Vanessa
Mdee amefafanua kauli yake ya kuacha muziki aliyoitoa hivi karibuni, akieleza
kuwa imetokana na ‘mauzauza’ aliyokutana nayo kwenye tasnia ya muziki, kiasi
cha kuhoji wanaotaka aendelee wanataka afe?
Akizungumza jana jioni
kupitia akaunti yake ya YouTube, Vanessa alisema kuwa kiwanda cha muziki
kilimfanya aishe maisha magumu sana kiasi cha kupata msongo wa mawazo na huzuni
kubwa mara kwa mara.
Alisema kuwa ingawa
watu huwaona wasanii wakiwa na furaha kupitia mitandao ya kijamii, hali iko
tofauti sana kiuhalisia kwani wengi wana maumivu moyoni wanayopitia hadi kuvuna
matunda madogo ya kazi zao.
Vanessa ambaye hivi
sasa yuko ughaibuni, alisema kuwa hawezi kuacha kuimba na kufanya matamasha
kwakuwa ndio sehemu ya maisha yake, lakini hatajihusisha moja kwa moja na
kiwanda cha muziki au tasnia ya muziki kama alivyofanya awali.
Msanii huyo wa kike
ambaye kabla ya kuanza muziki alikuwa mtangazaji, ametoa mfano wa mkulima
ambaye amekuwa akivuna mazao yake vizuri hata mara mbili kwa mwaka na watu
wakamsifu, lakini ndani ya kipindi cha kuandaa shamba hadi mavuno anakuwa
amepitia mateso makubwa kiasi cha kushindwa kufurahia kwa dhati mavuno
aliyonayo.
Amesema mkulima ndiye
unayefahamu anayopitia hadi kupata mazao hayo yanayosifiwa sokoni, lakini kama
anapitia mfumo uleule wa mateso kila mwaka uvumilivu utakushinda.
“Niko kwenye muziki kwa
miaka 13, lakini nimefanya muziki kwa miaka saba na kila mwaka narudia mfumo
uleule, lakini nimekuwa ninafanya kwa kujificha. Sasa, kwa kuficha nimekuwa
ndani naumia. Nataka kumridhisha kila mtu kuanzia mashabiki hadi makampuni
ninayofanya nayo kazi, lakini mimi sina raha, sina furaha kila siku naingia
shambani nang’atwa na nyoka, mavuno ni mazuri lakini mateso ni makubwa,”
alisema Vanessa.
Msanii huyo ambaye
albam yake ya Money Mondays imevunja
rekodi ya kuwa albam iliyosikilizwa na kupakuliwa mara nyingi zaidi mtandaoni
kwa Afrika Mashariki, alisema kuwa anaelewa kila biashara ina changamoto,
lakini biashara nyingi zenye changamoto tofauti na ilivyokuwa kwenye muziki
zinatoa ahadi na matumaini ya kubadilika siku za usoni.
Ameongeza kuwa kutokana
na hali hiyo, alikuwa anapata matatizo ya afya ya akili ambayo yamesababisha
madhara makubwa.
“Watu wengi hawawezi
kuelewa mental health (afya ya akili), sio kitu ambacho waafrika tunaona kama
kina umuhimu, kama akili yako haiko sawa, kuna msongamano wa mawazo… kama una
msongo wa mawazo, una presha nyingi, inakuweka katika nafasi ambayo hauna
furaha na maisha yako na huwezi kuendelea mbele wala kufanya kitu chochote,”
alisema.
“Kwahiyo, unakuwa
unatembea tu kama roboti unafanya vile vitu unavyotakiwa kufanya kwa sababu ni
kazi,” Vee Money aliongeza.
Alizungumzia pia
mitazamo ya watu wengi kwenye mtandao wa kijamii wanaomsihi kutoachana na
kiwanda cha muziki.
“Kuna mitazamo mingi
sana [kuhusu kuachana na tasnia ya muziki]. Je, mgependa kusikia baada ya miezi
au miaka kadhaa ‘Vanessa alikufa’, au ‘Vanessa alipata majeraha zaidi ya kiafya
na kimwili na kiakili’. Kwa sababu gani, hatujui,” Vanessa amefunguka zaidi.
Mkali huyo wa ‘Bambino’
alisema kuwa ni dhahiri kuwa kila mtu anaonja umauti, lakini kuna vitu vingine
vinaweza kuepukika na amechagua kuviepuka.
Katika hatua nyingine,
Vanessa alieleza kuwa baada ya kupata nafasi ya kuwa chini ya lebo ya Kimataifa
ya ‘Universal Music Group’, alijua atapiga hatua kubwa sana ikiwa ni pamoja na
kuongeza nafasi ya kuuza kazi zake duniani. Anasema alichokiona baada ya
kufanya kazi na lebo hiyo ni bora angeendelea kufanya kazi mwenyewe kwani ahadi
zilikuwa nyingi na kubwa lakini kwenye utekelezaji ni mitihani mikubwa.
Msanii huyo hivi sasa
anafanya kazi na lebo yake ya ‘Mdee Music’. Amesisitiza kuwa ataendelea kufanya
nyimbo na kutumbuiza lakini hatajihusisha moja kwa moja na tasnia ya muziki.
Vanessa alianza kung’aa
kwenye kiwanda cha muziki baada ya kuachia wimbo wa ‘Closer’ alioutoa mwaka
2013 akiwa chini ya lebo ya ‘B’Hitz’, wimbo ambao ulimpa tuzo.
Alianza muziki kama
rapper, akabadili gia angani na kuwa muimbaji aliyepata nafasi kwenye anga la
Kimataifa. Nyumbani alifanya ziara kubwa akiwa na mpenzi wake Jux, iliyoitwa
‘In Love and Money’.