} });
 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya wabunge wakati wa maswali ya papo hapo kwa bunge jijini Dodoma.

Mkutano wa tano wa Bunge ulimalizika jana ukihitimisha uhai wa mwaka mmoja wa Bunge la 12 ambalo lilijaa minyukano ya ndani na nje likiwa limejadili hoja na miswada mbalimbali, ikiwamo iliyokosolewa na wananchi na kufanyiwa marekebisho.

 

Mbali na hayo, Bunge hilo chini ya Spika Job Ndugai limekabiliana na mchangamoto kadhaa za kisiasa huku baadhi ya wabunge wakiwemo mawaziri wakifariki dunia.

 

Wakati likiahirishwa jana baada ya kukaa vikao tisa, kumekuwa na maoni tofauti kuhusu nafasi ya mhimili huo, wajibu na hadhi yake huku mkuu wake, Spika Job Ndugai akiwa mstari wa mbele kulitetea na kuwaonya wote wanaolikosoa.

 

Kwa upande mwingine, Ndugai amenukuliwa mara kadhaa akitoa kauli za ama kuishauri au kuikosoa Serikali na wakati mwingine kuwaonya na kuwatisha wakosoaji wa chombo hicho.

 

Kauli ya karibuni kabisa ya Ndugai ni ya juzi alipoeleza alichokiita “onyo la mwisho” kwa mwanasiasa na mwanahabari nguli, Jenerali Ulimwengu akimtuhumu kutoa maeneo ya rejareja ya kulikashifu Bunge.

 

Ndugai alihitimisha kwa kusema “akiendelea tutashughulika naye ndani na nje ya Bunge ikiwemo mahakamani.”

 

Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wabunge nao hawako nyuma wanaibuka na hoja za kuibana Serikali, ingawa wachambuzi wanaona kuwa bado hitimisho la mijadala ni kuunga mkono masuala mengi kama si yote yanayowasilishwa na Serikali, hata yale ambayo baadaye huonekana mwiba na kubadilishwa.

 

“Naona wanafungua milango ya kukosolewa zaidi. Nadhani wafanye vitu ambavyo vitawapambanua, waache kubishana na wadau,” alisema Dk Paul Loisulie ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, alipozungumza jana.

 

Hatua ya Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kusimama bungeni na kutaka deni la taifa lichunguzwe kwa madai kuwa fedha zilizokopwa kipindi cha miaka mitano iliyopita zilikuwa na usiri mkubwa ni mfano wa wabunge kuamka na kuanza kuonyesha sura ya uwajibikaji.

 

Kauli za Spika      

Katikati ya mwaka wa kwanza wa Bunge la 12, si wabunge tu walioanza kutoa kauli thabiti za kuikosoa Serikali, hata Ndugai mwenyewe amethibitisha hilo kwa kutoa kauli na maelekezo kwa Serikali juu ya masuala kadhaa ambayo kwa mtazamo wake anaona hayako sawa.

 

Baadhi ya watu wamekuwa wakizitazama kauli hizo kwa sura tofauti, baadhi wakiziunga mkono na wengine wakizishangaa na wakidai amebadilika, jambo ambalo limefanya kauli hizo kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii kama Twitter na YouTube.

 

Miongoni mwa kauli alizozitoa zikaibua mjadala ni ile ya Septemba ya kueleza kushtushwa jinsi sheria inayotaka mkulima kulipa ushuru wa bidhaa kwa asilimia mbili kwa TRA ilivyopitishwa wakati jambo hilo lilipita kwenye kamati.

Ndugai alitishia kuivunja kamati ya Bajeti kama haitafanya kazi zake ipasavyo kwa kuwa imeaminiwa na Bunge kufanya kazi kwa niaba yake.

 

“Wajumbe wa kamati ya bajeti mnapaswa kuwa makini sana katika kazi zenu kwa sababu mambo yakifika hapa, sisi tunaiamini kamati.

 

Nyingine ni ya Mei, mwaka huu wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi aliposema kwamba ya “kutaifisha mifugo ndani ya hifadhi ni mbaya, huku akihoji huenda ilipitishwa wakati wabunge wakiwa wamelala au yeye alikuwa safarini siku hiyo.

 

Novemba 4, uliibuka mjadala kuhusu kikokotoo ambapo mbunge wa viti maalumu, Esther Bulaya aliomba mwongozo wa Spika na alipopewa nafasi alidai Sheria ya kikokotoo.

 

Kauli ya mbunge huyo iliungwa mkono na Spika, ambaye alihoji kuna usiri gani ndani ya Serikali ambayo kila wakati inajificha kwenye “mchakato”.

 

Spika alisema kustaafu imekuwa ni giza mbele na kuna watumishi wanatafuta kila namna ili waweze kustaafu hata kabla ya umri wao ili kukwepa kikokotoo ambacho wanajua kitakwenda kuwaumiza.

 

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, oanayehusika na masuala ya kazi, na ajira, Jenista Mhagama alieleza sababu za kuchelewa kwa sheria hiyo kuwa “umakini mkubwa unatakiwa.”

 

makali ya Ndugai hayakuishia hapo, yalitambaa hadi kwenye suala la bima ya afya kwa wote, pale aliposema “chenga za Serikali katika jambo hilo zimekuwa nyingi na ziliwashinda wabunge kwa miaka mitano 2015/20 ambao kati ya mikutano 19 na 20 walikuwa wakiikumbushia lakini hawakufanikiwa.”

 

Ndugai alimwagiza Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Stanslaus Nyongo aanze kuisumbua wizara kwa kuwa akikaa kimya, atafeli kama walivyofeli wenzake waliomtangulia na akaagiza wabunge wanawake wasimamie kwa nguvu jambo hilo.

 

Si hayo tu, Septemba 10, kabla mkutano wa nne kuahirishwa, Ndugai aliwashukia mawaziri kwa kufanya mikutano na warsha nyingi Dar es Salaam badala ya Dodoma ambako ni Makao Makuu ya nchi.

 

Nafasi ya Bunge

Licha ya kauli hizo, Bunge limekuwa likituhumiwa kuwa halijachukua nafasi yake katika kutunga sheria na kuisimamia Serikali.

 

Mathalan, katika suala la tozo za miamala ya simu ambalo liliibua malalamiko ya wananchi baada ya kupitishwa na Bunge katika Bajeti kisha Serikali ikaamua kupunguza tozo hizo na maeneo mengine kama hiyo yanazua maswali kwa mhimili huo.

 

Akifafanua zaidi kuhusu hilo, Dk Loisulie alisema wabunge walipitisha bungeni lakini baada ya wananchi kulalamika nao (wabunge) wakaanza kulalamika. “Mimi binafsi sifurahii namna Bunge letu linavyotenda kazi,” alisema.

 

Naye Bubelwa Kaiza, mchambuzi mwingine wa siasa na masuala ya utawala bora, alisema licha ya majukumu ya msingi ya Bunge, limekuwa halitekelezi mambo hayo kikamilifu.

 

“Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu masuala ya Katiba Mpya, kila kona utasikia Katiba Mpya lakini Bunge limekaa kimya. Liliibuka suala la tozo kwenye miamala ya simu, watu wakataka Serikali iondoe tozo hizo lakini Bunge lilikaa kimya,” alisema Buberwa.

 

Vilevile, Buberwa alisema Bunge limeshindwa kuiwajibisha Serikali ya awamu ya sita kama ilivyokuwa wakati wa awamu ya tano kwa sababu Serikali imekuwa ikifanya mambo yake bila kuhojiwa na Bunge.

 

“Limekuwa ni Bunge la chama kimoja na watu waliaminishwa kwamba Bunge likiwa la chama kimoja mambo yatakwenda haraka lakini tunaona jinsi mambo yanavyokwenda, Bunge haliiwajibishi.

 

Akiwa na mtazamo kama huo, mbunge wa zamani wa jimbo la Kaliua, Magdalema Sakaya alisema Bunge hili limeonekana kutochangamka kama mabunge yaliyopita kwa sababu limejaa wabunge wa chama kimoja.

 

“Kwenye hili suala la tozo ambalo liliibua hisia za wananchi, ingekuwa ni Bunge lililopita, I am sure (nina uhakika) lisingepita,” alisema Sakaya na kusisitiza kwamba kwa uzoefu wake anaona pengo kubwa kati ya Bunge hili na yaliyopita.

 

Akiwa na mtazamo tofauti, mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, Angela Akilimali alisema Bunge linaongozwa kwa kanuni zake, hivyo haoni kasoro zinazodaiwa na baadhi ya watu kwa kuwa limekuwa likitekeleza majukumu yake.

 

Hata hivyo, alisema sheria zenye upungufu zinazopitishwa na Bunge si kielelezo cha kwamba Bunge ni dhaifu, bali ni uelewa mdogo wa baadhi ya wabunge ambao wanapitisha jambo bila kusoma kwa makini,” alisema.

soma habari kila siku kazi yetu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 305 957 #NURU YA KRISTO INAKUANGAZIA

Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top