Na Faustine Gimu Galafoni, Maswa - Simiyu.
Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imedhamiria kufikisha uzalishaji wa tani laki moja na elfu thelathini[130,000 ]za zao la pamba katika msimu wa 2021/2022.
Akizungumza na DIVINE FM Julai 27,2021 Afisa Kilimo halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Gimu Yohana amesema lengo ni kuongeza uchumi wa Taifa katika utekelezaji wa kampeni ya uongezaji thamani zao la Pamba nchi nzima ambapo matarajio ni uzalishaji wa tani za pamba milioni moja kote nchini.
Aidha,Afisa kilimo huyo ameainisha upandaji wa vipimo vipya vya zao la pamba kwa msimu wa 2021/22 ni sentimita 60 kati ya mstari na mstari na sentimita 30 kati ya shimo na shimo .
Baadhi ya Wakulima wa zao la Pamba Wilayani Maswa mkoani Simiyu wakizungumza kwa nyakati tofauti na kituo hiki Julai,27.2021 akiwemo Diwani wa viti Maalum tarafa ya Sengerema, Maswa Julieth Mongo wamesema hali ya soko ya zao la pamba inaridhisha ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo bei ya zao hilo ni Tsh.1400 hadi 1500 kwa kilo ikivuka lengo kwa bei elekezi ya serikali ambayo ni Tsh. 1050.
Ikumbukwe kuwa mkoa wa Simiyu umedhamiria kuongeza tija uzalishaji zao la pamba kutoka kilogram 200 kwa ekari hadi kilogram 800 na 1000 kwa ekari kwa msimu ujao 2021/2022 lengo ni uzalishaji wa tani laki tano na ifikapo Septemba 15,2021 kila mkulima anatakiwa kuhakikisha masalia yote ya pamba shambani yawe yameshang’olewa na kuchomwa moto ambapo balozi wa Pamba Tanzania Agrey Mwanri atafika Wilayani Maswa kuhamasisha kilimo cha pamba.
Post a Comment