Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amesema kwa mara nyingine tena
kuwa watu watumie petroli kuosha barakoa - na kusisitiza kwamba hafanyi mzaha.
Alisema maneno kama hayo wiki iliyopita lakini maafisa
walimrekebisha haraka sana na akasema kwamba huo ulikuwa mzaha.
Maafisa wa afya wanasema kuwa barakoa zilizotengenezwa kwa
kitambaa cha nguo zinatakiwa kuoshwa kama kawaida na zile barakoa zingine zitumike
mara moja tu na kutupwa.
Lakini Ijumaa, rais huyo alisisitizia matamshi yake na kuongeza
"kile nilichosema ni ukweli… nendeni kwenye kituo cha petroli".
Hakuna ushahidi wowote kwamba petroli inaweza kutumiwa kuua
vijidudu kwenye barakoa; na kuitumia kwa muda mrefu kunaweza kusababisha hatari
na kuinyunyizia vioevu kunaweza kusababisha moto.
Duterte alisema nini?
Akirejelea matamshi yake ya awali, Bwana Duterte alisema:
"Wakosoaji wanasema, 'Duterte ana kichaa.' Ni mpumbavu! Ikiwa mimi ni
mpumbavu, wewe unastahili kuwa rahisi, sio mimi.
"Kile nilichosema ni cha kweli. Ikiwa pombe haipatikani,
hasa kwa maskini, nenda tu kwenye kituo cha petroli, na utumie petroli kuua
vijidudu.
"Sio utani. Sio mzaha. Wewe… wewe jitahidi kuwa na mawazo
kama yangu."
Alisema nini wiki iliyopita
Bwana Duterte alisema wale ambao hawana vifaa vya kusafisha
wanaweza kutumia petroli kusafisha barakoa zao.
"Mwisho wa siku, tundika [barakoa] sehemu na uinyunyize
dawa ya kuzuia na kuua bakteria ya Lysol kama una uwezo," alisema, akirejelea
dawa maarufu ya kuua vijidudu.
"Kwa watu wasio na [Lysol], itumbukize kwenye petroli au
diseli... tafuta petroli kidogo na utumbukize mikono yako ikiwa imeshika
barakoa."
Baada ya matamshi ya wiki iliyopita, msemaji wa serikali Harry
Roque mara moja alimrekebisha.
"Siwezi kuamini kwamba baada ya miaka minne ya urais, bado
hujui [yeye]," amesema Bwana Roque, kwa mujibu wa tovuti ya habari ya
Rappler.
"[Ni utani] tu. Kwanini tutumie petroli kuosha kitu?"
Wakati huohuo afisa wa afya Maria Rosario Vergeire amesema
barakoa za nguo zinastahili kuoshwa na kukaushwa kama kawaida, na zile zingine
zitumiwe mara moja na kutupwa.
Hali ya corona iko vipi Ufilipino?
Alhamisi, nchi hiyo ilirekodi waathiriwa 3,954 kwa siku, na
kufikisha idadi jumla hadi 89,374.
Pia vifo chini kidogo tu ya 2,000 vyenye kuhusishwa na corona
vimerekodiwa.
Bwana Duterte Ijumaa alitangaza kwamba masharti ya kukabiliana
na virusi vya corona bado yanaendelea kutekelezwa katika mji wa Manila hadi
katikati ya August.
Mji wa Manila sasa hivi ni kama upo kwenye karantini - na
kupunguza uhuru wa kutembea kwa watu wenye umri mkubwa na watoto, pamoja na
utekelezaji wa masharti mengine yaliowekwa.
Rais pia aliahidi kuwa chanjo ya bure itatolewa punde baada ya
kupatikana huku wenye kipato cha chini nchini humo wakipewa kipaumbele.