![]() |
Makamu Askofu kanisa la Orthodox jimbo la Dar es Salaam, Cleophace Bachuba |
Wamachinga jijini Dar es
Salaam waliohamishwa eneo la Mbuyuni kata ya Wazo Wilaya ya Kinondoni
wanadaiwa kuvamia eneo la kanisa la Orthodox na kuanza kufanya biashara jambo
lililolalamikiwa na uongozi wa kanisa hilo.
Kundi la
wamchinga zaidi ya 200 wamevamia eneo hilo wakidai kuwa ni la wazi linamilikiwa
na Serikali hivyo wanaenda hapo kufanya biashara zao baada ya kufukuzwa
barabarani.
Mwananchi
lilifika eneo hilo na kushuhudia wamachinga hao wakiwa wamejipanga eneo la
mbele la kanisa huku wengine wakijenga vibanda vya kuweka bidhaa zao tayari kwa
kuuza.
Makamu Askofu
wa kanisa hilo jimbo la Dar es Salaam, Cleophace Bachuba amesema kuvamia kwa
wamachinga hao katika eneo lao kumesababisha baadhi ya shughuli za kanisa
kusimama.
Amesema
tayari wameshatoa taarifa kwa uongozi wa Serikali za mtaa na wilaya ambao
uliwarudishia majibu kuwa eneo la kanisa si eneo sehemu ya afanyabiashara
hivyo wavamizi wanapaswa kuondoka kupisha shughuli za kanisa kuendelea.
“Wakati Serikali
inafanya oparesheni ya kuwaondoa wamachinga barabarani ndipo hawa wa eneo la
Mbuyuni wakavamia eneo letu hili la kanisa na kukwamisha shughuli zingine
kuweza kuendelea,” amesema
Paroko wa kanisa hilo,
Padri Frumentios Msuri amesema kanisa hilo la Bikiria la Maria lilijengwa mwaka
1939 na tangu hapo Watanzania, Wagiriki na watu wa aina mbalimbali wamekuwa
wakijitokeza kusali lakini baada ya vurugu hizo wamelazimika kusali Upanga.
Kwa upande
wake mwenyekiti wa wamachinga hao, Kizito Ponsiano amesema wafanyabishara hao
hawafanyi biashara zao katika eneo la kanisa na kusisitiza kuwa eneo hilo sio
lote ni mali ya kanisa.
Hata hivyo
amesema wanauomba uongozi wa kanisa hilo kuwapatia vielelezo vinavyoonesha kuwa
eneo hilo ni mali yao na kwamba wakiviona na kujiridhisha wataondoka na
kutafuta eneo jingine.
Akijibu madai
hayo, mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mbuyuni Salasala, Robart Masawe amesema
katika eneo lake wafanyabiashara wamepangiwa eneo la Benako ambalo lina mgogoro
na eneo la Kisanga ambalo halina choo kwa sasa.
“Diwani
anapambana sasa hivi ili kupatikane choo, tukimaliza kujenga wamachinga hawa
watatolewa na kwenda kupangwa katika eneo hilo wala hakuna tatizo,” amesema
Hata hivyo Masawa amesema eneo waliopo wafanyabiashara hao limejitenga kabisa na kanisa hilo, na kuongeza kuwa mgogoro huo ulipofikia wanaliomba kanisa kuleta vielelezo vyao.
Post a Comment