
Mbunge wa Tarime
Vijijini Mwita Waitara ameingia kwenye mtego wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson
akitajwa kuwa amefanya kosa la utovu mkubwa wa nidhamu.
Hata hivyo
Spika Dk Tulia amesema kwa mtu yeyoyte mwenye afya ya akili asingefanya jambo
kama alilolifanya mbunge huyo ingawa alitangaza kumsamehe.
Dk Tulia
ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumanne Juni 14, 2022 baada ya kipindi cha
maswali na majibu ambapo ameleza masikitiko yake kuwa hakutegemea kama mbunge
mzoefu angefanya jambo lililofanywa na Mwita.
Spika ametaja
kosa la mbunge huyo kwamba, linatokana na kauli yake aliyonukuliwa na moja ya
magazeti (sio la Kampuni ya Mwananchi Communications Limited) akipinga kitendo
cha yeye (Spika) kuagiza Serikali ikachunguze madai yake kwamba wananchi wa
Tarime wanauawa na kuumizwa na watu wa Hifadhi ya Serengeti.
Juni 4, 2022
Spika Dk Tulia aliwapa maagizo wabunge Mwita Waitara na Philip Mlugo kupeleka
kwake ushahidi ndani ya siku nne baada ya wabunge hao kwa nyakati tofauti
kueleza madhara makubwa wanayopata wananchi wao kutokana na wanyama.
Hata hivyo wawili hao
waliwasilisha walichoita ni ushahidi wao kama walivyotakiwa, lakini Juni 9
Spika alitoa taarifa mbele ya Bunge kuwa walichopeleka kwake haikuwa ushahidi
bali ni malalamiko lakini akaagiza Serikali kufanya uchunguzi ndani ya siku 90
na kutoa majibu.
Leo Spika
amesema Mwita alilalamika kupitia gazeti hilo akinukuliwa kusema “Hifadhi ya
Serengeti ni mali ya Serikali, lakini kuruhusu Serikali ikajichunguze yenyewe
siyo sahihi hivyo spika alikosea kwani alipaswa kuunda tume huru ya kibunge
ndiyo ikachunguze,”
Dk Tulia
ameendela kunukuu kwamba mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Ukonga alisema Spika
alishawahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali hivyo anazijua sheria na
kwamba asingeweza kufanya hivyo.
Amesema mbunge
huyo ana uzoefu na anajua kuwa alipaswa kuandika barua kwa kutumia kanuni za
bunge kupeleka malalamiko yake kwa Katibu wa Bunge ili mambo yafanyiwe kazi
kama hakuwa ameridhika.
“Kwa mtu
mwenye afya ya akili alipaswa kutambua kuhusu jambo hili na hata kupongeza
uamuzi wa Spika, huu ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa mujibu wa kanuni zetu na
adhabu yake wabunge mnaitambua,” amesema Dk Tulia.
Hata hivyo ameliambia Bunge kwamba anampa onyo mbunge huyo akimtaka asirudie tena kudharau maamuzi ya spika lakini kwa kosa hilo ametangaza kumsaheme.
Post a Comment