Diwani wa
Kata ya Luduga iliyopo wilayani Wanging'ombe, Hassan Ngella amefariki dunia
usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya rufaa mkoani mbeya baada ya kuugua
ghafla.
Hayo yamethibitishwa leo na katibu wa siasa na uenezi wa chama cha mapinduzi
(CCM) Wilaya ya Wanging'ombe, Ruben Nyagawa alipozungumza na gazeti la
Mwananchi.
Amesema taarifa ya kifo cha diwani huyo ameipata usiku wa kuamkia leo akisema
diwani huyo aliugua na kukimbizwa hospitali ya Ilembula iliyopo wilayani
Wanging'ombe.
Amesema baadaye alihamishiwa katika hospitali ya rufaa iliyopo mkoani Mbeya
ambapo aliendelea na matibabu licha ya jitihada zote za madaktari usiku wa
kuamkia leo alifariki dunia.
Amesema taratibu za kichama zinaendelea ili kuona kwamba namna ambavyo chama
hicho kitashiriki mazishi ya diwani huyo.
"Kwa mujibu wa ratiba na taratibu chama na wanandugu mazishi yanatarajiwa
kufanyika hapo kesho," amesema Nyagawa.
Amesema
tukio la kufa sio zuri sana katika maisha ya binadamu lakini diwani huyo
ameacha pengo wilayani humo kwani huwezi kuzungumzia chama hicho wilayani
Wanging'ombe bila ya kumtaja diwani huyo.
Amesema chama hicho kimepoteza mtu mahiti, mchapakazi na mwaminifu kwakuwa
alikuwa akikipenda chama hicho na kufikia kutumia gharama zake binafsi kwa
ajili ya chama.
Amewapa pole wananchi wa kata ya Luduga kwa kuondokewa na diwani wao ambaye
alikuwa anawapenda wananchi wake kwa kutoa muda wake mwingi ili kuwatumikia.
"Nafahamu ameitumikia kata ya Luduga kwa miaka mingi ingawa kuna muda
aliondoka na baadaye alirudi na mwaka jana aliweza kushindana udiwani
wake," amesema Nyagawa.
Amewaomba wananchi wa kata hiyo kushiriki maandalizi ya mazishi ya diwani huyo
huku wakichukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa corona.
Post a Comment