WANANCHI wa Kijiji cha Mgazi kilichopo Igunga mkoani Tabora wameondoka na kero ya muda mrefu ya kupata maji baada Shirika lisilo la kiselika la Kusaidia na Kuhamasisha Maendeleo (DESPO) lenye makao yake makuu Mkoa wa Tabora kufanikiwa kuwachimbia bwawa na kupeleka maji katika kijiji hicho.
Mafanikio ya kazi hiyo ya kupeleka maji katika kijiji hicho yametokana na ushirikiano mkubwa baina ya shirika hilo, wananchi wa Kijiji cha Mgazi na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kwa Ufadhili wa Mfuko wa Ushirikiano wa Tanzania na Japan uitwao (Tanzania/ Japan Food Aid Counterpart Fund) .
Akizungumza jana katika hafla ya kukabidhi mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Fedes Mdala alisema mradi huo umechukua miaka mitatu hadi kukamilika.
Mdala alisema Julai 27, 2013 shirika hilo lilipokea barua kutoka ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Mgazi ikiomba mradi wa kuchimbiwa bwawa la maji kwa ajili ya matumizi ya mifugo.
Alisema katika barua hiyo, ilielezwa kuwa ifikapo mwezi wa nane visima vilivyopo hukauka na wananchi kulazilimika kutembea umbali wa hadi kilometa 12 kwa ajili ya kupata maji na wakati mwingine kulikuwepo na magonjwa ya mlipuka kutokana na ukosefu maji ya kutumia majumbani na pia kumekuwepo na kesi za kubakwa wanawake na magomvi ndani ya ndoa kutokana na muda mwingi ambao wamama wamekuwa wakitumia kwenda kutafuta maji.
Mdala alisema kutokana na hali hiyo Halmashauri ya Wilaya pamoja na Mbunge walifanya jitihada za kutafuta suruhisho la changamoto ya maji lakini kutokana na ufinyu wa bajeti jambo hilo halikuwa limewezekana.
"Kwa shida iliyokuwepo wananchi walichangishana fedha kwa ajili ya kuanzisha mradi wa maji hadi kiasi cha Tsh 750,000/= lakini kwa bahati mbaya haikuwezekana" alisema Mdala.
Alisema baada ya kupokea barua hiyo uongozi wa DESPO uliketi na kutathmini ombi hilo, na baadaye timu ya wataalam walifika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya kujirizisha zaidi juu ya changamoto iliyoripotiwa na Kijiji cha Mgazi.
Alisema Ofsi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ilitoa ushirikiano mkubwa kwa kuteua mtumishi mmoja ambaye aliongoza timu ya wataalam hao kutoka DESPO kwenda Kijiji cha Mgazi kwa ajili ya kukutana na uongozi wa kijiji na kujionea hali halisi ya tatizo la maji.
Alisema katika ziara hiyo iliyofanyika mwezi Oktoba 2013, timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na DESPO ilifanya kikao na Viongozi wa Serikali ya Kijiji kujadili changamoto ya uhaba wa maji kwa matumizi ya mifugo pamoja na binadamu katika kijiji hicho.
"Timu hiyo ilifanikiwa kuona vyanzo vilivyokuwa vinatumiwa kwa ajili ya kupata maji na ukweli hali ile ilisikitisha sana kuona wapo binadamu ambao hadi karne hii tena kwenye zama hizi wanaweza kutumia maji yaliyochanganyika na udongo tena yanapatikana kwa shida" alisema Mdala.
Alisema baada ya hapo mchakato wa kuanza ujenzi wa mradi huo ulianza huku Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ikiwa mstari wa mbele katika kuhakikisha shughuli zote za mradi zinakamilika kwa kiwango kilicho kusudiwa kwa kutoa usafiri, wataalamu, na wasimamizi wa mradi.
Akizungumzia ushiriki katika mradi huo Ofisi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Igunga, alisema imekuwa mstari wa mbele kwa kuhakikisha umoja wa watumiaji maji wa Mgazi unakamilika na kusajiliwa. Lakini pia Meneje wa RUWASA, Christopher Saguda, ambaye kwa bahati nzuri ndiye alikuwa Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kabla ya kuteuliwa nafasi aliyonayo kwa sasa, ameshiriki kwa sehemu kubwa katika ufuatiliaji na ufanikishaji wa mradi huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Revocatus Kuuli, alilipongeza shirika hilo kwa kukamilisha mradi huo na kuomba kupeleka mradi mwingine katika wilaya hiyo.
"Nawaombeni mtuletee mradi mwingine na mradi mlioukamilisha utakuwa wa mfano katika wilaya yetu na mikoa mingine hongereni sana" alisema Kuuli.
Kuuli aliwataka wananchi wa kijiji hicho kuutunza mradi huo na kuwa mtu atakaye bainika kuuhujumu hawata muonea huruma.
Katika hatua nyingine Kuuli aliwaomba wananchi hao kuyachemsha maji hayo kabla ya kunywa ili kujikinga na maradhi ya matumbo.