Wakati
Jeshi la Polisi likieleza jinsi mkaguzi msaidizi wa polisi Grayson Mahembe
alivyojinyonga akiwa mahabusu, hatua iliyoibua hisia na maswali kadhaa, baba
mzazi wa marehemu Gaitan Mahembe, ameendelea kulitaka jeshi hilo kuweka wazi
uchunguzi wa kifo cha mwanawe.
Mahembe
alikuwa miongoni wa maofisa wa jeshi hilo wanaodaiwa kumnyang’anya Sh33.7
milioni mfanyabiashara wa madini Mussa Hamis, kisha kuutupa mwili wake vichakani
huku katika kijiji cha Namgogoro mkoani Mtwara Januari 5, 2022.
Taarifa ya Polisi
Taarifa
iliyotolewa Jumatatu na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imesema kuwa
Grayson Mahembe aligundulika kujinyonga Januari 22, 2022 akiwa mahabusu kutokana
na tuhuma za kumnyang’anya fedha na kisha kumuua Mussa Hamis na kuutupa mwili
wake.
“Baada
ya kufanya tukio hilo la ukiukwaji wa viapo vyao, akiwa na wenzake, wakiwamo
maofisa, wakaguzi na askari wengine, hawakutoa taarifa kwa viongozi wao kwa
sababu walifahamu kuwa wamefanya hivyo kwa nia ovu, kwa tamaa zao na kinyume
cha sheria za nchi,” ilisema taarifa ya Misime.
Iliendelea
kusema kuwa, baada taarifa za tukio hilo kuwafikia viongozi wa Polisi Mkoa wa
Mtwara, walianza uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwakamata askari waliokuwa
wanatuhumiwa.
“Miongoni
mwa askari waliokamatwa na kuanza kuhojiwa ni huyo mkaguzi msaidizi wa Polisi
Grayson Mahembe. Alipohojiwa alieleza mtiririko mzima wa matendo waliyofanya na
mwisho akawapeleka maofisa waliokuwa wanafanya uchunguzi wa tukio hili sehemu
walipoutupa mwili wa Mussa Hamis na maelezo yake yaliandikwa na yakawa
yamerandana na ushahidi mwingine uliokuwa umekusanywa,” ilisema taarifa ya
Misime.
Alisema
baada ya hatua hiyo aliwekwa katika mahabusu ya peke yake kama walivyofanyiwa
wenzake ambao taarifa inasema ilibidi wapelekwe mahabusu za Mkoa wa Lindi ili
wasiharibu ushahidi uliokuwa ukiendelea kukusanywa. Ni maelezo yanayojibu swali
marehemu aliwezaje kujinyonga akiwa mahabusu.
“Baadaye
ndipo ikagundulika Grayson Mahembe amejinyonga. Baada ya tukio hilo taratibu
zote za ukaguzi wa matukio zilifuatwa ikiwemo kupiga picha na zipo kwa kutumia
wataalam wa kuchunguza matukio kama hayo’ ilisema ikiwa ni kujibu swali kuhusu
picha za marehemu akiwa amejinyonga.
Alisema
Mahembe asingeweza kuzikwa kijeshi kwa kuwa alipoteza sifa ya kufa kishujaa.
Familia yataka ripoti iwekwe wazi
Akizungumza
kwa simu jana baada ya taarifa ya Polisi kutolewa, baba mzazi wa Grayson,
alisema bado wanalitaka jeshi hilo kuweka wazi taarifa ya kifo cha mtoto wao.
“Postmoterm
hatujapewa na mimi kinachoniuma zaidi ni kwamba, ndugu yangu alikuwepo kule kwa
nini hakuitwa kwenda kushuhudia mtu aliyejitundika, kwa nini picha yeyote ya
mtu aliyejitundika haikuonyeshwa, hiyo wamefafanua nini?” alihoji Mahembe.
Alimtaja
ndugu yake aliyesema ni ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akisema
walimtuma kufuatilia tukio hilo, lakini alipelekwa kuonyeshwa mwili ukiwa
chumba cha maiti.
“Ninachosikitika
ni kwamba amekwenda kuitwa kwenda kuona mwili wa marehemu Ligula hospitali
basi, lakini sehemu ya tukio alipojinyongea hakuna anayejua,” alisema.
Aliendelea
kusema kuwa wamewatuma baadhi ya ndugu kuchukua vitu vya marehemu na kufuatilia
zaidi.
Alipoulizwa
kuhusu madai hayo ya familia, Misime alisema hakuna aliyehitaji kuiona hiyo
taarifa ya uchunguzi au picha kwa kufuata taratibu akanyimwa.
“Kama
wanahitaji kuiona na kuona picha wafuate taratibu na siyo kama mmoja alivyosema
hakuna picha iliyoonekana katika chombo chochote cha habari kwa maana kwamba
alitaka zisambazwe kwenye vyombo vya habari wakati kufanya hivyo si sahihi na
ni kinyume na sheria,” alisema.
Kuhusu
mtu kujinyonga akiwa mahabusu, alisema: “Binadamu aliyekata tamaa ya maisha,
mwenye msongo wa mawazo na anayefikiria aibu au adhabu atakayoipata kutoka na
kile alichofanya, kama ameweka nia, hachagui eneo la kutimiza lengo lake,
alisema.