Wakati bei za mafuta
zikiendelea kupaa hapa nchini, matumaini ya kushuka kwa bei ya mafuta ghafi
katika soko la dunia yameanza kuonekana.
Taarifa ya
mtandao wa Trending Economics ilionyesha hadi Julai 06, 2022 bei ya mafuta
ghafi kwa pipa ilikuwa Dola 101.4 (sawa na Sh233,220) ukilinganisha Dola 115.4
(sawa na Sh265,420) mwezi uliopita.
Kushuka kwa
bei ya bidhaa hiyo kwenye soko la dunia kunaashiria uwezekano wa kupungua kwa
bei miezi miwili ijayo kwa mujibu wa Katibu wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa
Mafuta ya Rejareja Tanzania (Tapsoa), Augustino Mmasi.
“Mafuta
tunayotumia sasa yalinunuliwa miezi miwili iliyopita kati ya Aprili na Mei,
hivyo tutanunua sasa na mchakato wa kuyaleta ni baada ya miezi miwili,”
alifafanua Mmasi.
Hata hivyo,
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael
Mgaya alisema bei hizo zinaweza kupungua kama wastani wa bei kwa mwezi mzima
utaendelea kuwa chini.
“Sasa hivi
inawezekana imepungua lakini bei hazitabiriki, kama zitaendelea kupungua basi
kuna uwezekano wa bei kupungua,” alisema.
Kwa bei za mwezi wa nane
Mgaya alisema wastani wa bei kwa mwezi wa sita ilikuwa Dola 115 (sawa na
Sh264,500) kwa pipa ukilinganisha na Dola 104 (sawa na Sh239,200) kwa mwezi wa
tano.
“Kama Serikali
itaendelea kutoa ruzuku ya kiwango hicho (Sh100 bilioni) basi kuna uwezekano wa
bei kuongezeka kwa mwezi wa nane kwani bei iliongezeka mwezi wa sita,” alisema
Mgaya.
Wakati
huohuo, Ripoti ya mapitio ya uchumi kwa Mei 2022 inayotolewa na Benki Kuu
(BoT), ilionyesha kupungua kidogo kwa bei. Pipa liliuzwa Dola 104.2 (sawa na
Sh239,660) kwa Aprili ukilinganisha na Dola 114.4 (sawa na Sh263,120) kwa
Machi.
Takwimu
zinaonyesha bei ya mafuta ilikuwa Dola 85.53 (sawa Sh196,719) kwa Januari, Dola
95.76 (Sh220,248) kwa Aprili.
Sababu ya
kupungua bei kwa Aprili ikinukuliwa kuwa, “Upungufu ukifuatia tangazo la
Marekani na wanachama wengine wa Shirika la Nishati la Kimataifa (IEA) la
kuziomba nchi kutoa mafuta waliyohifadhi ili yaweze kutumika katika kipidi hiki
ambacho Russia ikiwa kwenye vikwazo”.
Jitihada za Serikali
Waziri wa
Nishati, January Makamba alisema licha ya Serikali kutoa ruzuku, inatarajia
kuanza ujenzi wa hifadhi ya kimkakati ya mafuta ya Taifa, kubadilisha
miundombinu ya ushushaji wa mafuta bandarini na mwekezaji ameshapatikana.
“Moja ya
sababu za mafuta kuwa juu ni gharama zinazotozwa kwa meli kukaa muda mrefu
bandarini kwa sababu ya miundombinu hafifu. Bandari yetu kwa sasa imezidiwa na
meli zinakaa muda mrefu, tumepata mwekezaji hivyo tutafumua miundombinu na
kuweka mipya na kuongeza hifadhi,” alisema.
Bei za mafuta
za Julai
Kwa mujibu wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), bei ya petroli
imeongezeka kwa wastani wa Sh226 katika mikoa yote. Takwimu zinaonyesha bei ya
petroli Dar es Salaam imefikia Sh3,220 mwezi huu ukilinganisha na Sh2,994 ya
Juni.
Bei hiyo ni
ya chini zaidi kwa bidhaa hiyo nchini ikilinganishwa na maeneo mengine.
Bei ya lita
moja ya petroli imeongezeka hadi Sh3,214 mkoani Tanga na Sh3,205 mkoani Mtwara.
Kwa upande wa dizeli,
Dar es Salaam bei imeongezeka kwa Sh12 hadi Sh3,143 na mkoani Mtwara
imeongezeka kwa Sh7 na sasa inauzwa Sh3,172, mkoani Tanga bei ya bidhaa hiyo
imepungua kwa Sh8 kwa kila lita na inauzwa Sh3,150.
Licha ya ongezeko hilo,
bei ya dizeli Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo ya chini zaidi nchini ukilinganisha
na bei ya maeneo mengine.
Bei ya mafuta
ya taa imeongezeka kwa asilimia 4.3 kutoka Sh 3,299 kwa lita moja hadi Sh3,442
mwezi Juni kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa
Ewura, bei za mafuta katika maeneo mengine nchini zitategemea na ungezeko la
gharama za usafiri. Bei ya chini zaidi inatarajiwa kuwa Sh3,205 kwa kila lita
mkoani Mtwara.
Bei ya juu
zaidi ya petroli ni Sh3,458 wilayani Kyerwa (Ruberwa) mkoani Kagera. Pia bei ya
juu zaidi ya dizeli ni Sh3,748 na mafuta ya taa ni Sh3,679 kwa kila lita katika
wilaya hiyo.
Msemaji wa
Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) Mustapha Mwalongo ameiomba
Serikali idhibiti bei ya mafuta haraka.
Dereva Gasper
Kunambi alisema biashara yao imekuwa ngumu kutokana na uhaba wa wateja.
Saidi Kipandi dereva wa daladala kati ya Makumbusho hadi Bunju alisema bei za mafuta zinazoendelea kuwaumiza kwa kuwa zimepunguza fedha wanazopata.
Post a Comment