} });
 


WATU watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 14 likiwemo la kujipatia kiasi cha Sh 365 milioni kwa njia ya udanganyifu huku wakijifanya wafanyakazi wa Shirika la Ugawi wa Umeme (Tanesco).

 

Washtakiwa hao ni Regnald Massawe (38) mkazi wa Ununio, Garston Danda (38) mkazi wa Kilongawima Kunduchi, Claudius Kabugi (34) mkazi wa Mbezi, Inene Marwa (25) na Noel Kitundu, mkazi wa Africana.

 

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Maternus Marandu, amedai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la uhalifu, mashtaka sita ya kughushi, moja likiwa ni la kutoa nyaraka za uongo, na manne kujipatia fedha kwa njia ya uongo pia moja la utakatishaji wa fedha.

 

Marandu amedai katika shtaka la kwanza kati ya Desemba 2019 na Novemba,2020 jijini Dar es Salaam, waliongoza genge la kihalifu.

 

Shtaka la pili kati ya Desemba 17,2019 jijini Dar es Salaam mshtakiwa Massawe na Danda wakiwa na nia ya kufanya ulaghai waligushi nyaraka za benki kwa kudai wanatoa taarifa za mteja huku wakijua siyo kweli.

 

Katika shtaka la tatu tarehe hiyo na maeneo hayo mshtakiwa Massawe akiwa na nia ya kufanya ulaghai aligushi leseni ya biashara kwa ajili ya kuonyesha kwamba ilikiwa nyaraka ya kweli iliyotolewa na Tanesco.

 

Shtaka la nne kati ya Desemba 10,2019 eneo la Tawi la Msasani Benki ya NMB jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Massawe akiwa na nia ya ulaghai aligushi nyaraka ya akaunti ya mtu binafsi ya mfanyakazi wa Tanesco.

 

Miongoni mwa mashtaka mengine ni shtaka la kumi hadi la 13 ambayo inadaiwa kati Desemba 28, 2019 na Oktoba 02, 2020 wote kwa pamoja wakiwa eneo la Benki ya NMB tawi la Msasani, benki ya CRDB tawi la Msasani, walijipatia mkopo wa Sh 365 milioni kupitia akaunti binafsi ya mshtakiwa Massawe, Kabagi, Marwa na Kitundu ambapo  walijifanya ni wafanyakazi wa Tanesco.

 

Shtaka la mwisho ni kati ya Desemba 2019 na Novemba 2020, ambapo  washtakiwa wote kwa pamoja walijipatia Sh 365 milioni mali ya Tanesco huku wakijua fedha hizo ni mali ya mazalia ya uhalifu.

 

Akitoa ufafanuzi mbele ya washtakaiwa, Hakimu Mwandamizi, Rashid Chaungu, amesema kosa la kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji wa fedha ni ya uhujumu uchumi hivyo washtakiwa hao hawaruhusiwi kujibu chochote na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 21, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top