
Siku tano
tangu Sheria ya Kodi ya Miamala ya Simu ianze kutumika, Chama cha watoa huduma
za fedha kwa simu za mkononi (Tamnoa), kimesema biashara imeshuka kwa kiasi
kikubwa na kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kusitisha makato mapya.
Mwenyekiti
wa Tamnoa, Hisham Hendi alisema mamilioni ya wateja wameacha kutumia huduma zao
hasa wale wa vijijini, kutokana na ongezeko la gharama jambo linalotishia
biashara zao.
“Wateja
wanalalamika sana hasa vijijini ingawa tunaendelea kutoa huduma bora kadri
tuwezavyo tukitambua kwamba huduma za fedha kwa simu ya mkononi ni huduma
muhimu kwa jamii. Tunaamini Serikali italiona hili na itachukua hatua stahiki
kuokoa jahazi kwani kodi hii inaathiri biashara na kuwaumiza wananchi,” alisema
Hendi kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa na Tamnoa.
Pamoja
na kupoteza biashara, kampuni za mawasiliano zinazotoa huduma za fedha ambazo
ni Vodacom (Mpesa), Tigo (Tigopesa), Airtel (Airtel Money), Halotel (Halopesa),
Zantel (Eazypesa) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Pesa), zimesema kodi
hiyo inawapunguzia ushindani sokoni pamoja na kupunguza ari ya kuwekeza zaidi.
Hata
hivyo, wakati hali ikiwa hivyo kwa kampuni za simu, mambo ni tofauti kwa benki
na taasisi za fedha nchini ambazo zimekuwa zikitoa matangazo yanayoonyesha kuwa
zinatoa huduma nafuu zaidi ya miamala ya fedha kuliko washindani wao.
“Tunajiuliza
lakini hatupati majibu kwa nini benki hazishiriki kukusanya mapato haya muhimu
kwa Serikali kama ilivyo kwa kampuni za simu, ilhali wanatoa huduma kama zetu
kama wanavyojieleza kwenye matangazo yao,” inasema taarifa ya Tamnoa.
Kuhusu
usawa wa kodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPFS),
Francis Nanai alisema mfumo mzuri wa kodi ni ule unaowahusisha watu wengi, huku
kodi ikitozwa kwa viwango vidogo.
“Wazo
la kuanzisha kodi ya miamala lilikuwa zuri ila viwango vinavyotozwa ndio sio
rafiki. TPSF tunasikia malalamiko lakini tunaamini hakuna linaloshindikana.
Serikali ikae na wadau kujadili upya viwango hivi na benki zisiachwe katika
hili. Kutokana na teknolojia, simu nayo ni benki. Wapo watu wanakopa au kuweka
akiba kwenye simu zao,” alisema Nanai.
Kwa
kusikiliza maoni yanayotolewa na watoa huduma, wateja na mawakala wa huduma za
fedha kwa simu za mkononi, mkurugenzi huyo alisema kuna haja ya kufanya utafiti
kujua namna sahihi zaidi ya kutekeleza kodi hii.
Kukosekana
kwa mazingira sawa ya ushindani, chama hicho kimesema ni suala linalowaumiza
kichwa, ingawa wanaamini Serikali italiona hilo na kulifanyia kazi ili kuweka
mazingira rafiki ya kuwekeza na kufanya biashara.
“Wanahisa
na wawekezaji wetu wana wasiwasi na hali ya ushindani nchini. Wanafuatilia kwa
ukaribu sana,” alisema Hendi kwenye taarifa hiyo ya watoa huduma.
Tofauti
na sekta ya benki ambako benki kubwa nyingi ni za kizalendo, kampuni nyingi za
mawasiliano ni za wawekezaji kutoka nje ambao wasiporidhika kuwekeza nchini,
wanaweza kutafuta fursa mahali pengine.
Wawekezaji
wakubwa wa Vodacom, kampuni inayoongoza kwa wateja na uwekezaji nchini ni
Vodacom Group ya Afrika Kusini, wakati Tigo inayoimiliki pia Zantel, imepata
mwekezaji mpya kutoka Madagascar, kampuni ya Axian Group baada ya Millicom
International Cellular kutangaza kujiondoa Afrika.
Ingawa
Serikali inazo hisa ndani ya Airtel ila mwanahisa mkubwa ni Airtel Group ya
India huku Halotel ikimilikiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Vietnam.
Shirika
la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ndiye mtoa huduma pekee anayemilikiwa na
Serikali kwa asilimia 100, lakini anahudumia wateja wachache zaidi wa
mawasiliano, intaneti hata huduma za fedha.
Upande
wa pili, benki zenye mtandao mkubwa zaidi wa matawi na hata miundombinu ya
kuwahudumia Watanzania wengi ni NMB na CRDB, huku kwa pamoja zikimiliki
asilimia 40 ya thamani ya sekta hiyo. Benki hizi, kwa kiasi kikubwa
zinamilikiwa na wazawa. Nchini kuna zaidi ya benki 60 zinazotoa huduma.
Kutishika
kwa wawekezaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Huduma za Fedha
Tanzania (FSDT), Sosthenes Kewe alisema linapaswa kutazamwa kwa umakini ili
waendelee kuiona Tanzania ni sehemu salama kwao.
“Matangazo
ya benki yanaonekana mitandaoni. Linapokuja suala la kodi, mlipaji anatakiwa
kulipa kwa namna zote zinazowezekana na asiwepo wa kuachwa. Kama Serikali
iliona kuna fursa kwenye miamala ya kielektroniki sijui kwa nini iliziacha
benki. Kama kodi inatozwa kwenye miamala ya kidijitali hata akaunti ya benki ni
dijitali pia,” alisema Kewe.
Imani kwa Serikali
Katika
kutafuta nafuu, Hendi alisema kampuni za mawasiliano zinaendelea kuwasiliana na
Serikali pamoja na Bunge kueleza hoja zao anazoamini zitafanyiwa kazi kwa
mustakabali mwema wa Taifa.
Alisema
wanachukua hatua hizo kwa kutambua kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi huko
mbele, kwani tayari siku nne za kuanza kwa makato hayo biashara haiendi vizuri.
“Mapato
yameshuka kwa kiasi kikubwa kwa sababu wateja hawatumii huduma zetu kama
ilivyokuwa mwanzo. Hali si nzuri,” alisema.
Kuhusu
kodi ya muda wa maongezi inayotarajiwa kuanza siku chache zijazo, Hendi alisema
wanazungumza na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupata namna nzuri ya
kutekeleza hilo bila kuathiri biashara iliyopo.
Akifafanua
kwa nini benki hazishirikishwi kutoza kodi ya uzalendo kwenye miamala yao ya
kidijitali, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini katika Wizara ya Fedha
na Mipango, Benny Mwaipaja alisema huu ni mwanzo huko mbele kutakuwa na fursa
ya kutanua wigo.
“Watu
wakielewa tunaweza kutanua maeneo ya kukusanyia kodi hii. Tumeanza tu kwenye
miamala ya simu lakini huko mbele tunaweza kuangalia namna ya kutanua zaidi
wigo na tukazihusisha benki za biashara,” alisema.
Tume ya Ushindani na Benki Kuu
Alipotafutwa
ofisa mwandamizi wa habari na mawasiliano wa Tume ya Ushindani (FCC), Frank
Mdimi alisema mkurugenzi mkuu wa tume hiyo anaweza kulizungumzia vizuri zaidi
suala hilo.
“Ninachofahamu
ni kwamba benki huwa zinatoa taarifa za gharama zao mara kwa mara ili wateja
wao wazifahamu. Ukimpata mkurugenzi atakueleza vizuri zaidi. Unaweza kuwatafuta
Benki Kuu pia wao ndio wasimamizi wa taasisi za fedha,” alishauri Mdimi.
Alipotafutwa
mkurugenzi mkuu wa FCC, William Erio alisema tangu kuanza kuanza kutumika kwa
sheria hiyo hajafuatilia taarifa hivyo hajui kinachoendelea.
“Sijafuatilia
televisheni wala redio. Kuna mambo yamenibana na hapa nilipo najiandaa kwenda
kijijini,” alisema Erio.
Hata
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga hakuwa na
ufafanuzi wa kutosha kwenye jambo hilo akipendekeza atafutwe Waziri wa Fedha na
Mipango.
“BoT ni regulator wa monetary sector (msimamizi wa sekta ya fedha). Masuala ya mapato ya Serikali hasa kodi ni ya wizara,” alisema Profesa Luoga.
Post a Comment