![]() |
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega |
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah
Ulega amesema watawapa wasanii misamiati mipya kwa ajili ya kuitumia kwenye
nyimbo zao ili kukuza lugha ya Kiswahili.
Ulega ameeleza hayo leo Jumanne Machi 2, 2021 alipotembelea
makao makuu ya Uhamiaji pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Ziara
hiyo ililenga kuhamasisha na kukuza lugha ya Kiswahili kwa taasisi hizo katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Amesema Kiswahili ni lugha adhimu inayopaswa kukuzwa na kusambaa
katika nchi mbalimbali, akibainisha kuwa kuwapa wasanii misamiati mipya
itakayotolewa na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) itasaidia kukuza
lugha hiyo.
"Kwa mujibu wa kanuni za Bakita za mwaka 2019 zinaelekeza
kazi za wasanii kupelekwa kwenye baraza hilo kusanifiwa kabla ya kuingizwa
sokoni. Bakita wana misamiati mingi mipya ambayo tunaweza kuwapa wasanii
kuitumia ili kukuza lugha hii.”
"Sasa hivi watoto wadogo hasa wa shule za awali wanaimba
kwa ufasaha nyimbo za wasanii wetu maarufu akiwemo Daimond, Alikiba, Zuchu na
Harmonize. Hawa wana fuasi na mashabiki wengi kupitia kwenye akaunti zao na
wanasikilizwa nje na ndani ya nchi kwa hiyo wakiweka misamiati mipya itasaidia
sana," amesema Ulega.
Ulega amewataka Bakita kutojifungia ndani badala yake watoke nje na kuwafuata wasanii kwa ajili kuwapa misamiati wakati ukifika.
Ulega amesema hatua hiyo itasaidia pia kupanua wigo wa misamiati ya Kiswahili na kurasimisha maneno na istilahi zilizoeleka kwenye jamii.
Post a Comment