![]() |
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere |
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ameishauri Serikali kuipa nguvu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuajiri watumishi wake watakaoweza kusimamia
uchaguzi kwa haki badala ya kuendelea kutegemea waliopo kwenye mfumo wa
Serikali.
Mei 10, 2019,
Mahakama Kuu ilitoa hukumu ya kubatilisha vifungu vya 7(1) na 7(3) vya sheria
ya uchaguzi vinavyowapa mamlaka wakurugenzi wa miji, wilaya, manispaa na majiji
kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwenye maeneo yao.
Shauri hilo
lilifunguliwa na mwanaharakati wa Katiba, Bob Wangwe akishirikiana na Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Hata hivyo,
Serikali ilikata rufaa kuipinga hukumu huyo na baadaye Oktoba 2019 Mahakama ya
Rufani ikabatilisha uamuzi na hivyo kuruhusu wakurugenzi waendelee kusimamia
uchaguzi.
Pamoja na
uamuzi huo, suala hilo limeendelea kulalamikiwa na na sasa limeibuka mara
kadhaa wakati wa kutoa maoni katika kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia
Suluhu Hassan kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
Miongoni mwa
waliozungumzia suala hilo ni CAG Kichere, ambaye ameungana na viongozi wengine
kupendekeza uwepo muundo wa tume ya uchaguzi utakaoifanya iwe huru na hivyo
kuaminika zaidi.
Wengine waliozungumzia
suala hilo ni Jaji Damian Lubuva na CAG mstaafu, Profesa Mussa Assad ambao pia
kwa nyakati tofauti wameshauri kuhusu uhuru wa Tume hiyo.
Dhana ya mgongano wa masilahi
Akizungumza
Dar es Salaam baada ya kuwasilisha maoni yake, CAG Kichere alisema watumishi wa
Serikali, wakiwemo wakurugenzi (wa halmashauri, miji, majiji na manispaa)
kuendelea kusimamia uchaguzi kunakuwa na kitu kinaitwa passive conflict of
interest (dhana ya mgongano wa masilahi).
Alisema ili
kuondoa dhana tume ya uchaguzi ipewe nguvu ya kuajiri watumishi wake.
Alisema ikiwa
tume itaajiri yenyewe watumishi wake wote, hali hiyo itasaidia kujenga imani
kwa wananchi juu ya taasisi hiyo ambayo alisema kwa sasa imekuwa ikilalamikiwa
na moja ya sababu ni kutumia watumishi walioajiriwa na Serikali, ambao
wanadaiwa kutotenda haki kwenye usimamizi.
“Kwenye
uchaguzi tumetoa maoni yetu jinsi ya kuendesha chaguzi, tunatakiwa kuangalia,
tume inatakiwa iweje na tumependekeza iwe na nguvu ya kuajiri watumishi kwa
kuzingatia vigezo watakavyoweka kusimamia uchaguzi ili kuondoa malalamiko kwa
baadhi ya watu.
“Tumependekeza watumishi
wa tume waajiriwe, iwe ndani au nje, tume ipewe nguvu ya kuajiri watumishi wake
badala ya kuendelea kutegemea watumishi walioko kwenye system (mfumo wa
Serikali), wanatakiwa wawe waajiriwa wa tume ili waweze kusimamia uchaguzi,” alisema.
Kufanya
hivyo, alisema kutaenda kusaidia kuondoa minong’ono na malalamiko kwamba
wakurugenzi wakisimamia uchaguzi wanakuwa na upendeleo kwa baadhi ya wagombea.
“Kunakuwa na
kitu kinaitwa passive conflict of interest, pengine wanaweza wakawa wanafanya
kazi yao vizuri lakini kwa kuwa ni watumishi wa Serikali, watu wakasema
‘wakurugenzi ni waajiriwa wa Serikali na wameteuliwa wanaweza wakawa wana
upendeleo’, lakini kumbe si kweli na wanaweza kuwa wanafanya kazi yao vizuri tu
ila hiyo dhana inaleta hiyo changamoto,” alisema Kichere.
Waombe kazi, wafanyiwe usahili
Wiki
iliyopita, Jaji Lubuva, mwenyekiti mstaafu wa NEC na aliyepata kuwa mwanasheria
mkuu wa Serikali Zanzibar na baadaye Muungano, alishauri Serikali kuangalia
utaratibu mpya wa upatikanaji wa watendaji wakuu wa tume ya uchaguzi.
Alishauri
liundwe jopo chini ya jaji mkuu la kuwafanyia usahili waombaji wa kazi hizo,
kisha jopo hilo liwasilishe kwa Rais majina ya watakaopita katika mchujo kwa
ajili ya uteuzi.
“Wakisharidhika
huyu au yule anatufaa kuwa mwenyekiti au Kamishina, majina hayo ndiyo yapelekwe
kwa Rais afanye uteuzi. Hii itasaidia kuendana na imani ya wahusika,” alisema
Jaji Lubuva, aliyepata pia kuwa waziri wa sheria.
Hata CAG
mstaafu Profesa Mussa Assad alipotoa maoni yake alishauri kwamba katika
kutengeneza misingi ya utawala bora, ni vizuri kuboresha kwa kuangalia mifumo
au miundo mizuri na nafasi ambazo zipo kuhakikisha zinajazwa kwenye huo muundo.
Alishauri watumishi
wapatikane wenye sifa nzuri na wasiokuwa waongo, akitolea kwenye Tume ya
Uchaguzi.
Alisema
taasisi hiyo ni muhimu na nafasi hizo zinatakiwa kujazwa kisheria na si
vinginevyo na watu wote wanatakiwa kukubaliana nani anastahili kukaa katika
nafasi fulani kulingana na elimu na uzoefu wake.
Wakati huohuo, CAG Kichere alitumia fursa hiyo kuvishauri vyama vya siasa kupitia mikutano yao ya kisiasa kutengeneza utaratibu wa kutoa hoja na mapendekezo ya namna ya kujenga na kuimarisha uchumi wa Taifa lao.
Post a Comment