} });
 

Polisi Mkoa wa Rukwa inamshikilia kijana mmoja (35) mkazi wa Kata ya Chanji kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Thomas Mremi (85) na kumzika kimyakimya nyumbani kwao. 

Mremi, aliyekuwa ofisa mstaafu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza aliyestaafu utumishi wa umma akiwa na cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP), aliuawa usiku pasipo watu kufahamu. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, William Mwampaghale alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo juzi, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa. 

Alisema mtuhumiwa, ambaye hakumtaja jina kwa kuwa uchunguzi unaendelea, anadaiwa kumuua baba yake huyo kwa kumpiga kichwani na kitu kizito katokana na kuwepo kwa mzozo wa muda mrefu kati yao, ambapo mtoto huyo alitakiwa kuondoka nyumbani na baba yake kwa sababu amefikia umri wa kujitegemea. 

“Baada ya kuhakikisha kuwa amemuua baba yake, mtuhumiwa aliifunga miguu ya marehemu kwa kamba na kumburuza hadi nje ya nyumba ya marehemu huyo ambako aliutupia mwili wake katika shimo alilokuwa amelichimba kisha akalifukia kwa udongo na nyasi kavu na kuzirundika juu ya “kaburi’ hilo kisha akazichoma moto ili ionekane ni jalalani,” alidai Mwamapaghale. 

Alisema: “Mtuhumiwa alikuwa Moshi, mkoani Kilimanjaro, lakini aliposikia baba yake anataka kuuza nyumba hiyo, alirudi haraka Sumbawanga na kukuta wapangaji wote wamehama. 

Alisema kuanzia wakati huo hadi mauti yanamkuta marehemu alikuwa akiishi na mwanawe huyo. “Mpaka sasa haijafahamika mauaji hayo yalifanyika lini, ingawa mwili wa marehemu unaonyesha aliuawa siku chache zilizopita maana ulianza kuharibika,” alisema. 

Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa usiku wa kuamkia Julai 30 mwaka huu, maofisa wa polisi walifika eneo hilo na kuufukua mwili wa marehemu ambao umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top