} });
 

 

CCM baada ya kupita kwenye milima na mabonde ya uongozi wa makatibu wakuu kadhaa, sasa kinahitaji kupata katibu mkuu atakayekifanya kijitegemee.

 

Pia awe atakayejali masilahi ya watumishi wa chama hicho na akifanye kiwe chachu ya kusisimua siasa badala ya kuziminya bila kusahau misingi ya kuasisiwa kwake.

 

Kwa utamaduni wa CCM, jina la katibu mkuu hupendekezwa na mwenyekiti wa chama taifa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

 

Hivyo, nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa CCM ni utashi wa mwenyekiti mwenyewe.

 

Wajumbe wa NEC wanapopelekewa jina la katibu mkuu, kazi yao huwa kulipitisha na hakuna rekodi za pendekezo la wateule wa mwenyekiti kukataliwa na NEC.

 

CCM ya Mwalimu Nyerere

Muasisi wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kuunganisha vyama vya Tanu na Afro Shiraz (ASP) mwaka 1977 alitaka chama kipya kiwe na alama za wananchi wanyonge, ndio ikawekwa jembe na nyundo na hivyo mtendaji mkuu wa chama anatakiwa kusimamia msingi huo.

 

Wakati wa kuadhimisha miaka 44 ya kuzaliwa CCM, Pius Msekwa ambaye ni katibu mkuu wa kwanza wa CCM aliyeshika nafasi hiyo kuanzia mwaka 1977 hadi 1982, alisema alama hiyo ya jembe na nyundo, maana yake ni chama cha wakulima na wafanyakazi.

 

Katibu mkuu vilevile, anatakiwa kuijua CCM na msingi wake, kwamba ni chama kinachotakiwa kuleta mapinduzi ya maendeleo kwa wananchi.

 

Kwa mujibu wa Msekwa, “baada ya kukamilisha mambo ya katiba jina lilikuwa mwisho. Tulimuuliza Mwalimu akasema kiitwe Chama cha Mapinduzi, sababu vyama viwili vikiungana vitaleta mapinduzi ya maendeleo kwa wananchi,” anasema Msekwa.

 

Hivyo, Chama cha Mapinduzi au CCM kwa kifupi lilitokana na azma ya Mwalimu Nyerere ya kutaka kuleta mapinduzi ya kimaendeleo kwa wananchi.

 

Ni chama cha wanyonge?

Upinzani alioupata mgombea urais wa CCM, Benjamin Mkapa katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa 1995 kutoka kwa mgombea wa NCCR-Mageuzi Augustine Mrema, hiyo ilikuwa ishara ya kwanza kwa kwamba kinaweza kutikiswa

 

Baada ya uchaguzi huo, nguvu ya upinzani iliongezeka na kifo cha Mwalimu Nyerere kilichotokea Oktoba 1999, kuliifanya CCM ilegeze mambo yake mengi.

Ndio wakati kuliibuka wafanyabiashara walioingia kwa ‘gia’ ya walezi wa jumuiya, makamanda wa vijana, matawi ya CCM kuzinduliwa katika maeneo mengi ya biashara, tena maeneo yasiyoruhusiwa. Watu walitumia kivuli cha CCM kuficha maovu yao.

 

CCM ilishindwa kudhibiti nguvu ya fedha kwa wagombea uongozi ndani ya CCM, watu walipata vyeo kwa nguvu ya fedha, safu za uongozi ndani ya chama zilipangwa kwa makusudi na wanaotaka kugombea ubunge au urais.

Mali za chama zilimilikiwa na watu binafsi, baadhi ya viongozi wa CCM walipora magari, majengo na maeneo ya biashara, kodi zilikuwa zikiingia mifukoni mwa viongozi.

 

Kwa muda mrefu chama kimekuwa hakina mfumo mzuri wa kudhibiti mapato na matumizi, hakuna mfumo mzuri wa utunzaji wa kumbukumbu za chama. Mfano, ukitafuta hotuba za wenyeviti, makamu wenyeviti na makatibu wakuu waliopita hazipo popote.

 

Ilizoeleka ada za uanachama zinalipwa na mgombea kama hongo ya kutafuta kuungwa mkono, wana CCM hawakuwa na mapenzi ya dhati kulipa ada ya uanachama kwa hiari yao. Hiyo ndiyo ikawa kiu kubwa ya CCM kupata watendaji wa kuleta mabadiliko.

 

Nani anafaa nafasi hiyo?

CCM inahitaji katibu mkuu atakayeweza kuweka mfumo wa mzuri wa kutambua umuhimu wa watumishi wa chama na namna wanavyotakiwa kuwajibika.

 

Katibu mkuu anatakiwa awe na sifa na ushawishi anapotoa hoja kwenye majukwaa ya kisiasa, awe na mvuto na akiondoe chama kwenye siasa za kutegemea dola na badala yake kijenge mifumo thabiti ya kujibu mapigo ya hoja za wapinzani.

 

Na kwa kuangalia mifano ya utendaji wa baadhi ya makatibu wakuu waliopita hivi karibuni CCM inaweza kupata mmoja anayetosha kwa nafasi hiyo.

 

CCM ya Bashiru

Katibu mkuu mpya anatakiwa kuendeleza yale yaliyoanzishwa na Dk Bashiru Ally hasa kukifanya chama kujitegemea kimapato na kulinda mali za chama.

 

Dk Bashiru alikiwezesha chama kuwa na mfumo wa usimamizi wa fedha na kanuni ya fedha.

 

Pia, alikiwezesha kuanza kujitegemea bila kuomba msaada wa mtu katika uchaguzi mkuu wa 2020, tofauti na chaguzi zingine zilizopita ambazo CCM ilitegemea kuomba michango kwa wafanyabiashara.

 

CCM ya Kinana

Katibu mkuu mpya anatakiwa aweze kuisimamia Serikali itekeleze ilani ya uchaguzi ya CCM kama wakati wa Abdulrahman Kinana. Bila kuwa na mtendaji wa aina hiyo Serikali haitatekeleza ilani.

 

Hivyo, uongozi wa Kinana haukuwa na mchezo kwa watendaji wa Serikali walioonekana kukwamisha miradi ya maendeleo.

 

Alitekeleza maazimio ya mkutano mkuu wa CCM wa kukitaka chama kuisimamia Serikali katika kutekeleza ilani ya uchaguzi wa chama.

 

Ziara za Kinana na viongozi wenzake wa sekretarieti ziliwataja mawaziri walioshindwa kutekeleza majukumu yao na kuwaita ‘mawaziri mizigo.’ Na waliwapeleka kuhojiwa kwenye vikao vya CCM.

 

Pia, anahitajika katibu mkuu atakayeweza kuinua uhai wa chama kwa kufanya ziara na sekretarieti yake kusimamia utekelezaji wa ilani na kusikiliza kero za wananchi ili kuishauri Serikali.

 

CCM ya Mukama

Wakati wa katibu mkuu, Wilson Mukana kulikuwa na hoja ya kujivua gamba, yaani chama kizaliwe upya, kitengeneze mikakati mipya, kitengeneze mbinu mpya za kuweza kusalia madarakani.

 

Hoja ya kujivua gamba ni ya msingi kwa siasa za wakati huu, CCM inahitaji viongozi wenye mawazo mapya, kwa mantiki hiyo kinahitaji kutumia vyuo vyake kuzalisha makada wapya wenye mwelekeo mpya utakaoifanya CCM iwe ya kisasa na yenye kufanya tafiti za namna ya kuendesha siasa.

 

Katibu mkuu mpya anatakiwa kukivua gamba chama ili kiwe ‘kijana’ kama anavyofanya nyoka, kiende na hali ya sasa na kuachana na siasa za kizamani.

 

CCM ya Mangula

Anatakiwa katibu mkuu awe ni mtu mwenye kufuata maadili ya chama. Mfano mzuri ni Philip Mangula ambaye wakati wa uongozi na hata sasa amekuwa ni kiongozi aliyesifika kwa kufuata maadili ya chama na ndio maana alipewa jina la ‘mzee wa mafaili’. Bila maadili chama kitanuka rushwa.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top