} });
 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, limemhoji Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole kwa tuhuma za kupiga na kujeruhi, huku likiwatafuta watu wengine wawili wanaodaiwa pia kuhusika katika tukio hilo.

Mwenisongole na wenzake, wanatuhumiwa kumpiga Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Mbozi, Ignas Kinyowa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janneth Magomi ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 4, 2021.

Hata hivyo, Mwananchi Digital ilimtafuta mbunge huyo azungumzie sakata hilo naye amesema, “ anashangaa kuitwa na polisi kuwa yeye ndiye mtuhumiwa."

Amedai kuwa Katibu wa UVCCM akiwa na wenzake ndiyo waliopanga kumdhuru, lakini walizidiwa nguvu na vijana wake. "Niliomba msaada wa Polisi, lakini hawakunisaidia, nashangaa polisi wanaponiita mimi ni mshitakiwa ambaye nimemshambulia katibu huyo," amedai.

Lakini kamandaMagomi amesema mbunge huyo walimshikilia tangu jana jioni na alihojiwa hadi Saa 3 usiku na baadaye aliachiwa kwa dhamana. 

Kamanda Magomi amesema Mwenisongole anadaiwa kumpigia simu katibu huyo na kumtaka aende nyumbani kwake eneo la Ichenjezya akakutane na Polisi wazungumze kuhusiana na kuchomwa moto kwa gari la mbunge huyo na watu wasiojulikana.

Gari la Mwenisongole lilichomwa moto Jumamosi usiku nyumbani kwake yeye akiwa amelala ndani.

“Baada ya Katibu huyo wa UVCCM kufika nyumbani kwa mbunge, akaanza kushambuliwa na watu wawili wanadaiwa kutokea kwenye gari la mbunge huyo,” amedai kamanda huyo.

Kutokana na tukio hilo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Songwe,  Andrew Kadege amelaani kitendo hicho alichokiita kuwa ni cha kihuni na cha udhalilishaji.  

“Hatuwezi kuruhusu haya yaendelee sababu CCM sio chama cha siasa za kihuni, tuna taratibu zetu, kanuni, miongozo na katiba katika kushughulikia changamoto mbalimbali za ndani,” amesema Kadege.

Ametoa rai kwa Jeshi la Polisi, kuwakamata wahusika wote walioshiriki kufanya kitendo hicho alichokiita kuwa ni cha jinai na wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi. 

Lakini mbunge huyo katika andiko lake aliloliweka katika mtandao wake wa kijamii,  ameandika kuwa vijana wake wamefanikiwa kuwadhibiti watu wawili ambao walitaka kumshambulia leo Saa tano asubuhi.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top