
Baada ya mapumziko ya
mwisho wa wiki, leo kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na wenzake watatu inaendelea.
Mbowe na
wenzake wanashtakiwa kwa tuhuma za ugaidi, kesi inayoendelea kusikilizwa katika
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.
Katika mwendelezo huo,
upande wa mashtaka unatarajiwa kuendelea kutoa ushahidi na Mahakama inatarajiwa
kupokea ushahidi wa shahidi wa nane kati ya mashahidi 24 .
Shahidi wa
mwisho kabla ya leo (wa saba) alikuwa Inspekta Mahita Omar Mahita, aliyetoa
ushahidi wake Ijumaa iliyopita. Inspekta Mahita alikuwa miongoni mwa kikosi cha
maofisa wa Polisi kutoka Arusha kilichowatia mbaroni washtakiwa wawili katika
kesi hiyo.
Kulingana na
aina ya ushahidi wake, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala
alitumia saa 2:25 kumhoji maswali mbalimbali shahidi huyo kuhusiana na ushahidi
wake, muda ambao ni mrefu zaidi kutumiwa na wakili mmoja kumhoji shahidi tangu
kesi hiyo ianze kusikilizwa Septemba 15, mwaka huu.
Wakili Kibatala
alilieleza Mwananchi kuwa alitumia muda mwingi zaidi kumhoji shahidi huyo
kuliko mashahidi wengine kutokana na ushahidi wake ambao alisema uligusa maeneo
mengi.
Alieleza
mashahidi wengine ambao itakapofika zamu yao kutoa ushahidi atatumia muda
mwingi kuwabana kwa maswali ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jumanne na
Koplo Goodluck, ambao pia walikuwa katika timu hiyo iliyowatia mbaroni
watuhumiwa, pamoja na Luteni Denis Leo Urio.
Luteni Urio
ni Ofisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), kutoka kikosi Maalum (Special Force) au
92 KJ yaani kikosi cha makomandoo, kilichoko Ngerengere eneo la Sangasanga
mkoani Morogoro.
Huyu ni
shahidi katika kesi hiyo, kwani mujibu wa maelezo ya maandishi ya mashahidi wa
upande wa mashtaka, ndiye anadaiwa kuhusika kuibua tuhuma zinazowakabili
washtakiwa.
Wakati kesi
hiyo ikisubiriwa kuendelea leo, swali na ama shauku ya wadaawa, hususan
washtakiwa na mawakili wao pamoja na wadau wanaofuatilia kesi hiyo ni kujua ni
nani shahidi wa nane na kusikia ni ushahidi gani atakaoutoa.
Mbali na
Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan, Adamu Hassan
Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.
Washtakiwa hao watatu walikuwa askari wa JWTZ, 92 KJ, Ngerengere ambao waliachishwa kwa sababu za kinidhamu.
Post a Comment