} });
 

 

Utafiti wa afya ya uzazi na mtoto, utakaofanyika kuanzia Februari 2022, unatarajiwa kuja na taarifa ya matokeo ya idadi na asilimia ya wanaume wanaonyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya kikatili nchini. 

Hayo yamebainishwa Jumanne Oktoba 19, 2021 na Mtakwimu Mkuu wa Serikali,  Dk Albina Chuwa wakati wa uzinduzi na mafunzo ya utafiti wa majaribio wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya maleria, uliofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu cha ushirika Moshi, mkoani Kilimanjaro. 

Dk Chuwa amesema utafiti huo unalenga kuja na taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wanaume, hali ya udumavu kwa watoto pamoja na vifo vya watoto wachanga. 

"Utafiti huu wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya maleria wa mwaka 2021-2022, ni utafiti wa sita kufanyika nchini, unalenga kutoa viashiria, vitakavyotoa majawabu katika sekta ya afya kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo hali ya lishe na udumavu kwa watoto. 

 Amesema katika utafiti huo pia tunalenga kuangalia hali ya vifo vya watoto wachanga na pia tunaenda kukusanya taarifa za unyanyasaji kwa wanawake na wanaume nchini. 

"Tunataka tupate taarifa ya wanaume ambao wananyanyaswa, yaani tupate ni asilimia ngapi ya wanaume wanaonyanyasika nchini, maana tafiti nyingine tumekuwa tukifanya tukitafuta tu wanawake wanaonyanyasika, lakini safari hii, tutakuja pia na taarifa ya wanaume,” amesema.

Akizindua mafunzo ya utafiti huo, Waziri wa Afya nchini Tanzania Dk Dorothy Gwajima, amesema sekta ya Afya imekuwa kwa asilimia 4.8 wakati pato la taifa kwa kipindi hicho likikuwa kwa asilimia 4.3.

Aidha ametumia pia nafasi hiyo, kuwataka washiriki wa utafiti huo, kuhakikisha wanafahamu vizuri namna ya kuwahoji walengwa kwa upole na upendo, ili kuwezesha kupatikana kwa taarifa bora na sahihi.

"Fanyeni kazi kwa bidii na kujituma, mkakusanye taarifa sahihi na bora zitakazowezesha kupangwa kwa mipango ya maendeleo, maana natambua lengo la utafiti huu, ni kuiwezesha serikali na wadau wengine kupata taarifa sahihi." 

Washiriki wa utafiti huo ni wauguzi, wanasayansi wa maabara na watakwimu, ambapo kaya 16,354, zinatarajiwa kufikiwa na utafiti huo.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top