} });
 


Zaidi ya abiria 50 wametekwa nyara na watu waliojihami kwa silaha nzito za kivita katika Jimbo la Sokoto nchini Nigeria. Mamlaka za usalama katika Jimbo la Sokoto, wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo, lililotokea Jumapili ya Julai 25, majira ya jioni huku zikishindwa kutoa idadi kamili ya watu waliotekwa.

 

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, abiria hao walikuwa wakisafiria mabasi tofauti, yakiwemo matatu yanayomilikiwa na Mamlaka ya Usafiri Jimbo la Sokota, SPORA yaliyokuwa yakifanya safari zake kupitia Barabara Kuu ya Sokoto- Gusau.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea Jumapili asubuhi ambapo wapiganaji hao waliokuwa na silaha nzito, walikuwa wakifyatua risasi hewani na kusimamisha mabasi yenye abiria kisha kuwateka abiria na kutokomea nao porini.

 

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, Meneja wa Usafirishaji wa Umma katika Jimbo la Sokota, Yahusa Chika, amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akieleza kwamba taarifa walizonazo, zinaonesha kwamba miongoni mwa mabasi yaliyotekwa, yapo mabasi yanayomilikiwa na serikali.

 

Chika ameeleza kwamba watu wawili walifanikiwa kutoroka kutoka kwenye mikono ya wapiganaji hao ambao bado haijafahamika kwa nini wameyateka mabasi hayo.

 

Shuhuda mmoja ambaye ni mwendesha pikipiki, Abubakar Umar, amesema ameshuhudia zaidi ya watu 50 wakitekwa katika tukio lililochukua zaidi ya dakika 30 kwenye barabara hiyo.

 

Shuhuda huyo anaeleza kwamba, akiwa kwenye pikipiki yake, alisikia milio mingi ya risasi, akalazimika kusimamisha pikipiki yake na kujificha pamoja na waendesha pikipiki wenzake, ambapo ndipo waliposhuhudia tukio hilo.

 

Anaeleza kwamba baada ya majambazi hao kukamilisha zoezi hilo, walitokomea porini wakiwa na abiria waliowateka, ambapo anasema eneo la tukio kulikuwa na magari kadhaa yakiwemo mabasi ambayo yote yalikuwa tupu.

 

Mashuhuda wengine wanaeleza kwamba wameshindwa kuelewa ni kwa nini utekaji huo umefanyika kirahisi wakati kuna vizuizi vya polisi, maafisa uhamiaji na wanajeshi katika eneo la kuanzia Tureta mpaka Lamar Bakura ulipotokea utekaji huo.

 

Inaelezwa kwamba hii si mara ya kwanza kwa wapiganaji hao wanaohisiwa kuwa ni kutoka Kundi la oko Haram, kuwateka abiria katika barabara hiyo katika Jimbo la Sokoto  majimbo mengine yaliyopo Kaskazini Magharibi ambapo baadaye hudai fidia kubwa kutoka kwa serikali ili kuwaachia mateka hao.

 

Siku chache zilizopita, wapiganaji hao waliitungua ndege ya kijeshi, iliyokuwa inafanya doria ya kupambana na maharamia hao katika Jimbo la Zamfara nchini humo.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top