mwaka huu, wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2020.

 

Pia anakumbukwa Dk. Rajni Kabanabar ambaye ni daktari bingwa aliyekuwa mwanzilishi na Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency ya Upanga jijini Dar ambaye alifariki dunia mwezi Juni, 2019.


Kwenye orodha hiyo, pia anatajwa aliyekuwa mmiliki wa Mabasi ya Marangu Coach, James Dunia almaarufu Tajiri wa Marangu aliyefariki dunia mwezi Juni, mwaka huu.

 

MCHANGO WA SUBHASH PATEL

Mbali na kuwa Mwenyekiti Mtendaji na Mwanzilishi wa Makampuni Motisun, Subhash Patel, pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) inayosimamia na kuhamasisha sekta binafsi.

 

Chini ya Motisun Group, kuna kampuni zinazojihusisha na chuma, uchimbaji wa madini, saruji, plastiki, rangi, vyakula, ujenzi, mabati, nondo, nyaya za umeme na vinywaji ambapo pia anamiliki Hoteli za White Sands na Sea Cliff, Pearlsun Hotel & Resorts. Taarifa zinaeleza kuwa, anatoa ajira zinazokadiriwa kufikia 50,000.

 

Kampuni hizo zinasambaza huduma nchi za Tanzania, Zambia, Uganda na Msumbiji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TPSF, ilielezea masikitiko ya taasisi hiyo kumpoteza mfanyabiashara huyo tajiri na maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.

 

“Patel alikuwa ni injini ya ukuaji wa uchumi…” ilieleza taarifa hiyo.

Inafahamika kwamba mfanyabishara huyo alipenda kujitolea na kusaidia wananchi huku akihamasisha mtu mmojammoja kuchapa kazi kwa maendeleo yake binafsi.

 

“Ana mchango wake kwenye sekta ya viwanda, ametoa msaada kwa maskini na matajiri,” alisema Waziri Mkuu wakati akimuelezea mfanyabiashara huyo na kuongeza;

“Taifa limempoteza mmoja wa wazalendo wake.”

“Wakati nikiwa na majukumu serikalini nilishuhudia jinsi alivyosaidia miradi mingi vijijini, yenye nia ya kuwatoa Watanzania kwenye umaskini,” anasema Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani.

 

MCHANGO WA MZEE MENGI

Mbali na kumiliki makampuni mengi ndani na nje ya Tanzania kisha kuajiri watu wengi, mzee Mengi alisifika kwa kuwa ni mtu aliyekuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya ujasiriamali, mpole, asiye na majivuno, mkarimu na mwenye huruma, hususan juhudi zake za kuwasaidia watu wenye ulemavu na wasiojiweza.

 

Kabla ya kifo chake, Mzee Mengi alisaidia Taifa kama mtu mzalendo asiyetiliwa shaka huku akieleza mpango wake wa kuwa kwenye mchakato wa kuanzisha kiwanda cha magari na simu nchini.

 

MCHANGO WA MUFURUKI

Mufuruki alikuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya biashara nchini kwa kufungua fursa mbalimbali, muhisani na kocha wa masuala ya uongozi.


Mtendaji Mkuu wa jukwaa la sekta binafsi nchini, Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Godfrey Simbeye alikitaja kifo cha Mufuruki kuwa ni pigo na pengo kubwa katika dira ya sekta binafsi nchini Tanzania.

 

MCHANGO WA SHAMTE

Mbali na kuwa kiungo muhimu wa zao la mkongwe na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye anamtaja Shamte kwenye kundi la wafanyabiashara wazawa na wazalendo kama ilivyokuwa kwa Mzee Mengi na Mafuruki.


“Ukweli tumekuwa wanyonge sana ndani ya TPSF, msiba wake kwetu ni pigo kubwa,” anasema.

 

MCHANGO WA TURKY

Turky alikuwa mfanyabiashara maarufu Zanzibar na Mbunge wa Mpendae tangu 2010 akiwatumikia watu wake kwa moyo wa uzalendo na kutamani wawe na maendeleo. Hadi anafariki alikuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya Turky ambapo chini yake yalikuwa makampuni 12 yanayoendesha biashara zake Tanzania Bara, Zanzibar na Visiwa vya Comoro huku yakiajiri maelfu ya watu.

 

Baadhi ya makampuni hayo yanajumuisha Hoteli ya Golden Tulip na Hospitali ya Tasakhtaa Zanzibar inayotoa huduma kwa wagonjwa wengi.

 

MCHANGO WA KABANABAR

Mwaka 1979, Dk. Kanabar alianzisha mradi wa kupeleka wagonjwa wa moyo nchini India na kila mwaka zaidi ya watoto 100 kutoka Tanzania walikuwa wakipelekwa kutibiwa India bure.


Kupitia mradi huo uliofahamika kama Tanzania Heart Babies Project, wagonjwa wengi wakiwa na matatizo ya valvu kwenye moyo walikuwa wakipelekwa kwenye hospitali mbalimbali za India ikiwemo Narayana na Hayderabad.

 

Dk. Kanabar ambaye alikuwa mwendeshaji wa mradi huo kupitia Klabu ya Lions ya Dar es Salaam (Host), alikuwa mstari wa mbele kutafuta wafadhili wa kutoa pesa kwa ajili ya kupeleka watoto hao nje ya nchi.


Miongoni mwa wafadhili wakuu kwenye mradi huo ni Mzee Mengi ambaye kila mwaka alikuwa akitoa pesa za kupeleka wagonjwa zaidi ya 50 nchini India.

 

Dk. Kanabar alishiriki kuanzishwa kwa Hospitali ya Regency na kwa zaidi ya miongo mitatu alitwaa tuzo mbalimbali kutokana na mchango wake wa kuhudumia jamii hususan kwenye sekta ya afya.

 

MCHANGO WA TAJIRI WA MARANGU

Tajiri wa Marangu alikuwa ni mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Usafirishaji ya Abiria nchini Tanzania ya Marangu Coach.


Watu waliomfahamu tajiri huyo wanasema kuwa, bado pengo lake linaonekana na bado ni pigo kwani alikuwa mpambanaji asiyekuwa na mfano.

 

Baadhi ya wafanyakazi wa makampuni yake bado wanamkumbuka.

“Bado ni pigo kubwa sana kwa sababu nyuma yake kuna watu wengi ambao walitoka kimaisha kwa sababu yake. Itoshe tu kusema jamaa alikuwa jembe sana na alikuwa mfano wa kuigwa,” anasema mmoja wa wafanyakazi wa Marangu Coach, Innocent Moshi.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top