
Mbunge wa Viti Maalumu,
Halima Mdee ameibana Serikali akitaka kujua mpaka sasa inadaiwa kiasi gani cha
fedha ambazo imekopa kutoka Mifuko ya Hifadhi za Jamii.
Mdee katika
swali lake bungeni leo Jumanne Juni 14, 2022 pia amehoji ni kiasi gani cha
madeni kimeshalipwa na kwa utaratibu gani.
Akijibu
maswali hayo kwa pamoja, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande
amesema Serikali ilikopa fedha kutoka katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Chande
amesema deni la michango ya wastaafu waliokuwa katika utumishi kabla ya mwaka
1999 na kutaja mchanganuo wa madeni na kiasi kilicholipwa.
Naibu Waziri
huyo amesema Mfuko wa PSSSF ni Sh506.88 bilioni na imeshalipwa Sh500 bilioni
ambazo zimelipwa kwa utaratibu wa kibajeti.
Kuhusu
michango ya wastaafu waliokuwa katika utumishi kabla ya mwaka 1999 amesema
zilikopwa Sh4.46 trilioni huku zikiwa zimelipwa Sh2.17 trilioni kwa utaratibu
wa hatifungani maalumu.
“Aidha kiasi kilichobaki
cha deni la mfuko wa PSSSF Sh6.88 bilioni na michango ya wastaafu Sh2.29
trilioni, zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/23,” amesema.
Amesema
kwenye mfuko wa NSSF Sh292.59 bilioni zilizokidhi vigezo baada ya uhakiki wa
deni la Sh490.16 bilioni zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/23 wakati mfuko
wa NHIF Sh80.68 bilioni zilizokidhi vigezo baada ya uhakiki wa deni la Sh209.72
bilioni zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/23.
Kwa mujibu wa Chande, Serikali itaendelea kuhakiki sehemu iliyobaki ya deni la Mfuko wa NSSF na NHIF ili yaweze kujumuishwa katika mpango wa malipo.
Post a Comment