Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli ameagiza shule zote zilizokuwa zimefungwa kama hatua za kupambana na
mlipuko wa virusi vya corona, zifunguliwe Juni 29, 2020.
Akitoa
hotuba yake wakati wa kuvunja Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais Magufuli amesema kuwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na
Serikali na wananchi kwa ujumla katika kupambana na virusi hivyo, sasa hivi
athari za ugonjwa huo sio kubwa.
“Kutokana
na kuendelea vizuri kwa mapambano dhidi ya corona, napenda nichukue nafasi hii
kutangaza kuwa kuanzia tarehe 29 Juni, 2020 shule zote zifunguliwe zilizokuwa
zimebaki,” amesema Rais Magufuli.
Hata
hivyo, Rais Magufuli amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya
virusi vya corona.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amewapongeza wabunge walioendelea na vikao vya
Bunge na kwamba wachache waliokimbia wanapaswa kufahamu kuwa kukimbia tatizo
sio njia sahihi.
“Bunge
hili kuendelea na vikao vyake kwa kawaida kama lengo la kuwatumikia watanzania,
japo nafahamu wapo wachache waliokimbia, lakini sijui kama wamesharejea, lakini
niseme kukimbia haikuwa jambo sahihi kwa sababu matatizo hayakimbiwi, kukimbia
changamoto ni ishara ya udhaifu,” alisema Rais Magufuli.
Lakini
pia kukimbia ni ishara ya uogo, lakini pia ni ishara ya kutojiamini. Siku zote
njia sahihi ya kupambana na matatizo ni kukabiliana nayo, ndio maana sisi
tuliamua kukabiliana na ugonjwa wa corona huku tukiwa tunamtanguliza Mwenyezi
Mungu, na hadi sasa tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa,” aliongeza.
Machi 17,
2020, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliagiza Shule zote kuanzia
shule za awali na vyuo kufungwa, kama hatua za awali za kujikinga dhidi ya
virusi vya corona.
Mei mwaka
huu, Rais Magufuli alitangaza kufungua vyuo na kuruhusu wanafunzi wa kidato cha
sita kurejea shuleni kwa ajili ya kujiandaa na mitihani ya kuhitimu.