} });
 

 

Wakati kukiwa na malalamiko ya wananchi kuhusu mfumo wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa, Serikali imesema vitambulisho 1,300,000 vilivyotengenezwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) havijachukuliwa na wahusika. 

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Mwanza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akitoa taarifa ya wiki ya utendaji wa Serikali. 

Alisema baadhi ya vitambulisho hivyo vimeshapelekwa kwenye ofisi za kata nchi nzima. 

Msigwa alisema hadi kufikia Ijumaa Oktoba 16, 2021 Watanzania zaidi ya milioni 22 walikuwa wamehakikiwa taarifa zao kwa ajili ya kupatiwa kitambulisho hicho. 

Alisema Serikali inaendelea kuandaa mfumo rafiki utakaorahisisha kazi ya utengenezaji na utoaji wa vitambulisho hivyo ndani ya mwaka mmoja. 

“Nikitoka hapa nitalifuatilia ili kujua limefikia wapi, lakini lengo letu ni kuhakikisha tunaweka mifumo ambayo ni rafiki na wezeshi ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata vitambulisho,” alisema Msigwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari nchini (UTPC) Abubakar Karsan, aliiomba Nida kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaojitokeza kuomba kitambulisho hicho. 

“Mimi ni Mtanzania, nilipofika pale Nida nilisumbuliwa sana kiasi kwamba nikaanza hadi kukata tamaa sababu kuu ya kunizungusha hivyo ni rangi yangu. Sasa ukipima kuna watu wengi sana wanaokata tamaa kufuatilia kitambulisho hicho kutokana na usumbufu wanaoupata,” alisema Karsan. 

Ugonjwa wa Uviko - 19

Msigwa alisema Tanzania inatarajia kupokea dozi 500,000 za chanjo ya Uviko-19 aina ya Pfizer kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ikiwa ni sehemu ya mpango wa Covax. 

Alisema hadi kufikia Oktoba 15, 2021 Watanzania 940,000 walikuwa wamepatiwa chanjo aina ya Johnson & Johnson inayotolewa mara moja kwa dozi. 

“Tumetoka kupokea dozi 1,065,000 za Sinopharm ambazo nazo tunaamini watu watajitokeza kwa wingi kuchanja mara mbili kwa sababu hizi zinatolewa mara mbili tofauti na ilivyokuwa Johnson & Johnson,” alisema Msigwa. 

Aliongeza; “Tunaamini kama utaratibu wa kinga unavyosema kwamba, angalau asilimia 60 ya Watanzania wakipatiwa chanjo ya ugonjwa huo, nchi yetu itakuwa salama,” 

Suala la machinga

Alipoulizwa kuhusu na malalamiko ya baadhi ya machinga kuhamishwa kwa nguvu, huku bidhaa zao zikiharibiwa, Msigwa alisema Serikali ilitoa maelekezo kwa viongozi wa halmashauri zote nchini kuepuka matumizi ya nguvu na kuwapanga wafanyabiashara hao kwa utaratibu. 

Alitaja baadhi ya vigezo vya kuzingatia katika eneo wanalohamishiwa wafanyabiashara hao kuwa na huduma za msingi ikiwemo vyoo, maji na linaloweza kufikiwa na wateja kwa urahisi. 

“Kama kuna malalamiko ya watu kutumia nguvu kuwahamisha machinga hayo siyo maelekezo ya Serikali na naomba hilo suala nilichukue kwa ajili ya kwenda kulifanyia kazi ili tuweze kulitatua,” alisisitiza Msigwa.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top