} });
 


Baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya ugaidi ambayo hayana dhamana, swali limebaki ni nini hatima ya chama hicho kikuu cha upinzani.

 

Mbowe alikamatwa na polisi usiku wa kuamkia Julai 21, mwaka huu akiwa Mwanza alipokwenda kuunga mkono makada wa chama hicho waliokuwa wakitayarisha kongamano la Katiba Mpya ambalo lilizuiwa na Jeshi la Polisi.

 

Baada ya kukamatwa alisafirishwa hadi Dar es Salaam ambako alipekuliwa nyumbani kwake, kisha akawekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Oysterbay.


Julai 26, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili ya kula njama na kutoa fedha kufadhili shughuli za ugaidi.

 

Mashtaka hayo yaliyosomwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martin akisaidiana na Tulimanywa Majigo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Alidaiwa kuwa kati ya Mei na Agosti, 2020 katika hoteli ya Aishi iliyopo mkoani Kilimanjaro, mshtakiwa alikula njama za kutenda kosa kinyume cha sheria.

 

Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Agosti 5, 2021 baada ya upande wa mashtaka kusema upelelezi umekamilika na utawasilisha nyaraka muhimu na kusoma maelezo ya mashahidi na vielelezo vyake.

 

Mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza alisema Chadema inaweza kupata athari hasi au chanya.

 

“Kwa athari hasi, kama Chadema watabaki kusononeka kuwa Mbowe ameshtakiwa, basi hapo chama kitadorora. Wasipojidhatiti na kuendelea na harakati za kudai Katiba, chama kitazorota na ndiyo CCM wanachokitaka,” alisema.

 

“Lakini kama Chadema watatambua kuwa hivyo ni vikwazo wanavyowekewa na kupambana navyo kwa kuendeleza harakati zao, chama kitaimarika zaidi na kitakuwa na uzoefu wa kupambana na misukosuko,” alisema.

 

Mchambuzi wa masuala ya siasa ambaye pia ni Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari alisema kinachotokea kwa Mbowe kinaweza kuufanya upinzani kuimarika zaidi nchini.

 

“Kukamatwa kwa viongozi wa vyama hakutaathiri kasi ya upinzani. Ni kweli wapo baadhi ya wanachama watavunjika moyo, lakini wengi wataongeza nguvu,” alisema Profesa Bakari.

 

Kwa upande wake Dk Richard Mbunda ambaye pia ni Mhadhiri wa Siasa UDSM, alisema kesi ya Mbowe inayoendelea ni mtihani kwa Chadema wa kupima udhabiti wa taasisi imara na isiyomtegemea mtu mmoja kuendesha harakati.


Hata hivyo, alisema ni fursa kwa Chadema kuendelea kupata uzoefu wa kukabiliana na misukosuko.

 

“Hata mtu huyo akitikisika shughuli za taasisi zinaweza kuendelea kama kawaida na taasisi ikabaki kuwa imara. Siwezi kutabiri ya kesho lakini ni mtihani unafanyika, hivyo tusubiri majibu yake,” aliongeza Dk Mbunda.


Alisema mtihani huo haupo kwa Chadema pekee bali pia kwa Serikali na Mahakama, kwa kuonyesha kuwa vyombo hivyo viko huru katika kipengele cha kutenda haki na ionekane imetendeka.

 

“Ni mtihani kwa Serikali maana falsafa ya Serikali ya awamu ya sita na kinachotarajiwa ni kutenda haki na haki ionekane inatendeka, watu wanahoji iwapo shutuma hizo ni za kweli au za kubambikizwa kama ambavyo hata Rais (Samia Suluhu Hassan) amewahi kusema kuwa kuna ubambikizaji wa kesi,” alisema Dk Mbunda.

 

Pamoja na kauli za viongozi wa Chadema kuwa wataendeleza shughuli za chama kama kawaida, lakini uwepo wa Mbowe katika chama hicho umekifanya kuhimili vishindo tangu alipochukua uenyekiti mwaka 2004.

 

Akiwa mmoja wa waanzilishi wa chama hicho mwaka 1993, Mbowe alipanda vyeo kutoka mwenyekiti wa Umoja wa Vijana hadi kuwa mwenyekiti wa Taifa mwaka 2004 akirithi mikoba ya Bob Makani.

 

Chini ya uongozi wake, chama hicho kiliongeza idadi ya wabunge na madiwani kutoka watano wa kuchaguliwa na viti maalumu hadi kufikia zaidi ya wabunge 70 mwaka 2015.

 

Hata hivyo, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, chama hicho kilijikuta kikibaki na mbunge mmoja wa kuchaguliwa huku vigogo wengi akiwemo Mbowe wakianguka dhidi ya wagombea wa CCM kwenye uchaguzi ambao ulikuwa na malalamiko kutoka kwa wapinzani.

 

Wakati huu ambao Chadema imeanzisha ajenda ya kudai Katiba Mpya, Mbowe alionekana kuwa mstari wa mbele akiongoza hatua kwa hatua.


Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anayeishi Ubeligiji, alisema shughuli za chama zitaendelea kama kawaida.

 

Naye Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema alisema licha ya kuwa Mbowe hayupo, shughuli zinaendelea kama kawaida na hivi karibuni watatangaza ratiba.

 

“Tuna makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar, shughuli zinaendelea na wanaendesha vikao vya chama na hivi karibuni tutatangaza ratiba, hayo ndiyo maamuzi ya kamati kuu,” alisema Mrema.

 

Mbali na Lissu, mjumbe mwingine wa kamati kuu ya chama hicho mwenye ushawishi mkubwa, Godbless Lema naye kwa sasa anaishi Canada. Lema aliondoka nchini kupitia mpaka wa Namanga kwenda Kenya, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu akidai kuhofia usalama wa maisha yake.

 

Bawacha watinga ubalozi wa Marekani

Wakati hayo yakiendelea, Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) limesema liko tayari kuongoza mapambano ya kudai Katiba Mpya licha ya Mbowe kuwa gerezani.

 

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge alisema hawatarudi nyuma, wataendelea kudai Katiba Mpya hadi itakapopatikana.


“Kuna wengine tunaweza tusifike mwisho wa hii safari, lakini tuko tayari kuendeleza mapambano kwa mustakabali wa vizazi vyetu, ambao hatutafika wapo wengine watabaki kuendeleza safari hii,” alisema Catherine.

 

“Kukamatwa mwenyekiti wetu (Mbowe), si mwisho wa kudai Katiba Mpya, moto ndio kwanza umewaka,” aliongeza Catherine ambaye jana aliwaongoza baadhi ya makada wa baraza hilo kwenda Ubalozi wa Marekani nchini kuwasilisha kilio chao cha kudai Katiba Mpya wakiwa na mabango kuhusu kushikiliwa kwa Mbowe.

 

Wakiwa ubalozini hapo, Bawacha walipokewa na kuwasilisha ujumbe kwa Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Siasa, Douglas Morris na kueleza malalamiko yao.


“Kati ya mambo ambayo tumelalamika ni uvunjwaji wa demokrasia pamoja na kukamatwa kwa mwenyekiti, tumeomba waingilie kati kwa kuwa Marekani ni Taifa kubwa lililokomaa katika demokrasia.

 

Pia, ni nchi rafiki na Tanzania,” alisema Catherine aliyechaguliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top