Waziri wa Nishati, Dk
Medard Kalemani amepiga marufuku Shirika la Umeme (Tanesco) kuuza nguzo za
umeme kwa wananchi akisema tayari Serikali imeshazilipia.
Dk Kalemani ametoa agizo hilo jana Agosti 29 mkoani Njombe alipokuwa wa
uzinduzi wa kiwanda cha kuzalisha na kutibu nguzo cha Qwihaya kilichopo kata ya
Mtwango Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
"Kila mkoa tayari tumeleta fedha kiasi cha Sh2.7 bilioni ambazo ni za
nguzo sasa sitaki kusikia mnawatoza wananchi fedha kwa sababu serikali
imegharamia," amesema Kalemani.
Amewataka wenye viwanda vya kuzalisha nguzo nchini kuzalisha na nguzo za zenge
ili kukabiliana na maeneo korofi wakati huo nguzo za miti zikiendelea
kuzalishwa kwakuwa bado zinahitajika.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa kampuni ya kuzalisha na
kutibu nguzo za umeme Qwihaya, Leonard Mahenda ametangaza neema kwa shule za
msingi, sekondari na zahanati za Wilaya ya Ludewa na Njombe kwa kulipia huduma
ya kuunganishiwa umeme.
Amesema amekua akiiunga mkono Serikali katika kutatua changamoto ikiwa pamoja
na kupatikana kwa nishati ya umeme wa uhakika.
"Waziri nikuahidi
kwamba nitalipia umeme kwa shule za msingi na sekondari pamoja na zahanati za
halmashauri ya wilaya ya Njombe. Pia nisimuache Kaimu Mkuu wa mkoa wa Njombe,
Adrea Tsere ambaye ni mkuu wa wilaya ya Ludewa nako nitalipia shule za msingi
na sekondari kuingizia umeme," amesema Mahenda.
Awali mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe, Valentino Hongoli ambaye
pia alimuwakilisha mbunge wa jimbo la Lupembe, Edwin Swale alimwambia Waziri
Kalemani kuwa, licha ya huduma ya umeme kufika sehemu mbalimbali katika jimbo
hilo lakini bado kuna shule na zahanati hazina umeme.
Post a Comment