} });
 

Rais wa MAT, Dk Shadrack Mwaibambe

Mwenendo wa ugonjwa unaosababisha changamoto ya upumuaji umewaibua madaktari ambao wamesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa hao sehemu mbalimbali za nchi.

 

Katika siku za karibuni suala hilo la upumuaji limekuwa likitajwa maeneo mengi nchini kiasi cha Mbunge wa Mbulu Mjini (CCM), Zachary Isaay kuibua suala hilo bungeni akidai jimboni kwake watu wengi wameathirika na tatizo hilo.

Kufuatia hali hiyo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) jana kimetoa tamko kikifafanua kuwa changamoto ni dalili tu ya ugonjwa ambao unaweza kuwa ni nimonia, pumu, magonjwa ya moyo, hatua za mwisho za mgonjwa kabla hajafariki au Covid -19.

 

Katika tamko hilo, Rais wa MAT, Dk Shadrack Mwaibambe alisema changamoto katika sekta ya afya zipo na haziwezi kutatuliwa kwa siku moja, lakini zile zinazohatarisha maisha na afya za madaktari lazima tahadhari zitolewe na wenye wajibu wa kuzitatua watimize wajibu wao.

 

Dk Mwaibambe alisema pamoja na kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wenye changamoto hiyo, MAT inawataka madaktari wazingatie kiapo cha taaluma yao na waendelee kuwahudumia wagonjwa bila kujali rangi zao, kabila au aina ya ugonjwa walionao huku wakizingatia hatua za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.


“Katika kuzuia magonjwa ya mlipuko, hususani mlipuko mpya, hakuna nchi ambayo ina uhakika wa asilimia 100 wa mbinu zake. Kila nchi inajaribu mbinu zake inazoona zinafaa kulingana na jinsi walivyouelewa ugonjwa na aina ya maisha ambayo watu wake wanaishi,” alisema.

 

Dk Mwaibambe aliwataka madaktari watumie ujuzi wao kitaaluma na kuendelea kuwaelimisha wagonjwa na Watanzania kwa ujumla kufika vituo vya kutolea huduma za afya haraka iwezekanavyo mara wanapopata dalili za magonjwa mbalimbali.

 

“Chama cha madaktari kinawasisitiza wananchi wote kwa ujumla kuondoa hofu, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono, kuvaa barakoa, watu wachache kwenye misiba na mazishi na kuzingatia maelekezo mengine yote yanayotolewa na wizara pamoja na wadau wengine wa afya,” imeeleza taarifa hiyo.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top