Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limesitisha ibada iliyokuwa ikiendelea katika Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Rungwe kufuatia vurugu zilizowahusisha waumini wa kanisa hilo kumkataa Askofu wao, Edward Mwaikali huku likieleza kuufahamu mgogoro huo wa muda mrefu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema tukio hilo limetokea muda mfupi baada ya kuanza kwa ibada na polisi walipata taarifa na kuwahi kudhibiti vurugu hizo kwa kumtoa askofu ndani ya kanisa baada ya waumini kupandwa jazba.
Matei amesema miongoni mwa sababu zilizosababisha vurugu hizo ni kumtuhumu askofu huyo kuhamisha mali za Kanisa la KKKT Dayosisi ya Rungwe kuzipeleka Kata ya Ruanda jijini hapa.
Amesema sababu nyingine ni mgogoro wa muda mrefu kati ya askofu huyo na wachungaji wa kanisa hilo ambao walipokuwa wakimshauri alikuwa akiwahamisha vituo vya kazi au kuwaondoa kabisa jambo ambalo waumini hawakukubaliana nalo na kueleza kutomhitaji kuendelea kutoa huduma.
"Huu ni mgogoro wa muda mrefu sana na polisi tuliusikia kwani askofu huyo amekuwa akitumia matakwa binasfi kuliendesha kanisa na anaposhauriwa hataki mpaka waumini wameamua kufanya vurugu leo, Agosti 22. Ni jambo walilolivumilia kwa muda mrefu," amesema Matei.
Kamanda huyo amefafanua kuwa baada ya askofu kuondolewa kanisani hapo polisi wamewatuliza waumini na hakuna madhara yoyote yaliyojitokeza wala mtu kushikiliwa kuhusiana na tukio hilo.
“Jeshi la Polisi tunaendelea kuchunguza ili kujua kwa nini waumini wamefanya uamuzi huo licha ya baadhi ya sababu za mgogoro huo kubainika na waumini kusitisha ibada kwa muda jambo ambalo halimpendezi Mungu," amesema kamanda Matei.
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment