Mkutano wa tano wa Bunge
ulimalizika jana ukihitimisha uhai wa mwaka mmoja wa Bunge la 12 ambalo lilijaa
minyukano ya ndani na nje likiwa limejadili hoja na miswada mbalimbali, ikiwamo
iliyokosolewa na wananchi na kufanyiwa marekebisho.
Mbali na
hayo, Bunge hilo chini ya Spika Job Ndugai limekabiliana na mchangamoto kadhaa
za kisiasa huku baadhi ya wabunge wakiwemo mawaziri wakifariki dunia.
Wakati
likiahirishwa jana baada ya kukaa vikao tisa, kumekuwa na maoni tofauti kuhusu
nafasi ya mhimili huo, wajibu na hadhi yake huku mkuu wake, Spika Job Ndugai
akiwa mstari wa mbele kulitetea na kuwaonya wote wanaolikosoa.
Kwa upande
mwingine, Ndugai amenukuliwa mara kadhaa akitoa kauli za ama kuishauri au
kuikosoa Serikali na wakati mwingine kuwaonya na kuwatisha wakosoaji wa chombo
hicho.
Kauli ya
karibuni kabisa ya Ndugai ni ya juzi alipoeleza alichokiita “onyo la mwisho”
kwa mwanasiasa na mwanahabari nguli, Jenerali Ulimwengu akimtuhumu kutoa maeneo
ya rejareja ya kulikashifu Bunge.
Ndugai
alihitimisha kwa kusema “akiendelea tutashughulika naye ndani na nje ya Bunge
ikiwemo mahakamani.”
Wakati hayo yakijiri,
baadhi ya wabunge nao hawako nyuma wanaibuka na hoja za kuibana Serikali,
ingawa wachambuzi wanaona kuwa bado hitimisho la mijadala ni kuunga mkono
masuala mengi kama si yote yanayowasilishwa na Serikali, hata yale ambayo
baadaye huonekana mwiba na kubadilishwa.
“Naona
wanafungua milango ya kukosolewa zaidi. Nadhani wafanye vitu ambavyo
vitawapambanua, waache kubishana na wadau,” alisema Dk Paul Loisulie ambaye ni
mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, alipozungumza jana.
Hatua ya
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kusimama bungeni na kutaka deni la taifa
lichunguzwe kwa madai kuwa fedha zilizokopwa kipindi cha miaka mitano iliyopita
zilikuwa na usiri mkubwa ni mfano wa wabunge kuamka na kuanza kuonyesha sura ya
uwajibikaji.
Kauli za
Spika
Katikati ya mwaka wa
kwanza wa Bunge la 12, si wabunge tu walioanza kutoa kauli thabiti za kuikosoa
Serikali, hata Ndugai mwenyewe amethibitisha hilo kwa kutoa kauli na maelekezo
kwa Serikali juu ya masuala kadhaa ambayo kwa mtazamo wake anaona hayako sawa.
Baadhi ya
watu wamekuwa wakizitazama kauli hizo kwa sura tofauti, baadhi wakiziunga mkono
na wengine wakizishangaa na wakidai amebadilika, jambo ambalo limefanya kauli
hizo kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii kama Twitter na YouTube.
Miongoni mwa
kauli alizozitoa zikaibua mjadala ni ile ya Septemba ya kueleza kushtushwa
jinsi sheria inayotaka mkulima kulipa ushuru wa bidhaa kwa asilimia mbili kwa
TRA ilivyopitishwa wakati jambo hilo lilipita kwenye kamati.
Ndugai
alitishia kuivunja kamati ya Bajeti kama haitafanya kazi zake ipasavyo kwa kuwa
imeaminiwa na Bunge kufanya kazi kwa niaba yake.
“Wajumbe wa
kamati ya bajeti mnapaswa kuwa makini sana katika kazi zenu kwa sababu mambo
yakifika hapa, sisi tunaiamini kamati.
Nyingine ni
ya Mei, mwaka huu wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi
aliposema kwamba ya “kutaifisha mifugo ndani ya hifadhi ni mbaya, huku akihoji
huenda ilipitishwa wakati wabunge wakiwa wamelala au yeye alikuwa safarini siku
hiyo.
Novemba 4,
uliibuka mjadala kuhusu kikokotoo ambapo mbunge wa viti maalumu, Esther Bulaya
aliomba mwongozo wa Spika na alipopewa nafasi alidai Sheria ya kikokotoo.
Kauli ya
mbunge huyo iliungwa mkono na Spika, ambaye alihoji kuna usiri gani ndani ya
Serikali ambayo kila wakati inajificha kwenye “mchakato”.
Spika alisema
kustaafu imekuwa ni giza mbele na kuna watumishi wanatafuta kila namna ili
waweze kustaafu hata kabla ya umri wao ili kukwepa kikokotoo ambacho wanajua
kitakwenda kuwaumiza.
Hata hivyo,
Waziri wa Nchi, oanayehusika na masuala ya kazi, na ajira, Jenista Mhagama
alieleza sababu za kuchelewa kwa sheria hiyo kuwa “umakini mkubwa unatakiwa.”
makali ya
Ndugai hayakuishia hapo, yalitambaa hadi kwenye suala la bima ya afya kwa wote,
pale aliposema “chenga za Serikali katika jambo hilo zimekuwa nyingi na
ziliwashinda wabunge kwa miaka mitano 2015/20 ambao kati ya mikutano 19 na 20
walikuwa wakiikumbushia lakini hawakufanikiwa.”
Ndugai
alimwagiza Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Stanslaus Nyongo
aanze kuisumbua wizara kwa kuwa akikaa kimya, atafeli kama walivyofeli wenzake
waliomtangulia na akaagiza wabunge wanawake wasimamie kwa nguvu jambo hilo.
Si hayo tu,
Septemba 10, kabla mkutano wa nne kuahirishwa, Ndugai aliwashukia mawaziri kwa
kufanya mikutano na warsha nyingi Dar es Salaam badala ya Dodoma ambako ni
Makao Makuu ya nchi.
Nafasi ya Bunge
Licha ya
kauli hizo, Bunge limekuwa likituhumiwa kuwa halijachukua nafasi yake katika
kutunga sheria na kuisimamia Serikali.
Mathalan,
katika suala la tozo za miamala ya simu ambalo liliibua malalamiko ya wananchi
baada ya kupitishwa na Bunge katika Bajeti kisha Serikali ikaamua kupunguza
tozo hizo na maeneo mengine kama hiyo yanazua maswali kwa mhimili huo.
Akifafanua
zaidi kuhusu hilo, Dk Loisulie alisema wabunge walipitisha bungeni lakini baada
ya wananchi kulalamika nao (wabunge) wakaanza kulalamika. “Mimi binafsi
sifurahii namna Bunge letu linavyotenda kazi,” alisema.
Naye Bubelwa
Kaiza, mchambuzi mwingine wa siasa na masuala ya utawala bora, alisema licha ya
majukumu ya msingi ya Bunge, limekuwa halitekelezi mambo hayo kikamilifu.
“Kumekuwa na
mjadala mkubwa kuhusu masuala ya Katiba Mpya, kila kona utasikia Katiba Mpya
lakini Bunge limekaa kimya. Liliibuka suala la tozo kwenye miamala ya simu,
watu wakataka Serikali iondoe tozo hizo lakini Bunge lilikaa kimya,” alisema
Buberwa.
Vilevile,
Buberwa alisema Bunge limeshindwa kuiwajibisha Serikali ya awamu ya sita kama
ilivyokuwa wakati wa awamu ya tano kwa sababu Serikali imekuwa ikifanya mambo
yake bila kuhojiwa na Bunge.
“Limekuwa ni
Bunge la chama kimoja na watu waliaminishwa kwamba Bunge likiwa la chama kimoja
mambo yatakwenda haraka lakini tunaona jinsi mambo yanavyokwenda, Bunge
haliiwajibishi.
Akiwa na
mtazamo kama huo, mbunge wa zamani wa jimbo la Kaliua, Magdalema Sakaya alisema
Bunge hili limeonekana kutochangamka kama mabunge yaliyopita kwa sababu limejaa
wabunge wa chama kimoja.
“Kwenye hili
suala la tozo ambalo liliibua hisia za wananchi, ingekuwa ni Bunge lililopita,
I am sure (nina uhakika) lisingepita,” alisema Sakaya na kusisitiza kwamba kwa
uzoefu wake anaona pengo kubwa kati ya Bunge hili na yaliyopita.
Akiwa na
mtazamo tofauti, mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, Angela Akilimali
alisema Bunge linaongozwa kwa kanuni zake, hivyo haoni kasoro zinazodaiwa na
baadhi ya watu kwa kuwa limekuwa likitekeleza majukumu yake.
Hata hivyo,
alisema sheria zenye upungufu zinazopitishwa na Bunge si kielelezo cha kwamba
Bunge ni dhaifu, bali ni uelewa mdogo wa baadhi ya wabunge ambao wanapitisha
jambo bila kusoma kwa makini,” alisema.