
Wakati
mama na dada wa marehemu Hamza Mohammed wakiachiliwa baada ya mahojiano,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema bado
wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo.
Hamza
aliuawa na polisi Agosti 25, mwaka huu baada ya kuwaua kwa risasi askari wanne,
watatu kati yao wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, jirani na
ulipo Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.
Kufuatia
tukio hilo Jeshi la Polisi liliwakamata ndugu kadhaa wa Hamza waliokuwa jijini
na Dar es Salaam na wengine Chunya mkoani Mbeya.
Hata
hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu watu waliokamatwa kutokana na tukio hilo
jana, Kamanda Muliro alisema; “Jamani nyie hamtaki tupeleleze? Ni sahihi tuseme
hadi wapo mahabusu namba ngapi? Ametoka au hajatoka? Ndugu yangu Mwananchi!”
Wakati
Muliro akisema hayo, Msemaji wa familia ya Hamza, Abdul-rahman Hassan
aliliambia Mwananchi kuwa watu takribani saba wakiwamo mama na dada wa Hamza
wameachiwa na wengine watano wanaendelea kushikiliwa na polisi.
Hayo
yamebainika ikiwa ni siku moja, baada ya mwili wa Hamza kuzikwa juzi usiku
katika makaburi ya Kisutu Jijini Dar es Salaam.
“Kati
ya waliokuwa wamekamatwa ndugu walikuwa mama na dada yake tu, wengine ni
marafiki na jamaa. Walioachiwa ni kama saba na wengine watano bado wanaendelea
na mahojiano na polisi...,” alisema Hassan.
Gazeti
hili jana lilimnukuu Hassan, nduguye Hamza, akidai walichelewa juzi kuzika hadi
usiku kwa sababu mwili huo ulikuwa unatolewa risasi.
Alipoulizwa
kuhusu idadi ya risasi zilizotolewa kwenye mwili huo jana, Kamanda Muliro
alisema hawezi kujibu swali hilo, bali anachofahamu ni kuwa juzi polisi
walikabidhi mwili huo kwa ndugu zake kwa ajili ya maziko.
“Itoshe
kujua mwili wao tuliwakabidhi, sasa kama wamezika au hawakuzika, kuna maswali
ni yangu, mengine sio ya kwangu. Sawasawa uniulize wamezika au hawakuzika, sasa
nitakujibu nini hapa,” alisema Muliro.
Hata
msemaji wa familia hiyo alisema hawezi kujua mwili wa Hamza ulikutwa na risasi
ngapi ingawa alisema walichelewa kuuzika kwa sababu ulikuwa ukitolewa risasi.
Mwili
huo ulitakiwa kuzikwa saa 7 mchana, lakini ukazikwa saa mbili usiku.
Hatua
ya mwili huo kuzikwa usiku inaelezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza
la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka kuwa ni ya kawaida, kwa
kuwa utaratibu wa kuzika unafanyika wakati wowote ilimradi makaburi husika yawe
na taa, akisema hilo ndiyo jambo muhimu katika maziko.
Sheikh
huyo anafafanua kuwa ikiwa mwili wa marehemu una kitu kinachowezekana kutolewa
kinatakiwa kutolewa kabla ya kuzikwa.
“Lakini
kama hakiwezekani kinaachwa. Mfano maiti ya ajali yenye vyuma vimemuingia,
watafanya kila liwezekanalo kuondolewa, hawezi kuzikwa navyo na ndivyo
walipoona kuna risasi imemuingia waliitoa,” alisema Sheikh Mataka aliyeongoza
mazishi ya Hamza.
Hakuacha mke, mtoto
Katika
hatua nyingine, Msemaji huyo wa familia alisema Hamza hakuacha mke wala mtoto
na wakati wote alikuwa akiishi na mama yake eneo la Upanga na kila aliporudi
kutoka Mbeya alifikia pale.
“Hana
mke wala mtoto, alikuwa akija anafikia kwa mama yake, anakaa wiki mbili, tatu
au moja anaondoka kwenda Mbeya kwenye shughuli zake.
Kuhusu
vitu vilivyobebwa na jeshi la polisi siku walipofanya ukaguzi alisema hana
uhakika ni vitu gani huku akibainisha kuwa ni vile vilikuwa vinahusiana na
Hamza.
Uchunguzi wa kina
Agosti
27, 2021 katika ibada ya kuaga askari waliopoteza maisha katika tukio hilo,
Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene alisema uchunguzi wa kina
utafanyika ili kubaini sababu za Hamza kufanya mauaji hayo na taarifa rasmi
itatolewa ikiwa na mapendekezo ya nini kifanyike kwa siku za usoni yanapotokea
matukio yanayofanana na hilo.
Siku moja baadaye Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro alisema mwili wa Hamza watawakabidhi ndugu zake baada ya polisi kumaliza kazi yao wameshaufanyia kazi.
Post a Comment