
Rais wa Tanzania, John Magufuli amemkabidhi eneo la hekta 52
mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu na kumtaka kuliendeleza kwa ajili ya
wakazi wa jimbo la Kibamba na Ubungo.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi ameeleza hayo leo Jumatano Februari
24, 2021 katika uzinduzi wa kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli Dar es Salaam.
“Ninaagiza ndani ya siku tatu Wizara ya Kilimo itoe hati, leo
Jumatano kabla ya wiki haijaisha Ijumaa wawe wamekabidhiwa, mbunge na watu wake
wakabidhiwe wakaisimamie , ila mkaiendeleze kwa faida ya wananchi wanyonge wa
eneo la Kibamba,” amesema Rais Magufuli.
Akizungumza awali Rais Magufuli alimmwagia sifa mbunge huyo kwa
kuonyesha unyenyekevu.
“Nilikuwa namsikiliza mbunge Mtemvu alivyokuwa akijaribu kujieleza
hapa tuliwakosa muda mrefu wabunge wa aina yake na saa zingine tuwe tunajilaumu
kwa kukosea kuchagua alipokuwa akiomba pale akinyenyekea mimi nimeguswa sana.”
“Nakupatia hekta 52 bure ukaziendeleze kwa ajili ya wananchi
hawa nikitoka sijakupa nitatoka na uchungu umenifurahisha sana, hongera sana
Mtemvu na wananchi wa Kibamba kwa kufanya mabadiliko makubwa,” amesema Rais.
Amesema alishangazwa mbunge huyo alipoomba kwa unyenyekevu
kujengewa barabara za kiwango cha lami na kumwagiza mtendaji mkuu wa Wakala wa
Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale kuambatana na Mtemvu kuona ni
barabara ipi wataanza nayo.
“Mfugale kapite na mbunge uniletee mapendekezo kujua akajenge barabara ipi katika jimbo la kibamba na Ubungo , yaani nafurahi sana jamani Dar es Salaam mmenifurahisha ukigeuka huku Mtemvu huku Chaurembo, unapokuwa kiongozi lazima upate watu wanaowakilisha watu usipopata connection hii mambo hayaendi ni viongozi wanaojituma .” amesema.
Post a Comment